MRADI wa Mabasi ya Haraka Dar es Salaam (DART) umezidi kupigwa kalenda ambapo sasa Mkuu wa Wakala wa Usafiri wa Haraka, Cosmas Takule, amekiri kutojua lini mradi huo utaanza. Takule aliliambia gazeti hili mwishoni mwa wiki kuwa miundombinu mingi ya mradi huo haijakamilika hali inayosababisha kushindwa kuanza kwa mradi huo.
Awamu ya kwanza ya mradi huo ambao ndio tegemeo kubwa la kuondoa kero ya msongamano wa magari kwa wakazi wa Dar es Salaam, ilikuwa ikamilike mwezi huu na basi la kwanza lianze kufanya safari zake; lakini imeshindikana kuanza kutokana na maelezo mbalimbali.
Awali Wakala huyo aliahidi kuwa basi la kwanza chini ya DART lingeanza kufanya safari zake mwaka 2009 baada ya kushindikana kuanza mwaka 2006.
Lakini ahadi hizo za nyuma zimeendelea kuugubika mradi huo na hadi mwaka huu unaenda kumalizika, haijulikani lini utaanza rasmi.
Safari hii maelezo ya DART ya kushindwa kuanza kwa mradi huo ni kesi iliyofunguliwa na wananchi wa Gerezani wanaopinga fidia ndogo waliyolipwa kupisha ujenzi wa kituo cha mabasi katika eneo la Kariakoo.
Lakini licha ya kesi hiyo, hata ujenzi wa barabara zilizoko katika awamu ya kwanza ambazo zingetumiwa na mabasi hayo kutoka Kimara hadi Kivukoni na Morocco hadi Magomeni na Fire hadi Kariakoo hazijaanza kujengwa.
Katika hatua ya awali ambayo ilikuwa ikamilike mwezi huu, ilikuwa ihusishe ujenzi wa barabara hizo zenye urefu wa kilometa zaidi ya 20. Pia kuna ujenzi wa vituo vitano vya mabasi ambavyo vingekuwa katika maeneo ya Kimara, Ubungo, Morocco, Kariakoo na Kivukoni.
DART katika mwaka wa fedha uliopita uliidhinishiwa kiasi cha Sh bilioni 1.7 ili kutekeleza mipango yake mbalimbali, ikiwemo kulipa mishahara watumishi wake.
Kwenye awamu hiyo pia kungekuwa na ujenzi wa vituo vidogo 29 na vituo vingine sita ambavyo vingetumiwa na daladala kwa ajili ya kushusha abiria ambao wanakwenda kupanda mabasi hayo yaendayo haraka.
Takule alitaja vituo vya mabasi hayo ambavyo vimekamilika kuwa ni Kivukoni, Kimara na Morocco. Lakini vituo ambavyo imeshindikana ujenzi wake kumalizika ni Gerezani ambako kesi yake iko mahakamani na haijulikani lini itamalizika.
Takule alisema wanasubiri kesi hiyo imalizike ili kituo cha Gerezani kianze kujengwa. Haijajulikana ni lini kesi hiyo itamalizika kwani ilifunguliwa tangu mwaka 2008 na hadi leo hakuna uamuzi uliotolewa na Mahakama. Lakini pia Oktoba imefika hata ujenzi wa barabara itakayotumiwa na mabasi hayo kutoka Kimara hadi Kivukoni haijaanza hali inayoonesha kuwa mradi huo kuanza kwake kwa mwaka huu ni vigumu.
Kwa mujibu wa Takule, ujenzi wa barabara peke yake utachukua miaka miwili, lakini taarifa zilizopo ni kwamba anatafutwa mkandarasi wa kufanya ujenzi huo baada ya mkandarasi wa kwanza kunyang’anywa zabuni hiyo.
Barabara ambayo inatakiwa kujengwa ni ya zege inayoelezwa na wataalamu kuwa barabara hiyo itadumu kwa miaka 25 zaidi ya barabara ya lami ambayo kudumu kwake ni kati ya miaka mitano hadi 10.
Pia Mtendaji huyo Mkuu wa DART alisema wakati awamu ya kwanza haijakamilika wataendelea na awamu ya pili na ya tatu ya ujenzi wa mradi huo.
Awamu ya pili inahusu ujenzi wa barabara na vituo katika Barabara ya Kilwa Road wakati awamu ya tatu inahusu ujenzi wa miundombinu Barabara ya Nyerere.
“Sisi tumeona tuwatafute makandarasi tuendelee na awamu nyingine wakati tunasubiri ujenzi wa barabara na vituo ambavyo vinasubiri uamuzi wa Mahakama,” alisema Takule ambaye alisisitza kuwa Wakala wake uko tayari kuanza mradi, lakini wanasubiri mamlaka zingine zinazohusika kumaliza vikwazo vilivyopo.
Mradi wa DART umepangwa kugharimu zaidi ya Dola za Marekani milioni 270 na lengo la kuanzishwa kwa mradi huo ni kuondoa tatizo la msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.
Hata hivyo, mradi huo umekuwa kitendawili na sasa inaelezwa kuwa basi la kwanza chini ya mradi huo haijulikani litaanza lini safari zake huku mradi ukionesha kuwa utakamilika mwaka 2035. Mabasi yatakayoruhusiwa chini ya mradi huo ni yale yanayoruhusu abiria kati ya 140 na 150.
Categories: