MAFISADI CCM WAKALIA KUTI KAVU

*Mkakati wa kuwamaliza kidiplomasia yatajwa
*JK alikwepa mtafaruku,kupisha upepo mbaya

Na Mwandishi Wetu

SIKU tatu baada ya kumalizika kwa vikao vya juu vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini Dodoma wiki iliyopita, upepo mbaya umeanza
kuwaelekea watuhumiwa wa ufisadia ndani ya chama hicho wanaotakiwa kujivua magamba kwa kutafakari wenyewe tuhuma zao kabla ya kuondolewa kwa nguvu.

Hali hiyo inatokana na siri nzito kutoka ndani ya vikao hivyo kueleza kuwa mbinu iliyotumiwa na Mwenyekiti wa chama hicho Rais Jakaya Kikwete, kurudisha suala hilo kuamuliwa na Kamati ya Maadili kisha kuwasilisha maamuzi yake kwa Kamati Kuu unalenga kuwamaliza kabisa watuhumiwa hao.

Imeelezwa kuwa syahili hiyo mpya iliyotumika mjini Dodoma haikulenga kufuta mchakato wa kuwaondoa watuhumiwa haoa kama ilivyodaiwa bali ulilenga kuepusha malumbano ndani ya kikao baada ya kubainika kundi hilo kuandaa watu wao kuwatetea kwanguvu kubwa na kuwa tayari hata kuchafua hali ya hewa.

Taarifa zilizoifikia Majira juzi na jana, vinaeleza kuwa baada ya kundi hilo kudaiwa kuwa na wafuasi wengi ndani ya Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), washauri wa masuala ya kisiasa ndani ya CCM walitaka Kamati ya Maadili imalize suala hilo kukwepa mjadala mzito kutokana na wahusika kuwa na kundi kubwa la kuwatetea.

"Kilichotakiwa watu waelewe tangu mwanzo ni kwamba CCM kama chama ni wajanja kuliko kundi la mafisadi, wale jamaa walijiandaa na wana wafuasi na kundi kubwa ndani ya NEC, kuwamaliza mle ni tatizo kubwa.

"Njia pekee wa kuwamaliza ni kuwaachia Kamati ya Maadili ambako mle kuna wajumbe wachache na wenye msimamo thabiti na wanaoijua vizuri chama, kama mnafikiri kujivua gamba imefikia mwisho subirini mtaona matokeo, Kamati inakwenda kumaliza kila kitu,"kilisema chanzo chetu.

Taarifa hizo zilieleza kuwa Rais Kikwete baada ya kuona hali halisi na kupewa taarifa za siri za jinsi kundi hilo ilivyojipanga kupambana kufa na kupona alishauriwa na wakongwe mbalimbali wa kisiasa kumaliza suala hilo kwa njia ya diplomasia na kwamba hakuna atayelaumiwa.

"Kamati ya Maadili ikishamaliza itawasilisha maamuzi yake ambayo kwa lugha ya diplomasia ya chama huitwa mapendekezo, Kamati Kuu itabariki maamuzi hayo na hapo ndio mwisho wa hatua hiyo watafuata wengine," kilisema chanzo chetu ndani ya CCM.

Majira ilipomtafuta Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Bw. Nape Nnauye, kuthubitisha taarifa hizo alisema yupo kwenye kikao na kuahidi kutoa ufafanuzi baada ya kumaliza. Hata hivyo hadi tunakwenda mtamboni kiongozi huyo hakuweza kuzungumzia suala hilo kwa maeleoz kuwa bado anaendelea na kikao.

Wajumbe wa Kamati ya Maadili ya CCM ni Mwenyekiti wa Taif Rais Jakaya Kikwete, Makamu Bara Bw. Pius Msekwa, Amani Karume, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balosi Seif Iddi, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Katibu Mkuu Wilson Mukama, Naibu Katibu Mkuu Bara Bw. John Chiligati, Vuai Ali Vuai.


Kwa mujibu wa taratibu za CCM Kamati ya Maadili inaweza kuchukua hatua moja kwa moja au kutoa mapendekezo kwa Kamati Kuu (CC) ambayo pia wajumbe wake karibu wote wanaingia pia kuyabariki.

Katika kikao cha NEC cha wiki iliyopita Waziri Mkuu aliyejizulu Bw. Edward Lowassa, alilalamika kuchafuliwa huku Waziri Mkuu Mstaafu Bw. Frederick Sumate, alitaka majibu ya sababu zinazofanya wanaochafua Bw. Lowassa kutochukuliwa hatua kama hana kosa.

Suala la kujivua gamba ndani ya CCM imeleta mwamko mpya wa kimtazama ndani ya CCM huku kundi moja linalojipambanua kuwa na msimamo wa kimaadili ikielezwa kuusimami na upande wa pili ukieleza kuwa ni mchakato unaokivuruga chama hicho kwa madai kuwa hakuna ushaidi wa magamba yanayotakiwa kuvuliwa.

Categories: