Kesi ya akina Mramba yapigwa kalenda

NA HELLEN MWANGO


Mawaziri wa zamani, Basil Mramba na Daniel Yona na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Hazina, Gray Mgonja

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imepiga kalenda kesi ya matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 11.7, inayowakabili mawaziri wa zamani, Basil Mramba na Daniel Yona na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Hazina, Gray Mgonja hadi Oktoba 19, mwaka huu.
Kesi hiyo iliahirishwa jana na Hakimu Mkazi, Mfawidhi Illivin Mgeta, baada ya jopo linalosikiliza kesi hiyo kuwa na udhuru wa kikazi.
Kesi hiyo inasikilizwa na mahakimu watatu, John Utamwa, Saul Kinemela na Sam Rumanyika, linapitia mwenendo wa kesi hiyo na kisha kugawa nakala kwa mawakili wa pande zote mbili ili waweze kutoa hoja mahakamani kama washtakiwa wana kesi ya kujibu au la.
Akiahirisha kesi hiyo, Hakimu Mgeta, alisema itatajwa Oktoba 19, mwaka huu ambapo mahakama itaangalia kama jopo hilo litakuwa limemaliza kupitia mwenendo huo.
Upande wa mashtaka umeshafunga ushahidi wake baada ya kuita mashahidi 13 na kuwasilisha vielelezo 26 mahakamani.
Katika kesi hiyo, washitakiwa wanadaiwa kuwa, kati ya Agosti mwaka 2002 na Juni 14 mwaka 2004, jijini Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma, walitumia vibaya madaraka yao.

CHANZO: NIPASHE

Categories: