Pinda akunwa na teknolojia kilimo cha muhogo Brazil

Imeandikwa na Joseph Kulangwa, Sao Paulo


WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amekunwa na teknolojia ya kilimo cha muhogo, ambapo mashine maalumu zinatumika kupandia zao hilo tofauti na Tanzania ambako kilimo hicho bado ni cha kiwango cha chini na duni.

Waziri Mkuu alioneshwa kukunwa na teknolojia hiyo juzi alipotembelea kampuni ya kutengeneza vifaa na mashine za kilimo ya ABIMAC mjini hapa akiwa katika ziara yake ya kikazi nchini Brazil.

Hata hivyo, alisema maendeleo hayawezi kupatikana bila kufanya kazi kwa bidii, lakini pia kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Alilazimika kusema hayo alipopewa fursa ya kufanya hivyo baada ya kuangalia video ya mambo yanayofanywa na kampuni hiyo yenye matawi katika mikoa 10 nchini hapa na kampuni tanzu 4,500.

Waziri Mkuu alisema kwa Tanzania teknolojia hiyo inapaswa kutekelezwa hatua kwa hatua na si kuikimbilia.

Akizungumzia juu ya teknolojia ya kilimo cha muhogo, Pinda alisema: “Tunaweza kutumia fursa hii kuboresha kilimo cha muhogo ... tunaweza kuula, lakini ni vema sasa nasi tukaanza kuuza nje pia,” alishauri.

Kuhusu mifugo, alisema teknolojia ya kutengeneza chakula cha mifugo kutokana na majani ya kawaida, miwa na mahindi, inaweza kuwasaidia wafugaji nchini Tanzania.

“Sisi kwetu Tanzania tuna mifugo takribani milioni 21, lakini Afrika kwa jumla tuna tatizo ... hali ya hewa inapobadilika tu mifugo hukosa chakula na kufa, lakini kwa teknolojia hii tunaweza kuiokoa,” alisema.

Naye Waziri wa Ardhi na Maji Zanzibar, Ali Juma Shamuhuna ambaye anafuatana na Waziri Mkuu, alieleza kuvutiwa na teknolojia hiyo ya kilimo cha muhogo na chakula cha mifugo, akisema inaweza kuwasaidia Watanzania kama wataamua kuitumia kikamilifu.

Alisema teknolojia hiyo inaweza kusaidia wakulima na wafugaji kuinua hali yao ya kipato na hata kuondokana na umasikini lakini ikitumiwa vizuri.

Mbunge wa Rufiji, Dk. Seif Rashid alisema teknolojia hiyo inawezekana ingawa ni mpya, lakini akasema Watanzania wanaweza kufundishwa wakaielewa na kuitumia kujiendeleza.

Baadaye ujumbe wa Pinda ulitembelea kiwanda cha kutengeneza nishati ya ethanol itokanayo na miwa inayozalishwa na Kampuni ya Construtora Queiroz Calvao S/A.

Akiwa hapo hapo wilayani Piracicaba, Waziri Mkuu na ujumbe wake walitembelea kampuni nyingine ya Dedini ambayo licha ya kutengeneza mitambo ya kuzalishia ethanol inayotengeneza pia bidhaa mbalimbali za kiteknolojia pamoja na chakula na vinywaji.

Chanzo: Habari leo

Categories: , ,