JUKWAA LA KATIBA LAPANGA MAANDAMANO NCHI NZIMA

Habari Na Geofrey Nyangóro,


MUUNGANO wa Asasi za kiraia zaidi ya 180 zinazounda Jukwaa la Katiba nchini umepanga kufanya maandamano nchi nzima, lengo likiwa kushinikiza Rais Jakaya Kikwete kutosaini Muswada wa mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2011.

Muswada huo uliopitishwa na Bunge wiki iliyopita ulikuwa ukipingwa na Jukwaa hilo, Chama cha Demokrais na Maendeleo Chadema, Chama cha NCCR-Mageuzi na makundi mbalimbali ya wanataalamu.

Akisoma tamko la muungano wa asasi hizo kwa wanahabari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba alimtaka Rais kutosaini muswada huo akida mchakato wake umewanyima wananchi wengi fursa ya kuchangia maoni yao.

“Tunatoa wito kwa watanzania kujitokeza kwa wingi katika maandamano ya amani yatakayofanyika Jumamosi wiki hii yenye lengo la kumtaka Rais asitie saini muswada huo kuwa sheria, kwa kuwa wananchi wengi watakuwa wamekosa fursa ya kushiriki katika mchakato huo kuanzia hatua ya msingi,” alisema Kibamba.

Kibamba alifafanua kuwa muswada huo haukupaswa kusomwa kwa mara ya pili bungeni huku akiainisha kuwa sababu kuu ni kwa kuwa umeandikwa kwa lugha ya Kiswahili kwa mara ya kwanza.

Alisema kutokana na lugha hiyo kueleweka vema hapa nchini, ushiriki wa wananchi vijijini na mijini ungetoa fursa kwao kushiriki vema kutengeneza msingi imara wa kuandika katiba mpya. “Jukwaa la Katiba nchini tutaendelea kusema ukweli kwamba muswada wa mabadiliko ya sheria ya katiba haukupaswa kufikishwa bungeni kabla ya kufikishwa kwa wananchi vijijini na mijini Tanzania bara na visiwani,” alisema Kibamba.

Alisema muswada huo wa Kiswahili ambao ulikuwa hitaji kwa watanzania ulitarajia kutoa fursa kwa wabunge kupata maoni kutoka kwa wapiga kura wao ambayo yangewezesha kuwafanya wachangie vema mjadala huo.

Alisema maandamano hayo ambayo yanaratibiwa na asasi zaidi ya 180 zinazounda Jukwaa hilo kote nchini yatafanyika Jumamosi wiki hii na kwa Dar es Salaam yamepangwa kuanzania Viwanja vya Mnazi Mmoja hadi Viwanja vya Jangwani.

“Taratibu zote za kisheria kuhusu maandamano hayo zimeanza kutekelezwa na tayari tumeshamuandikia barua Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Said Mwema, tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi kuheshimu sheria zilizopo kwa kuacha watu wafanya maandamano ambayo ni haki yao kikatiba,” alisema Kibamba.

Alisema Katiba ya sasa Ibara ya 12 hadi 20 inatoa haki hizo
Faida za wananchi kushiriki hatua za awali

Alisema zipo faidi nyingi kwa wananchi kushiriki mchakato huo kuanzia hatua za awali ikiwamo ya kuimiliki na kujenga muafaka wa kitaifa.Alisema huo ndio msingi wa wananchi kuikubali,kuiheshimu na kuithamini katiba wanayoiandika kwakuwa itakuwa imetokana na ridhaa yao inayoeleza jinsi wanavyotaka kuendesha nchi yao.

Alisema faida nyingine ni wananchi kuamua jinsi ya kuwapata wajumbe wa tume ya kukusanya maoni, wajumbe wa Bunge la Katiba na kubaini ni chombo gani kisimamie wananchi waweze kupiga kura ya maoni.
Bunge lilivyojadili Jukwaa la Katiba liliwatuhumu wabunge kuwa waliacha kujadili hoja kwa msingi unaozingatia masilahi ya taifa na badala yake kujikita kwenye itikadi za vyama vyao vya siasa.

Alisema hatua hiyo ndiyo iliyosukuma Bunge kupitisha muswada huo bila kuzingatia hitaji la wananchi wengi waliokuwa nyuma ya mchakato huo wakipinga kusomwa bila ya kufikishwa kwa wananchi ili watoe maoni yao. “Sisi Jukwaa la Katiba tunaamini muswada huo ndio msingi wa Katiba, wabunge walipaswa kujiuliza, je nyumba ikijengwa juu ya msingi dhaifu itaweza kudumu?” alihoji Kibamba na kuongeza;

“Muswada wa Katiba ambao hauna ridhaa ya wananchi utakuwa unatengeneza Katiba ya nani na kwa faida ya nani? Je wananchi ambao watakuwa hajawashiriki kuijenga msingi wa Katiba yao mpya watawezaje kushiriki kuijenga na kuandika Katiba yenyewe,” alihoji na kusema kama hawataweza watakuwa wanatengeza Katiba kwa faida ya nani.

Alisema Jukwaa la Katiba linaamini mchakato usio wahusishwa wananchi kutoka hatua za awali ambao ni kutengeneza sheria ya mabadilikoya Katiba haiweze kuwa na manufaa kwao.

“Kama Rais atasaini kunauwezekano mkubwa wa rasimu ya Katiba itakayopendekezwa kukataliwa na wananchi,” alisema. Mjumbe wa Jukwa hilo na Mkurungenzi Mtendaji wa Tamwa, Ananilea Nkya aliwatuhumu wabunge wanawake aliodai wamewaangusha watanzania.

“Tuliwategemea wabunge wanawake kuwa wakituwakilisha kwenye nafasi za maamuzi wangeweza kulisaidia taifa lakini ndio wamekuwa msitari wa mbele kutuangusha kwa kuchangia mijadala kwa kuangalia itikadi za vyama vyao vya siasa,” alisema Nkya. Nkya alisema wabunge hao badala ya kujadili hoja zenye kuleta maslahi kwa taifa walibadilika katika mjadala huo na kuanza kuzishambulia asasi za kiraia na watu waliotoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kusomwa muswada huo kwa mara ya pili.

Kwa upande wake, kaimu Katiba Mkuu wa Shirikisho la vyama vya wafanya kazi Tanzania (Tucta) Hezron Kaaya alisema kama Rais atasaini muswada huo wao wataunda chombo kitakachoratibu mchakato wa kukusanya maoni na kutengeneza rasimu ya Katiba nchi ya mfumo wa sasa.

“Hatuamini kama Rais hatatusikiliza, lakini kama atasaini sisi tutatengeneza chombo kitakachoratibu na kukusanya maoni ya wananchi kwa ajili ya kutengeneza rasimu ya Katiba mpya nje ya mfumo unaopendekezwa na serikali,” alisema Kaaya

Kaaya alisema Jukwaa hilo ambalo Tucta ni mwananchama wanataka Katiba itakayojibu mahitaji ya wananchi wote yakiwamo matatizo ya wafanya kazi huku akisistiza kuwa siku zote watawala uwa hawataki katiba inayoingilia masirahi yao.

“Sisi tunapinga utaratibu uliotumika kupitishwa muswada huo,kama utabaki kama ulivyo ndio utakaotumika katika kuandika katiba mpya ambayo haitakuwa tofauti nah ii tuliyonayo,” alisema Kaaya.

Alifafanua kuwa siku zote watawala huwa hawapendi Katiba inayoingilia maslahi yao na kufafanua vitendo vya ukukwaji wa haki za binadamu na ufisadi ni matokeo ya Katiba mbovu inayohusudiwa na watawala hao.

Alimtaka Rais kikwete kulifanya jambo zuri la pili kwa kama ilivyokuwa katika hotuba yake kwa kutosaini muswada huo kuwa sheria

Categories: