TAARIFA KUTOKA SHIRIKISHO LA SOKA NCHINI (TFF) LEO

MTANZANIA AOMBEWA ITC UJERUMANI
MCHEZAJI Costancia Maringa wa Tanzania ameombewa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ili aweze kucheza mpira wa miguu wa wanawake nchini Ujerumani.

Chama cha Mpira wa Miguu cha Ujerumani (DFB) kimetuma maombi hayo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ili kumwezesha mchezaji huyo kuichezea timu ya FC 1919 Marnheim ya nchini humo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa DFB, Helmut Sandrock, Maringa mwenye umri wa miaka 12 ameombewa ITC na chama hicho kama mchezaji wa ridhaa. TFF inafanyia kazi maombi hayo na hati hiyo itatolewa mara baada ya taratibu husika kukamilika.


LIGI DARAJA LA KWANZA
Michuano ya Ligi Daraja la Kwanza hatua ya makundi msimu huu inayochezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini inaanza Oktoba 15 mwaka huu. Jumla ya timu 18 zinashiriki katika ligi hiyo.

Kundi A kesho itakuwa Temeke United vs Polisi Dar es Salaam (Uwanja wa Mlandizi, Pwani) na Mgambo Shooting vs Transit Camp (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga). Mechi nyingine ya kundi hilo kati ya Burkina na Morani itachezwa Oktoba 16 mwaka huu Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Mechi za kundi B kesho ni Polisi Iringa vs Small Kids (Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora, Iringa), Tanzania Prisons vs Mbeya City (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Mbeya) na Mlale JKT vs Majimaji (Uwanja wa Majimaji, Songea).

Kundi C kesho ni AFC vs Manyoni (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha), Polisi Morogoro vs 94 KJ (Uwanja wa Jamhuri, Morogoro), Polisi Tabora vs Rhino (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora).

Categories: