NA MUHIBU SAID
*Asema upinzani unakua kwa asilimia 40
*Aeleza ununuaji shahada ni ujambazi wa kisiasa
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, amesema matokeo ya uchaguzi mdogo wa Igunga ambao mgombea wa CCM alishinda kwa mara nyingine yametoa picha kuwa upinzani unazidi kukua na CCM inashuka.
Akitoa tathimini ya uchaguzi huo, ambao ushindani mkubwa ulishuhudiwa miongoni mwa vyama vitatu wakati wa kampeni, CCM, Chadema na CUF, Tendwa, alisema alikwisha kusema tangu baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana kuwa upinzani umekua kwa asilimia 40 ikilinganisha na ushindi wa kishindo wa CCM wa mwaka 2005.
“Matokeo ya uchaguzi wa Igunga yanaonyesha kuwa upinzani unazidi kukua na CCM inashuka,” alisema Tendwa alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari.
Alisema hali hiyo inatokana na ushindani mkubwa wa kisiasa uliopo hivi sasa nchini kati ya vyama vya upinzani na CCM.
Kadhalika alitaja sababu za watu wachache kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga, mkoani Tabora, ikilinganishwa na idadi ya walioandikishwa, kuwa ni pamoja na ujambazi wa kisiasa uliofanywa na baadhi ya wanasiasa kununua shahada za wapigakura.
Wakati Tendwa akitaja sababu hizo, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo hilo, Protace Magayene, ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kubuni mbinu mbadala ya kuhakikisha wananchi wanajitokeza kupiga kura.
Wapigakura walioandikishwa katika Jimbo la Igunga ni 171,019 na waliojitokeza kupiga kura mwaka huu ni 53,672 sawa na asilimia 31.3, kukiwapo ongezeko la asilimia 2.7 ikilinganishwa na idadi ya waliopiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, ambao walikuwa 49,013 sawa na asilimia 28.6 ya 171,077 waliokuwa wamejiandikisha.
Hata hivyo, Tendwa, alisema:“Uchaguzi ulikuwa wa amani na utulivu. Kura zilipigwa kwa amani, hakukuwa na msukosuko, ingawa kulikuwa na kasoro za kiutendaji. Kasoro hizo zimewaathiri watu wa Igunga kutokupiga kura.
Aliongeza: “Athari hizo si kubwa, lakini athari ni athari. Idadi ya waliojitokeza kupiga kura Igunga inasikitisha … Nasubiri ripoti, lakini nimeambiwa kulikuwa na kununua kwa kadi za kupiga kura na baadhi ya wanasiasa. Huu ni ujambazi wa kisiasa.”
Alisema sababu nyingine iliyochangia watu wachache kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi huo, ni kauli na vitendo vya vitisho vilivyotolewa na baadhi ya wanasiasa wakati wa kampeni.
Tendwa alisema vitisho hivyo viliwafanya wananchi wa Igunga, ambao wengi wao wanaishi vijijini kuogopa kwenda kupiga kura, badala yake kuamua kwenda kutafuta mahitaji yao muhimu, kama vile maji.
Alisema sababu nyingine iliyowafanya watu wachache kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi huo, ni kutokutolewa kwa elimu ya upigaji kura, hivyo kuwafanya wananchi wengi kutokuelewa umuhimu wa kupiga kura.
“Matokeo yake vijana hawakujitokeza kupiga kura, kwa sababu elimu hawakupata, hivyo, kadi za kupiga kura wamebaki wakizitumia kama vitambulisho na baya zaidi walitishwa. Ripoti inakuja, tutafanya tathmini ya kueleweka,” alisema Tendwa.
Alisema kipindi cha kabla ya uchaguzi huo, hakikuwa kizuri na kwamba, matukio yaliyojiri kabla na baada ya uchaguzi, hayakuwa ya kidemokrasia.
Zaidi ya hivyo, alisema hakukuwa na uvumilivu wa kisiasa miongoni mwa vyama vya siasa na kwamba, maadili na kanuni za uchaguzi havikufuatwa.
Alisema akiwa mlezi wa vyama vya siasa, amekuwa akivishauri vyama kuzingatia utawala bora, uongozi mzuri na uvumilivu wa kisiasa, lakini ushauri wake huo umekuwa ukipuuzwa kwa sababu tu ya kutaka kura na kula.
“Kwanini polisi waanze kupiga mabomu? Kwa sababu hakukuwa na nidhamu ya wanasiasa. Matukio hayakuwa mazuri kabla na baada ya uchaguzi,” alisema Tendwa.
Kutokana na hilo, alisema mwezi ujao Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania, litakutana katika mkutano utakaotoa fursa kwa vyama vyote vya siasa kutoa tathmini yao kuhusu uchaguzi mdogo wa Igunga na kutoa ushauri.
Hata hivyo, alisema kila chama cha siasa, kikiwamo chama tawala (CCM), kinawajibika kubadilika na kuzingatia utawala bora, uongozi mzuri na uvumilivu wa kisiasa kwa vile hakiko peke yake katika medani za siasa.
Alisema kuanzishwa kwa Baraza la Vyama vya Siasa kulizingatia mambo hayo na kutoa fursa kwa vyama vya siasa kukaa pamoja kuwekana sawa.
Hata hivyo, alisema kulingana na mfumo wa uchaguzi wa Tanzania, alama ndogo tu inatosha kukipatia chama cha siasa ushindi katika uchaguzi.
“Mfumo wetu wa uchaguzi, ukimpita mwenzio kwa bega, kwa kidole au kwa pua tu basi umeshinda. Mtu hushinda kwa alama tu,” alisema Tendwa.
Katika uchaguzi huo, aliyekuwa mgombea kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Dallaly Kafumu, aliibuka mshindi kwa kura 26,484 sawa na asilimia 50.56.
Aliyekuwa mgombea kupitia Chadema, Joseph Kashindye, alipata kura 23,260 sawa na asilimia 44.32, huku aliyekuwa mgombea wa CUF, Leopard Mahona, akiambulia kura 2,104 sawa na asilimia 4.01.
Hata hivyo, Kashindye, alikataa kusaini fomu ya matokeo hayo baada ya kuona idadi ya kura alizopata na tayari imekwisha kutangaza azma yake ya kwenda mahakamani kupinga matokeo hayo.
Wagombea wengine walikuwa ni Stephen Mahui wa Chama cha AFP (kura 235), Hassan Lutegeza wa Chausta (183), Said Cheni wa DP (kura 76), John Maguma wa Sau (kura 83) na Hemed Dedu wa UPDP (kura 63).
MSIMAMIZI IGUNGA ATOA USHAURI KWA NEC
Kutoka Igunga, Msimamizi wa Uchaguzi jimboni humo, Magayene ameitaka Nec kubuni mbinu mbadala ya kuhakikisha wananchi wanajitokeza kwa wingi kupiga kura.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo, Magayane, alisema mwamko wa wananchi kujitokeza kupiga kura ni mdogo na kutolea mfano katika uchaguzi wa Igunga.
Alisema jitihada za kutosha zinahitajika kuhakikisha wananchi wanapiga kura kwa wingi tofauti na hali ilivyo kwa sasa, kwani idadi ya wapiga kura inazidi kupungua.
Aliishauri Nec kurekebisha baadhi ya adhabu katika sheria ya maadili kwa kuwa ni ndogo ikilinganishwa na makosa.
Vile vile, alishauri adhabu ya kosa la kupanda jukwaani na silaha iwe faini isiyopungua Sh. 500,000 na kifungo kisichopungua miaka mitatu jela vinginevyo vitendo hivyo vitakithiri katika chaguzi.
Katika uchaguzi wa Igunga, Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Ismail Aden Rage, alitozwa faini ya Sh. 100,000 na Kamati ya Maadili ya Wilaya ya Igunga baada ya kupanda jukwaani katika mkutano wa kampeni akiwa na bastola kiunoni.
Pia aliishauri ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kurekebisha baadhi ya sheria na kamati mbalimbali za uchaguzi ili kwenda na wakati kuhakikisha sheria zinakuwa na uzito kwa mtu atakayebainika kuvunja.
Miongoni mwa changamoto za uchaguzi huo, alisema ni vyama vya siasa kuweka mawakala bila kuwafundisha sheria za uwakilishi katika kuhakikisha zoezi la kupiga kura linakamilika, hali ambayo alisema imechangia kupoteza muda wa kupiga kura kwa suala ambalo lingeweza kutatuliwa mapema.
CHANZO: NIPASHE
Categories: