JK,CHADEMA WAKUBALIANA KUBORESHA MUSWADA


Rais Jakaya Kikwete akimuaga Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe baada ya kumalizika kwa mazungungumzo na viongozi wa chama hiyo juu ya muswada wa marekebisho ya Katiba Mpya, Ikulu, jijini Dar es Salaam, jana. Picha na Edwin Mjwahuzi



WASEMA IPO HAJA ILI UKIDHI MAHITAJI,MWAFAKA WA KITAIFA

Na Boniface Meena
RAIS Jakaya Kikwete na viongozi wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wao, Freeman Mbowe wamekubaliana kwamba ipo haja ya kuendelea kuuboresha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 ili ukidhi mahitaji ya kuaminiana na mwafaka wa kitaifa.Pia, wamekubaliana yawepo mawasiliano na mashauriano ya mara kwa mara kati ya Serikali na wadau mbalimbali juu ya kuboresha sheria hiyo kwa lengo la kudumisha mwafaka wa kitaifa kwenye mchakato wa Katiba Mpya.

Makubaliano hayo yamefikiwa jana na kusainiwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Emmanuel Nchimbi baada ya kumalizika kwa mkutano wa siku mbili baina ya pande hizo mbili kuhusu muswada huo.

Katika kikao cha jana Mbowe aliongozana na wajumbe wa kamati hiyo Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara) Said Arfi na Makamu Mwenyekiti (Zanzibar) Said Issa Mohamed, Mshauri wa Masuala ya Siasa wa chama hicho, Profesa Mwesiga Baregu, Profesa Abdallah Safari na Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Tundu Lissu na John Mrema.

Katibu Mkuu Dk Willibrod Slaa ambaye ni mjumbe hakuwapo katika kikao cha juzi na cha jana na taarifa zilizopatikana baadaye na kuthibitishwa na yeye mwenyewe ni kwamba alikuwa safarini kwenda kuhudhuria kesi yake mahakamani Arusha jana.

Kabrasha lililokabidhiwa na ujumbe wa Chadema kwa Rais Kikwete lilikuwa lina waraka uliotoa mapendekezo mbalimbali ya kurekebisha muswada huo huku wakitaka sheria iweke wazi kwamba Rais hana mamlaka yoyote juu ya Bunge Maalum la Katiba zaidi ya mamlaka ya kuliitisha kwa mara ya kwanza na kwamba mamlaka ya Bunge hilo yataisha mara baada ya kupitishwa kwa Katiba Mpya katika Bunge Maalum la Katiba.

Wametaka ifanyike hivyo kwa kuwa sheria hiyo inampa Rais mamlaka juu ya Bunge Maalum la Katiba wakati Bunge hilo linatakiwa kuwa chombo huru na chenye mamlaka ya juu kuliko mamlaka nyingine zozote katika nchi.

Katika waraka wao, Chadema wameeleza kutaka vifungu vyote vinavyokiuka haki za kimsingi za kikatiba vifutwe na kuwapo na uhuru kamili wa kujadili, kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi juu ya utungaji wa Katiba Mpya hata kama itakuwa kinyume na matakwa ya Tume ya Katiba na masharti ya Sheria hiyo.

Katika ukusanyaji na uratibu wa maoni ya wananchi juu ya Katiba Mpya na masuala ya muungano wametaka ziundwe tume mbili za katiba, moja itakayokusanya na kuratibu maoni ya wananchi kuhusu katiba mpya kwa ajili ya masuala yasiyokuwa ya Muungano ya Tanganyika na ya pili itakayokusanya na kuratibu maoni ya wananchi juu ya masuala ya Muungano.

Wameeleza tume ya katiba itakayohusu masuala yasiyokuwa ya Muungano ya Tanganyika iwe na wajumbe na sekretarieti watakaotoka Tanganyika wakati tume ya katiba itakayohusu masuala ya Muungano iwe na wajumbe na sekretarieti watakaotoka katika pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano kwa msingi wa usawa wa uwakilishi.

Waraka huo umependekeza sheria ibadilishwe ili kuweka utaratibu wa kuanzishwa tena kwa Serikali ya Tanganyika itakayoweza kujadiliana mustakabali wa Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa usawa.

"Pendekezo hili linaenda sambamba na mapendekezo ya Tume ya Rais ya Mfumo wa Chama Kimoja au Vyama Vingi vya Siasa (Tume ya Nyalali) na Tume ya Kukusanya Maoni Juu ya Katiba, White Paper namba 1 ya 1998 (Tume ya Kisanga),"umeeleza waraka huo.

Walitaka serikali mpya ya Tanganyika itakayoundwa ijadiliane upya na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu ya mambo ya Muungano na muundo wa Muungano wenyewe.

"Sheria ibadilishwe ili kuweka utaratibu wa kuitishwa kwa kura ya maoni juu ya Muungano na muundo wake."

Walieleza masharti ya katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano na Sheria za Uchaguzi yanahitaji kufanyiwa marekebisho ili kuiunda upya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa lengo la kuipa uhuru mkubwa zaidi na kwa lengo la kuweka utaratibu wa namna ya kuendesha kura ya maoni.

Pia, sheria iweke wazi kwamba endapo katiba mpya itakataliwa na wananchi walio wengi kwenye kura ya maoni, basi mchakato wa utungaji wa katiba mpya utaanza tena kwa kuzingatia matakwa na makubaliano ya wadau mbalimbali.

Katika mapendekezo yao mwisho wamemtaka Rais atumie mamlaka yake ya kikatiba kutoukubali muswada wa sheria hiyo ili kuwapa Watanzania fursa ya kutengeneza mchakato wa katiba mpya utakaowawezesha wote bila kujali itikadi zao za vyama vya siasa, kutunga katiba yao wenyewe.

Rais Kikwete alianza kukutana na viongozi hao juzi ambapo alikabidhiwa kabrasha la mapendekezo yao na kujadili mchakato wa utungwaji wa katiba mpya.

Alikutana na viongozi hao majira ya saa tisa na nusu alasiri mpaka saa 12 jioni na kukabidhiwa kabrasha la maoni ya viongozi hao kabla ya viongozi hao walioongozwa na Mbowe, kupiga picha za pamoja na Rais wakiwa ndani na baadaye nje ya jengo la Ikulu na hatimaye kuendelea na majadiliano.

Jana viongozi wa Chadema waliwasili viwanja vya Ikulu saa 4:00 na kupokewa na Rais Kikwete na kufanya mazungumzo kwa muda wa saa tano kisha kutoka na kuagana.

Ujumbe ulioambatana na Rais Kikwete jana ulikuwa ni pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, Mathias Chikawe, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera , Uratibu na Bunge), William Lukuvi na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Emmanuel Nchimbi.

Categories: