Lema awataka wafuasi wa Chadema gerezani


Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema),Godbless Lema.





Habari na Peter Saramba na Mussa Juma, Arusha.

MBUNGE wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ambaye yuko mahabusu, amewataka wafuasi wa chama hicho kumtembelea gerezani kwa wingi leo ambayo ni siku ya kawaida ya kuona mahabusu, akiwataka wasiwe na hofu yoyote kufanya hivyo.

Lema alituma ujumbe maalumu kwa wanachama wa chama hicho akiwataka kuwa watulivu na kumwunga mkono katika harakati zake alizoziita za kupigania haki, usawa na demokrasia ya kweli nchini bila kujali vitisho vya dola.

Katika ujumbe wake huo uliotolewa na Mwenyekiti wa Mfuko wa Maendeleo Arusha (ARDF), Elifuraha Mtowe aliyemtembelea gerezani jana, Lema alisema ameamua kuchukua dhamana ya kukubali kwenda magereza ili kufikisha ujumbe kwa dola na wote wenye kujaribu kuwatisha wenye nia na kiu ya kupigania haki na usawa na kwamba yuko tayari kulipia gharama yoyote kukamilisha ndoto yake.

Aliwataka wananchi kuchanga fedha kwa ajili ya watu aliowakuta Magereza wakitumikia vifungo baada kushindwa kulipa faini walizohukumiwa kwa kutiwa hatiani kwa makosa madogo na alisema tayari ameomba kwa uongozi wa Magereza, orodha ya waliofungwa walioshindwa kulipa faini.

Kwa mujibu wa Mtowe, Lema amewakaribisha wananchi kumtembelea gerezani katika utaratibu wa kawaida wa wafungwa na mahabusu kutembelewa siku za Jumatano, Jumamosi na Jumapili.

Alisema uongozi wa Chadema Mkoa wa Arusha utaratibu ziara hizo kuhakikisha sheria, taratibu na kanuni za Magereza zinazingatiwa kwa wenye nia hiyo.

Lema gerezaniOfisa mmoja mwandamizi wa Gereza la Arusha ambaye alikataa kutaja jina lake, alisema mbunge huyo alifikishwa gerezani hapo juzi saa 10:00 jioni akiongozana na watu wengine 12 waliomsindikiza ambao licha ya kutokuwa watuhumiwa wala wafungwa, walikuwa tayari kuingia naye mahabusu.

Alisema ili kumhakikishia usalama, mbunge huyo ametengewa chumba maalumu na haruhusiwi kukutana na wafungwa au mahabusu wengine.

“Mheshimiwa Lema tumempokea vyema, tumempangia chumba chake maalumu na tumemweleza kuwa haruhusiwi kukutana na wafungwa au mahabusu wengine ingawa yeye alipendelea kuchanganywa kwenye seli ya kawaida ili achanganyike na mahabusu wengine.
Hana shida yoyote na jana alitembelewa na mkewe (Neema Lema), watu wasiwe na hofu yoyote kwani anatendewa haki sawa na wengine,” alisema ofisa huyo kwa simu jana.”

Alikanusha habari zilizozagaa mjini Arusha kuwa baada ya Lema kufikishwa gerezani, kulitokea mtafaruku wa wafungwa na mahabusu kupiga kelele kupinga uonevu wa vyombo vya dola, dhidi ya mbunge huyo kijana.

Ilidaiwa kelele na vurugu hizo za wafungwa na mahabusu zilitokana na redio moja ya mjini hapa kurusha hewani waraka maalumu wa Lema, akitangaza hiari yake ya kwenda mahabusu.

Hata hivyo, Kaimu Mkuu Magereza Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Marcel Lorry hakutaka kuzungumza lolote kuhusu suala hilo akisema anayeweza kufanya hivyo ni mkuu wa gereza alipo Lema jambo ambalo pia halikuwezekana.

Bavicha wachukizwa
Nalo Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) Mkoa wa Arusha, limemtaka Mkuu wa Polisi (IGP), Said Mwema kumng'oa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha (OCD), Zuberi Mwombeji kutokana na kile wanachodai kuwa ni kuwaonea viongozi na wafuasi wa chama hicho.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jana,  Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Arusha, Ephata Nanyaro alisema wamechoka kunyanyaswa, kukamatwa ovyo, kupigwa na
kudhalilishwa na OCD huyo.

Mwenyekiti huyo wa Bavicha alitoa mfano wa jeshi la polisi kushindwa kuwachukulia hatua vijana wa CCM (UVCCM), walioongozwa na Kaimu Mwenyekiti wao wa Taifa, Benno Malisa kufungua matawi mjini hapa, kuandamana na kufanya mkutano wa hadhara bila kibali cha jeshi hilo licha ya shughuli hiyo kupigwa marufuku na OCD huyo aliongoza ulinzi katika shughuli hiyo haramu.

“Kaimu RPC (Kamanda wa Polisi Mkoa) alikiri kwamba vijana hao wa CCM walikaidi amri halali ya polisi. Badala ya kukamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria, alitoa onyo. Maana yake ni kwamba utekelezaji na utendaji wa polisi Arusha unazingatia nani mhusika katika kosa na ana itikadi gani,” alidai Nanyaro.

Awali, Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa alisoma taarifa ya kurasa tatu ambayo pamoja na mambo mengine, alitaja mambo mawili ya msingi yanayopaswa kushughulikiwa sasa na kwa haraka kurejesha amani, utulivu na maendeleo ya Arusha kuwa ni pamoja na vyombo vya dola kukomesha uonevu wenye lengo la kujenga hofu kwa wananchi, wanachama wa Chadema, viongozi wao.

Golugwa alisema msingi wa maendeleo ya jamii yoyote ni haki na usawa kwa wote na kutaka jeshi la polisi kuzingatia misingi ya sheria katika kutekeleza wajibu na dhamana waliyokabidhiwa na umma.

Chanzo: MWANANCHI

Categories: ,