Nahodha: Biashara zinaweza kufanyika Dar usiku ikiwa..

Hadija Jumanne

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha, amesema biashara katika Jiji la Dar es Salaam, zinaweza kufanyika hadi usiku wa manane iwapo ulinzi shirikishi utaimarishwa.

Nahodha aliyasema hayo juzi katika hafla ya kuchangia kazi za ulinzi na usalama shirikishi, ambapo alisema kama nchi ikidhamiria kufanya biashara usiku, itaweza na shughuli za maendeleo zinataongezeka. Bila kufafanua zaidi, Nahodha alisema kuwa, kuna uhusiano mkubwa kati ya maendeleo ya uchumi na usalama wa raia na mali zao, hivyo jamii kwa ujumla ina kazi ya kuhakikisha ulinzi shirikishi unakuwepo katika sehemu yoyote.

Alibainisha kuwa hadi sasa jeshi hilo lina askari polisi 40,000, idadi aliyosema ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya Watanzania wanaokadiriwa kuwa 40 milioni.

“Kwa viwango vya kimataifa askari mmoja anatakiwa kulinda watu 450 lakini hapa kwetu askari mmoja analinda watu 1000 na mahitaji ya ulinzi na usalama wa raia na mali zao ni makubwa ikilinganishwa na idadi ya watu,”alisema Nahodha na kuongeza: “Watanzania ni wepesi kulaumu na kulalamika, lakini ni wagumu kutoa mawazo na fikra”.

Katika hafla hiyo iliyofanyika Bwalo la jeshi Osterbay jijini humo, jumla ya Sh106.8 milioni taslimu zilichangwa na wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara wakubwa na wadogo. Michango mingine ilikuwa ni kompyuta saba, pikipiki 47, mashine za kudurufu tatu, Radio za mawasiliano 15, ving’ora sita ambavyo vitatumika katika kupunguza ajali za barabarani.

Categories: