Na Boniface Meena
WANANCHI sasa wataweza kusafiri kwa haraka zaidi kutoka mkoa mmoja hadi mwingine, ifikapo mwaka 2013 kwa kutumia ndege za shirika la Precision.
“Sasa hivi tuna ndege 11 na tunaendelea kujitanua ifikapo mwaka 2013 tutatakuwa na ndege zinazoweza kufanya safari katika mikoa yote nchini,”alisema Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Alifonse Kioko.
Pia sasa wananchi mbalimbali na mashirika wameshauriwa kununua hisa za shirika hilo ili wawe sehemu ya wamiliki . Shirika hilo limepewa vibali vya kuuza hisa katika Soko la Awali (IPO) na kuorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Shirika hilo litatoa zaidi ya hisa 58 milioni na kwamba kila hisa itauzwa Sh475. "Mtu ataruhusiwa kununua hisa 200,"alisema Kioko.Shirika hilo linatarajia kupata Sh28 bilioni kutokana na mauzo ya hisa hizo. Mauzo hayo yataliwezesha shirika hilo kununua ndege yoyote wanayoihitaji.
Pia wana mpango wa kuongeza ndege tatu aina ya Boing 737-300, tano aina ya ATR 72-500, mbili aina ya ATR-42-500 na ndege nne aina ya ATR-42-600.
“Jumla tutakuwa na ndege 14 mpya ambazo zitatusaidia kuongeza safari zetu katika mikoa mbali mbali nchini kwa miaka miwili ijayo, hivyo shirika linakuwa,”alisema Kioko.Kioko alisema safari ya nje ya nchi nazo zitaongezeka na kwamba watakuwa wanakwenda Bujumbura, Juba, Kigali, Harare, Nampula na Lubumbashi.
Mwaka 2004, shirika hilo lilikuwa na mali yenye thamani Sh21 bilioni, lakini hadi sasa imefikia Sh 240 bilioni. Kutokana na ukuaji huo shirika hilo limekuwa kwa asilimia 20.
Katika hatua nyingine, mapato yamekuwa kutoka Sh20 bilioni mwaka 2004 mpaka kufikia Sh113 bilioni mwaka huu.
Categories: