Mbunge azipa shule vifaa vya maabara

Imeandikwa na Khatib Suleiman, Zanzibar


MBUNGE wa jimbo la Kiembesamaki kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Waride Bakari Jabu ametoa vifaa vya maabara vya sayansi vyenye thamani ya Sh miloni mbili kwa shule mbili za jimbo hilo ili kuwawezesha wanafunzi kufaulu vizuri masomo yao.

Akikabidhi vifaa hivyo, Waride alisema kwa muda mrefu shule mbili za jimbo hilo Kiembesamaki pamoja na Chukwani zinakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa vifaa vya maabara ambavyo vimechangia kwa wanafunzi hushindwa kufaulu vizuri masomo ya sayansi.

“Mara baada ya kuchaguliwa kuwa Mbunge nilipokea maombi ya shule mbili zikiwa na mahitaji ya vifaa vya maabara...leo natekeleza ahadi hiyo kwa vitendo,” alisema Waride.

Aliwataka wanafunzi kuvitumia vizuri vifaa hivyo ambavyo vitasaidia kuweza kufaulu vizuri masomo ya sayansi ambayo yanahitaji vifaa vya maabara kwa kazi za vitendo.

Naye mwalimu wa masomo ya sayansi katika shule ya Chukwani, Awena Muumini alisema vifaa hivyo vimekuja katika wakati muafaka huku wanafunzi wakikabiliwa na mitihani ya kidato cha nne.

“Tunakushukuru mbunge kutupatia vifaa hivi vimekuja wakati muafaka ambapo wanafunzi wapo katika mitihani ya kidato cha nne ikiwemo masomo ya sayansi,” alisema.

Vifaa hivyo vina thamani ya Sh milioni 2 tayari vimeanza kutumika kwa wanafunzi wa kidato cha nne wanaofanya mitihani ya taifa mwaka huu katika masomo ya fizikia, kemia pamoja na baolojia.

Chanzo: Habari leo

Categories: