Mheshimiwa diwani Edwin Haule Spika wa kata ya Ruhuhu Ludewa aliyefumwa akivunja amri ya sita na mwanafunzi
Bw. Edwin Haule Spika akiwa amepoteza uchangamfu baada ya kutolewa polisi na madiwani wenzake.
*****
DIWANI wa Kata ya Ruhuhu wilaya ya Ludewa, katika mkoa mpya wa Njombe, Edwin Haule Spika (CCM) amefikishwa mbele ya vyombo vya dola baada ya kufumaniwa na binti anayedaiwa kuwa ni mwanafunzi katika mojawapo ya shule za sekondari wilayani Ludewa.
Spika alikamatwa akiwa na mwanafunzi huyo (jina tunalihifadhi) katika nyumba ya kulala wageni ya Mbilinyi Guest House, majira ya saba usiku, mara tu baada ya diwani huyo kutua katika mji wa Ludewa akitokea katika kata yake ya Ruhuhu, Manda kwa ajili ya kuja kushiriki kikao cha Baraza la Madiwani.
“Hatua ya kukamatwa kwa mheshimiwa Spika ilitokana na mtego uliowekwa na vyombo vya ulinzi na usalama katika wilaya ya Ludewa, baada ya kupata taarifa za kuwa diwani huyo amekuwa na tabia hiyo,” walisema madiwani wenzake.
“Ni kweli kwamba diwani mwenzetu amekuwa na kawaida ya kutembea na ‘akiba’ ya mwanamke kutoka kwenye Kata yake kila anapokuja kwenye vikao, ijapokuwa hakuna ukweli wowote ambao unaonyesha kuwa mwanamke aliyekutwa naye katika nyumba ya kulala wageni iliyopo mjini Ludewa ni mwanafunzi,” walisema.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Matei Kongo, amethibitisha kukamatwa kwa diwani huyo.
“Hata hivyo kiukweli ni kwamba mwanamke aliyekutwa naye si mwanafunzi kama ambavyo ilivyokuwa ikidaiwa,” akiongeza kuwa “Mwanamke aliyefumainiwa naye mhe. Spika ni mama mtu mzima mwenye watoto wawili.” alisema Kongo.
Kongo alisema kuwa diwani wake (Spika) alikamatwa na Polisi kwa kushirikiana na maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Ludewa na kwamba baada ya kushikiliwa kituo Kikuu cha Polisi cha Wilayani hapo Ludewa na kuhojiwa kwa masaa kadhaa aliachiwa huru, ili aweze kushiriki vikao vya Baraza vilivyokuwa vinafuatia siku ya pili yake.
Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina yao baadhi ya madiwani toka Ludewa walionyesha kutofautiana kuhusiana na kitendo cha kukamatwa kwa mhe. Spika (diwani mwenzao) huku baadhi yao wakidai kuwa ni mbinu chafu za kutaka kulichafua Baraza hilo la Madiwani zinazofanywa na watu wenye uchu wa madaraka kutoka kwenye kata zao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Spika mwenyewe alithibitisha kukamatwa kwake na vyombo vya dola.
“Hizo ni mbinu chafu zinazofanywa na baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa ambao amekuwa akiwapinga mara kwa mara kutokana na matumizi yao mabaya ya fedha za wananchi,” alisema Spika.
Kwa mfano, Spika alisema, wakati wa kikao cha kumsimamsha kazi Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Juma Ally, yeye [ Spika] alikuwa mmoja kati ya madiwani waliosimama kidete kuunga mkono uamuzi wa kumsimakisha kazi afisa huyo.