BILIONI 8.6/- KUNUNUA ENEO LA KUJENGA SAFARI TOWN

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Arusha limeidhinisha zaidi ya Sh bilioni 8.6 za malipo ya ununuzi ekari 432 katika eneo la Lakilaki litakalojengwa mji mpya utakaojulikana kama Safari Town. Malipo hayo yatafanyika baada ya kupatiwa mkopo kutoka Benki ya Biashara ya Afrika (CBA) baada ya halmashauri hiyo kukubali kufungua akaunti kwa ajili ya fedha hizo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Halifa Hida alisema kabla ya kufanyika kwa mauziano na halmashauri hiyo, shamba hilo lilifanyiwa tathimini na kubainika kuwa thamani yake ni Sh bilioni 29. Tathmini ilifanywa na Kampuni ya M $ R Agency ya Dar es Salaam.  “Baraza la Madiwani waliidhinisha fedha hizi tangu Agosti 15, mwaka huu kwa ajili ya malipo ya ardhi hii, lakini hapa tunalipa kwa kila ekari moja shilingi milioni 20 na milioni 40 tutalipa katika vyanzo vya mapato,” alisema Hida.

Alisema lengo kubwa la ununuzi wa ardhi hiyo ni kujenga mji mpya. Wataalamu kutoka Uturuki ndiyo watakaojenga nyumba katika mji huo ambazo baadhi yake, zitauzwa kwa bei nafuu kwa wananchi na nyingine zitapangishwa ili kuiingizia mapato halmashauri.

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mercy Silla, aliipongeza halmashauri hiyo kwa kubuni mradi huo mkubwa endelevu wa kuingizia fedha nyingi halmashauri. Alisema ni vema Halmashauri nyingine ziige mfano wao.
Chanzo; Habari leo

Categories: