Ni wanasheria Dk Tenga, Makia wa Tanesco
Na Mwandishi wetu
WAKATI Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) likibanwa kuilipa Kampuni ya Dowans Sh 111 bilioni, wanasheria walioshuhudia mkataba kati za kampuni hizo, wameibuka na kusema ni kawaida migogoro inayojitokeza kwenye makubaliano kama hayo, kusuluhishwa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Biashara (ICC).
Wanasheria hao wameeleza kuwa mikataba mingi ya kimataifa ina kipengele kilichoweka bayana kwamba migogoro inayojitokeza inasuluhishwa na ICC.
Walisisitiza kuwa kipengele kilichopo katika mkataba wa Richmond na Tanesco kinachoeleza kwamba iwapo mgogoro baina ya pande mbili utatokea lazima upelekwe ICC, ni jambo la kawaida katika mikataba ya kimataifa.
Kauli ya Dk Tenga
Wakili wa kujitegemea kutoka Kampuni ya Law Associates, Dk Ringo Tenga ambaye alitia saini mkataba huo Juni 23, 2006 kama shahidi wa Kampuni ya Richmond, aliliambia Mwananchi Jumapili katika mahojiano maalumu kuwa wawekezaji wanapenda migogoro yao kusuluhishwa na mahakama hiyo kwa sababu ina uzoefu wa masuala ya biashara za kimataifa.
"Kuhusu Tanesco kuingia mkataba na Richmond na kuwepo kipengele cha mgogoro kupelekwa ICC, mikataba mingi ya kimataifa inakuwa na kipengele hicho," alisema Dk Tenga.
Katika kesi iliyofunguliwa na Dowans mwaka 2009 kupinga kuvunjwa kwa mkataba wake iliorithi kutoka Richmond kwenye Mahakama ya kimataifa, kampuni hiyo ilishinda na Tanesco kuamriwa kulipa Sh111 bilioni.
Baada ya hapo Januari 25 mwaka huu Kampuni ya Dowans iliiomba Mahakama Kuu isaijili tuzo hiyo. Hata hivyo, Tanesco ilipinga. Mahakama Kuu ya Tanzania katika hukumu yake Septemba 28 mwaka huu, iliyosomwa na Jaji Emilian Mushi, ilikubali kuisajili tuzo ya ICC na Tanesco kutakiwa kulipa kiasi hicho cha fedha.
Jaji Mushi, alisema mahakama hiyo haina uwezo wa kuingilia maamuzi ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya kibiashara iliyotoa tuzo hiyo, Novemba 15, mwaka jana.
Kwa mujibu wa mkataba huo, waliotia saini kwa upande wa Kampuni ya Richmond ni Mkurugenzi wake, Mohammed Gire na Tanesco iliwakilishwa na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji, Johannes G. Loterring (Net Group Solution).
Dk Tenga, alisema wawekezaji wengi wanahofia kama mkataba usipokuwa na kipengele cha matatizo yao kumalizwa na ICC, wanaweza kupoteza haki yao kutokana na uhaba wa wataalamu wa sheria katika mahakama za kawaida.
Alisema ugeni katika sekta ambayo mwekezaji anawekeza pia unaweza kuwa moja ya sababu ya kuamua migogoro itakayoibuka na mtu aliyeingia naye mkataba, iende ICC.
Mtaalamu huyo wa sheria alisema kupeleka migogoro ya usuluhishi katika mahakama za kawaida mara nyingi hutumia muda mwingi na pengine kulazimika mahakama kutafuta utaalamu katika eneo hilo.
Alitoa mfano wa mgogoro wa kibiashara ambao ulitokea kati ya Kampuni ya Microsoft ya Marekani na kampuni zingine ambazo zilikuwa zikifanya biashara na kampuni hiyo kwamba kesi yake baada ya kupelekwa katika mahakama ya kawaida, iliwafanya mahakimu kuhitaji muda zaidi kujua undani wa masuala ya sekta hiyo.
Dk Tenga alisema: "Katika kesi hiyo ili mahakama kupata uwezo wa kuisikiliza ilibidi mahakimu waende kupata elimu ya mambo ya ‘software’ hali ambayo ilichelewesha zaidi kumaliza kesi hiyo tofauti na kama wangekwenda ICC."
Alisema kutokana na hali hiyo, ndiyo maana wawekezaji wa nje hupendelea wanapoingia mikataba kuwa na kipengele kinachoeleza kuwa migogoro ikitokea, lazima ipelekwe Mahakama ya Usuluhishi wa Kimataifa.
"Ninachotaka kusema ni kwamba, si jambo la ajabu mkataba wa mwekezaji kuwa na kipengele cha usuluhishi wa mgogoro kupelekwa ICC," alisema Dk Tenga ambaye pia ni Mhadhiri mstaafu wa Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Alisema kila sekta ina chombo kinachosimamia usuluhishi wake, akitoa mfano jinsi migogoro katika sekta ya habari nchini inavyopelekwa Baraza la Habari Tanzania (MCT) kusuluhishwa badala ya mahakamani.
Dk Tenga alisema hajaisoma hukumu ya Jaji Mushi kuhusu tuzo ya Dowans, lakini kama kuna kipengele ambacho Tanesco inaona kimekiukwa katika hukumu hiyo, wanaweza kukata rufaa Mahakama ya Rufani.
Alisema sheria ya usuluhishi nchini sura ya 15, inaeleza wazi kuwa unaweza kukata rufaa kupitiwa upya hukumu kama msuluhishi aliyesikiliza kesi hiyo kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi, alisikiliza upande mmoja, hakuweka kumbukumbu sawasawa maelezo ya ushahidi au msuluhishi alikuwa na mgongano wa kimaslahi katika kesi hiyo.
Dk Tenga, alisema lakini kama aliamua kesi hiyo kulingana na misingi ya kisheria, huwezi kukata rufaa ukashinda.
Alisema Tanesco lazima itafakari kwanza uamuzi wa kukata rufaa kwani sheria zote zinafahamika.Hata hivyo, Dk Tenga aliishauri Serikali kuwa wakati wa kuingia mikataba mikubwa kimataifa, lazima ifuate weledi wa watalaam.
Alisema kila sekta ina utaalamu wake hivyo, wakati inapoingia mikataba hiyo, lazima itafute wanasheria wenye ujuzi na sekta hiyo.
Mtalaam huyo wa sheria alisema kuwa, kabla ya kuingia mkataba mikubwa ni vyema kwa sasa serikali ikawatumia washauri wa kukodi kutoka Benki ya Dunia na Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola ambao wana uzoefu wa muda mrefu.
Vilevile, aliishauri serikali kurejesha utaratibu wa kupeleka wanasheria wake kusoma kwenye Chuo cha Kimataifa cha Maendeleo ya Sheria (IDLI) kilichopo Italia kama ilivyokuwa ikifanya miaka ya nyuma ili kuwaongezea uwezo kwenye mikataba ya kimataifa.
"Zamani wanasheria wengi wa mashirika ya umma walikuwa wakipelekwa IDLI Rome, Italia kusomea masuala ya mikataba," alisema na kuongeza:
"Wanasheria wanatakiwa kuwa na uelewa mpana kuhusu masuala ambayo wanaingia mikataba."
Kuhusu wanaharakati na baadhi ya wanasiasa ambao wanaoshinikiza wale walioingia mikataba hiyo kulipa fedha hizo, Dk Tenga ambaye alikuwa shahidi wa Kampuni ya Richmond wakati wakiingia mkataba huo, alisema watu hao wana haki ya kusema hayo lakini suala hilo ni la kisheria.
"Suala hili ni la kisheria sio la mtu kusema tu," alisema na kuongeza : "Kama wanaona kuna eneo ambalo bado lina udhaifu kisheria, waende mahakamani badala ya kulizungumza tu."
Dk Tenga ambaye alisema anazungumza kama mwanasheria, alionya kuwa shinikizo la kisiasa kutolipa fedha hizo bila ya kufuata sheria, linaweza kuifanya Serikali ibanwe kwa kutaifishwa mali zake.
Alisema endapo Tanesco kwa sasa itakata rufaa na kushindwa kesi hiyo halafu ikagoma kulipa, mahakama itaamuru mali zake kutaifishwa au wahusika kufungwa kwa kosa la kudharau mahakama.
Mwanasheria wa Tanesco
Kwa upande wake, Mwanasheria wa Tanesco, Godson Makia, ambaye alitia saini mkataba huo kama shahidi wa shirika hilo, aliiambia Mwananchi Jumapili kuwa wanatafakari kuona kama watakata rufaa katika siku 60 ambazo wamepewa na mahakama kisheria.
Alisema, wanapitia hukumu ya Mahakama Kuu kuona kama kuna kipengele ambacho hakikuwekwa sawa na mahakama hiyo ili wakate rufaa Mahakama ya Rufani.
Makia ambaye alikuwa shahidi na Mwanasheria wa Tanesco aliyesaini mkataba wa Richmond, alisema kwanza wataangalia hukumu kuona kama kulikuwa na makosa wakati wakusikilizwa kesi hiyo au tafsiri ya kisheria haikuzingatiwa, ndipo wakate rufaa.
Hata hivyo, alikiri kuhusu kipengele katika mkataba huo kinachotaka usuluhishi wa mgogoro wowote kati ya pande hizo mbili lazima upelekwe kusikilizwa ya ICC kwa maelezo kuwa kinawafunga.
Makia alisema mara nyingi kwenye mikataba ya wawekezaji wa nje kuwepo kipengele kinachobainisha kuwa migogoro itakayoibuka ipelekwe mahakama ya ICC, kwani huichukulia mahakama hiyo kama kinga yake.
Kuhusu wanaharakati na wanasiasa ambao wanaoshinikiza waliosaini mkataba huo kulipa tuzo hiyo ya sh bilioni 111, Makia alisema hawaelewi masuala ya sheria ndiyo maana wanasema hivyo.
Aliongeza: "Wanaharakati wanaweza kusema chochote, lakini sheria ndio tunayotakiwa kuifuata."
Wanaharakati mahakamani
Septemba 6, mwaka huu, wamiliki wa Kampuni ya Dowans walishinda kesi iliyofunguliwa Mahakama Kuu ya Tanzania na wanaharakati nchini, kupinga kulipwa tuzo yake ya Sh94 bilioni.
Wanaharakati hao ambao walidai kuwa wameamua kupinga usajili wa tuzo hiyo kwa maslahi ya umma ni pamoja na Kituo cha Msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Wengine ni Chama cha Wanasheria wa Mazingira (LEAT) na Kampuni ya Sikika (Sikika Company Limited- CL). Taasisi hizo ziliwakilishwa na wakili, Dk Sengondo Mvungi pamoja na mwanahabari Timothy Kahoho.
CHANZO: MWANANCHI
Categories:
Dr Ringo Tenga,
richmond,
Tanesco,
umeme