Balozi wa Afrika ya Kusini, Bw. Henry Chiliza, akiweka shada la maua kwenye moja ya makabuli ya wapigania uhuru wa nchi hiyo, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Maridhiano na kumbukumbu ya mapambano ya ukombozi Kusini mwa Afrika, yaliyofanyika kwenye kambi ya Dakawa, mkoani Morogoro juzi.
*****
UBALOZI wa Afrika Kusini nchini, juzi uliadhimisha kumbukumbu ya askari wake ambao walipoteza maisha katika harakati za kupigania uhuru wa nchi hiyo katika eneo la Dakawa, mkoani
Morogoro.
Maadhimisho hayo yalifanyika katika makaburi ya mashujaa hao ambapo viongozi mbalimbali, waliweka mashada ya maua akiwemo Balozi wa Afrika Kusini nchini Bw. Thanduyise Chiliza ambaye alisema, Tanzania ilitoa mchango mkubwa katika kupigania uhuru wa nchi hiyo ambayo hivi sasa wanasherehekea miaka 19 ya uhuru.
“Wapigania uhuru wa Afrika Kusini waliandaliwa hapa Dakawa, tutaendelea kuwakumbuka na kuenzi mchango uliotolewa na Tanzania katika harakati za ukombozi wa nchi yetu,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa huo, Bw. Joel Bendera, alisema uhuru wa nchi hiyo ulipatikana mwaka 1994 baada ya kumalizika kwa ubaguzi wa rangi ambapo Tanzania ilitoa msaada mkubwa pamoja na eneo hilo kwa ajili ya wapiganaji waliokuwa wakiwindwa na utawala wa kikoloni.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro Bw. Petro Kingu, alisema ushirikiano wa chama hicho na kile cha Afrika Kusini cha African National Congress (ANC), hauwezi kusaulika wala kuvunjika kutokana na uhusiano mzuri ambao ulianza muda mrefu na kuleta mafanikio makubwa.
Alisema licha ya ushirikiano huo pia maridhiano ni muhimu kwa kuwa wapo watu wanaoishi Tanzania lakini wazazi wao wako Afrika ya Kusini ambapo huo ni undugu wa damu.
Bw. Brian Magazi ambaye alifika katika maadhimisho hayo nchini Afrika Kusini, alisema amefurahi kuona makaburi ya wenzao ambao walionesha uzalendo wa kupigania uhuru wa nchi hiyo na kuwafanya raia wa nchi hiyo waishi kwa amani.
“Nimejifunza uzalendo kwa ajili ya kizazi kijacho kwani wapigania uhuru kwa sasa hawapo hivyo sisi tunafaidi matunda yao,” alisema.
Categories: