MAMENEJA TANROADS MIKOANI WABADILISHWA

*Lengo ni kuongeza ufanisi usimamizi miradi

Na Mwandishi Wetu

MTENDAJI Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, amefanya mabadiliko makubwa katika safu ya Mameneja kwenye
katika mikoa yote 25 ya Tanzania Bara.

Mabadiliko haya yamelenga kuongeza ufanisi wa kusimamia miradi ya barabara hasa mikoani ambapo mameneja, sasa watawajibika kusimamia ubora wa kazi, miradi kuhakikisha miradi iliyopo katika mikoa yao inatekelezwa kwa kuhakikisha thamani ya fedha zilizotumika ‘value for money’ inazingatiwa.

Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Wizara ya Ujenzi Dar es Salaam jana, Bw. Martin Ntemo, alisema katika mabadiliko hayo, kuna mameneja wapya saba na wengine watano, wamehamishwa vituo, wanne wamepelekwa katika mikoa mipya na tisa wamebaki katika vituo vyao vya zamani.

Mameneja saba wapya ni pamoja na Mhandisi Julius Ndyamukama ambaye kituo chake cha kazi kitakuwa Dar es Salaam ambapo awali alikuwa TANROADS Makao Makuu akiwa amechukua nafasi ya Bw. James Nyabakari aliyehamishiwa mkoani Mbeya.

Mhandisi Lucian Kileo aliyekuwa mkoani Mbeya atapangiwa kazi nyingine ambapo Mhandisi Mwita Rubirya amepelekwa mkoani Kilimanjaro, akitokea Wizara ya Ujenzi Makao Makuu. Mhandisi Tumaini Sarakikya, aliyekuwa Meneja mkoani humo, amehamishiwa mkoani Pwani.

Wengine ni Mhandisi Isaac Mwanawima, ambaye amehamishiwa Mkoa wa Lindi akitokea Makao Makuu ya Wizara ya Ujenzi, akichukua nafasi ya Mhandisi Michael Kulaya, anayehamia TANROADS Makao Makuu.

Mhandisi Dorothy Mtenga, amepelekwa mkoani Morogoro akitokea Dodoma ambaye anachukua nafasi ya Mhandisi Charles Madinda ambaye kwa sasa amehamishiwa Makao Makuu.

Mwingine ni Mhandisi Augustine Philip ambaye amepelekwa mkoani Shinyanga, akitokea TANROADS Dar es Salaam ambaye anachukua nafasi ya Mhandisi Damian Ndabalinze aliyehamishiwa mkoani Tabora.

Mhandisi Florian Kabaka amehamishiwa mkoani Rukwa akitokea TANROADS Makao Makuu, ambaye anachukua nafasi ya Mhandisi Joseph Nyamhanga aliyeteuliwa kukaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Barabara, Wizara ya Ujenzi.

Nafasi hiyo ya Mkurugenzi wa Barabara ilikuwa wazi baada ya Mhandisi Mussa Iyombe kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Pia Mhandisi Isaack Kamwelwe, amehamishiwa Mkoa mpya wa Katavi akitokea Wizara ya Ujenzi Makao Makuu.

Mameneja watano waliohamishiwa mikoa mingine ni Mhandisi Damian Ndabalinze ambaye amepelekwa mkoani Tabora akitokea Shinyanga. Mhandisi Ndabalinze amechukua nafasi ya Mhandisi Partson Masebo aliyehamishiwa Makao Makuu.

Mhandisi Tumaini Sarakikya, maepelekwa Mkoa wa Pwani akitokea Mkoa wa Kiliamnjaro. Aliyekuwa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani Mhandisi Gabriel Mwikola, amepelekwa mkoani Mtwara ambapo Mhandisi Mussa Mataka aliyekuwa Meneja mkoani humo, amepangiwa Tanroads Makao Makuu.

Mwingine ni Mhandisi James Nyabakari amepelekwa mkoani Mbeya akitokea Dar es Salaam.

Alisema mameneja wanne waliopangiwa mikoa mipya ni Mhandisi Haruna Senkuku, ambaye anakwenda Mkoa wa Geita akitokea Mkoa wa Kigoma. Nafasi yake kwa Mkoa wa Kigoma inafanyiwa kazi.

Mhandisi Isaack Kamwelwe amepelekwa Mkoa wa Katavi ambapo awali alikuwa Makao Makuu Wizara ya Ujenzi.

Mhandisi Yusuf Mazana amepelekwa Mkoa wa Njombe akitokea TANROADS mkoani Ruvuma. Mhandisi Emanuel Kibeya amepelekwa Mkoa wa Simiyu akitokea mkoani Tabora.

Mameneja tisa waliobaki katika vituo vyao vya zamani ni Mhandisi Deusdedit Kakoko (Arusha), Mhandisi Leonard Chimagu (Dodoma), Mhandisi Poul Lyakurwa (Iringa), Mhandisi Johnny Kalupate (Kagera) na Mhandisi Emmanuel Korosso (Mara).

Wengine ni Mhandisi Yohani Kasaini (Manyara), Mhandisi Leonard Kadashi (Mwanza), Mhandisi Yustaki Kangole (Singida) na Mhandisi Alfred Ndumaro (Tanga).

Categories: