Mabasi 14 ya Dar Express yafungiwa





Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko

MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imezuia mabasi 14 ya Dar Express kutoa huduma ya usafiri katika mikoa ya Dar es Salaam Arusha na Tanga kuanzia kesho hadi yatakapokaguliwa. 

Hatua hiyo imefikiwa baada ya kubainika kwamba mabasi hayo kuanzia Januari mwaka huu hadi sasa, yamehusika katika matukio ya ajali katika maeneo mbalimbali nchini. 

Hayo yalisemwa jana na Meneja Mawasiliano kwa Umma wa Sumatra, David Mziray, alisema pamoja na kutokea kwa ajali hizo, mmiliki wa Dar Express hakutoa taarifa za matukio hayo kwa Mamlaka kama sheria inavyotaka. 

Alisema huo ni ukiukaji wa kanuni namba 22 ya kanuni za Ufundi na Usalama na Ubora wa Viwango vya Huduma zinazotolewa kwa magari ya abiria za mwaka 2008. 

“Mabasi hayo yataruhusiwa kuendelea kutoa huduma ya usafiri katika njia hizo baada ya Mamlaka kupokea taarifa za ukaguzi zinazothibitisha kuwa yanakidhi viwango vya ubora na kwamba madereva wake wana sifa za kuendesha mabasi hayo,” alisema Mziray. 

Alisema ukaguzi wa mabasi yaliyosimamishwa utafanywa na Mkaguzi wa Magari kutoka Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani na mmiliki wake ameelekezwa kuwasiliana na Mkaguzi huyo, ili kwa pamoja wapange namna ya kufanikisha ukaguzi huo. 

Alitaja magari hayo kuwa ni yenye namba T844BDR; T845ASZ; T161BLB; T168BCB; T663AXL; T120BPQ; T979BPP; T640AXL; T833BDR; T255BLC; T172BLC; T637AXL; T666AXL na T311ANX. 

Alisema ili kujiridhisha na sifa za madereva na viwango vya ubora wa magari yanayomilikiwa na kampuni hiyo, Mamlaka kupitia kifungu namba 15 cha Sheria ya SUMATRA namba 9 ya mwaka 2001, imeiagiza kusitisha utoaji huduma kwa magari yake yote yanayotoa huduma kati ya Dar – Arusha na Arusha Tanga kuanzia kesho. 

Alitaja baadhi ya ajali zilizotokea kuwa ni ya Januari 4 ambapo basi namba T311ANX lilimgonga mpanda pikipiki na kumsababishia kifo katika maeneo ya Kifaru, Mwanga, mkoani Kilimanjaro na kwa mujibu wa taarifa za Jeshi la Polisi, chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi. 

Nyingine ilitokea Oktoba 24 ambapo basi namba T637AXL liligonga gari lingine kwa nyuma namba T185ARX/T457ARU na kuacha njia na kupinduka maeneo ya Kitumbi, Korogwe. Katika ajali hiyo watu tisa walijeruhiwa na kwa mujibu wa taarifa za Polisi, chanzo cha ajali hiyo ni dereva kupita gari la mbele yake kwenye kona. 

Agosti Sumatra ilifungia kwa muda usiojulikana mabasi ya kampuni ya Champion, ili kuyafanyia uchunguzi, kutokana na ajali ya basi namba T763AEQ lililopinduka eneo la Nara, Dodoma na kusababisha vifo vya watu wanane na kujeruhi wengine 52. 

Septemba Mamlaka hiyo ikafungia mabasi yote ya Kampuni ya Allys Sports, ili ichunguze ubora wa mabasi hayo na uwezo wa madereva, kutokana na kuhusika na ajali za mara kwa mara. 

Mwezi jana Mamlaka hiyo ilifungia basi la Deluxe Coach kwa siku 30 kuanzia Oktoba 30, 2011 baada ya kuhusika na udanganyifu katika biashara yake ya usafirishaji. Basi hilo lilipasuka tairi la mbele na kupinduka kabla halijashika moto ulioteketeza watu kadhaa.

Categories: