NA MUHIBU SAID
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini aliyesimamishwa kazi, David Jairo
Kazi ya kuwahoji mashahidi inayofanywa na Kamati Teule ya Bunge inayochunguza tuhuma dhidi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, ya kuingilia haki, kinga na madaraka ya Bunge na kumsafisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini aliyesimamishwa kazi, David Jairo, inatarajiwa kukamilika wiki hii, huku sehemu kubwa ya watu mashuhuri wakiwa wamekwisha kuhojiwa.
Mahojiano hayo yanayofanywa na kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake, ambaye ni Mbunge wa Tunduru Kaskazini (CCM), Ramo Makani, yalianza rasmi Septemba 5, mwaka huu.
“Tunakamilisha mahojiano wiki hii, tunaendelea vizuri,” alisema Makani alipokuwa akijibu swali la NIPASHE kuhusu hatua iliyofikia kamati yake kufikia jana.
Alisema baada ya mahojiano hayo kukamilika wiki hii, wiki ijayo wataanza kuchambua hoja na nyaraka zote zilizotolewa na mashahidi waliohojiwa na kamati.
Makani alisema watafanya uchambuzi huo kwa kulinganisha hoja na nyaraka hizo na Katiba na sheria za nchi pamoja na kanuni za Bunge.
Alisema baada ya hapo, wataanza kujibu hadidu za rejea walizopewa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, moja baada ya nyingine.
Miongoni mwa watu mashuhuri waliotarajiwa kuhojiwa na kamati hiyo ni pamoja na Luhanjo, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utou na Jairo.
Katika tuhuma hizo, Luhanjo anadaiwa kutamka mbele ya waandishi wa habari kwamba: “Alichofanya Jairo ni utaratibu wa kawaida kabisa...na kama Jairo ataweza kuwashtaki waliomdhalilisha ni yeye tu.”
Miongoni mwa kazi za kamati hiyo, ni pamoja na kuchunguza sakata lote la kumsafisha Jairo dhidi ya tuhuma za kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwashawishi wabunge kupitisha bajeti ya wizara hiyo ya mwaka wa fedha wa 2011/2012, zinazomkabili.
Mbali na Makani, wajumbe wengine wanaounda kamati hiyo, ni Gosbert Blandes (Karagwe-CCM); Mchungaji Israel Natse (Karatu-Chadema); Khalifa Suleiman Khalifa (Gando-CUF) na Martha Umbulla (Viti Maalum-CCM).
Kamati hiyo inafanya kazi kwa kuongozwa na hadidu za rejea tano; mojawapo ikiwa ni kuchunguza utaratibu uliobainika wa kukusanya fedha kwa ajili ya kukamilishwa kwa uwasilishaji wa hotuba za bajeti za wizara bungeni.
CHANZO: NIPASHE
Categories: