NHC yatimua wizara kwa kulimbikiza deni

NA RICHARD MAKORE


Idara ya Mkulima wa Kisasa iliyopo chini Wizara ya ya Kilimo, Chakula na Ushirika imetimuliwa na vifaa vyake kutolewa nje ya ofisi zake baada ya kushindwa kulipa kodi ya pango kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Sh. milioni 30.
Zoezi hilo ni mwendelezo wa kuzitimua taasisi za serikali zilizopanga katika nyumba za NHC na kulimbikiza madeni ya pango na kudaiwa Sh. bilioni 2 yakiwa ni malimbikizo ya miezi 15.
Kabla ya mwishoni mwa mwaka jana NHC ilikuwa inawadai wateja wake nchi nzima Sh. bilioni 5.5.
Shirika hilo liliitimua wizara hiyo jana mchana na baada ya kutoa vifaa vya ofisi, milango yote ya ofisi hizo ilifungwa.
Ofisi hizo zipo makutano ya barabara ya Mkwepu na Garden Avenue karibu na Posta Mpya jijini Dar es Salaam.
Meneja wa Kitengo cha Kukusanya Madeni wa NHC, Japhet Mwanasenga, alisema wapangaji hao wametimuliwa baada ya kushindwa kulipa kodi na kuwa walipewa notisi ya mwezi mmoja na kutakiwa kulipa, lakini hawakuchukua hatua zozote ikiwemo kuonyesha nia ya kutaka kulipunguza.
Aidha, alisema dalali wa NHC naye alitoa notisi ya siku 14, lakini kipindi chote hicho mpangaji wao hakujibu.
Alifafanua kuwa NHC imelenga kukusanya madeni yote kutoka kwa wapangaji wake na kwamba haiogopi kuzidai taasisi za serikali ambazo zimekuwa sugu kwa kushindwa kulipa.
Mwanasenga alisema kila bajeti ya serikali inayopitishwa kila mwaka fedha kwa ajili ya kulipia pango zinatengwa, lakini hazilipwi.
Kwa upande wake, uongozi wa wizara hiyo ulikiri kuwa unadaiwa na kwamba hawana cha kusema zaidi.
“Ni kweli tunadaiwa fedha hizo na NHC, wapo sahihi ila hatuna cha kuzungumza zaidi hapa ni kama unavyoona vyombo vyetu vimetolewa nje, alisema mmoja wa wafanyakazi wa kitengo hicho.
NHC ilichukua vifaa hivyo na kuvipelekwa katika ofisi zake zilizopo Upanga na kutoa alitoa siku saba kulipa deni hilo vinginevyo vitauzwa kwa mnada.

CHANZO: NIPASHE

Categories: