HATMA YA JAIRO, LUHANJO MIKONONI MWA PINDA

Na Mwandishi Wetu
*Bunge lasema limemaliza linasubiri maamuzi ya serikali
*Wanasheria: Wabunge walikosea njia kuandaa taarifa ya kamati

SIKU 15 baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuazimia serikali kuwachukulia hatua za kinidhamu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Bw. David Jairo,
Katibu Mkuu Kiongozi Bw. Philemon Luhanjo huku Mkaguzi na Mdhibiti na Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bw. Ludovick Utoh, pia akituhumiwa kwa kushindwa kufanya kazi yake, hatma ya viongozi hao sasa ipo mkononi mwa Waziri Mkuu Mizengo pinda.

Bw. Jairo anadaiwa kuchangisha fedha kinyume cha sheria kwa ajili ya kuwezesha kupitishwa kwa bajeti ya wizara hiyo kinyume cha taratibu huku Bw. Luhanjo akidaiwa kumkingia kifua kiongozi huyo kwa kutoa hukumu bila kuhusisha Bunge lililoibua suala hilo.

Bw. Utoh anadaiwa na bunge kushindwa kazi yake kwa kutoa taarifa inayodaiwa kumsafisha Bw. Jairo kinyume na hali halisi.

Vyanzo vya habari ndani ya serikali vilieleza Majira kuwa tayari Ofisi ya Bunge imewasilisha taarifa za azimio la Bunge serikalini kwa Waziri Mkuu kama msimamizi wa shughuli za serikali ndani ya bunge na mtekelezaji wa shughuli za kila siku za serikali.

"Hivi sasa hatma ya akina Jairo na Luhanjo pamoja na Ngelenja zipo mkononi mwa Pinda, tayari amepewa taarifa ya azimio la Bunge tangu wiki iliyopita, "kilisema chanzo chetu ndani ya serikali.

Akizungumza na Majira Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashililla, alikiri Ofisi ya Bunge kuwasilisha taarifa hiyo serikalini na kuongeza kuwa kwa kawaida huchukua muda wa saa 72 tu kuwasilisha Azimio la Bunge serikalini kama hakuna tatizo lolote.

"Ni kweli ofisi ya bunge imewasilisha taarifa ya azimio la bunge serikalini, kwa kawaida sisi tunawasilisha taarifa kama hiyo ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye ndiye Mkuu wa shughuli za serikali ndani ya Bunge," alisema Dkt. Kashililla na kuongeza.

Kwa kawaida tunachukua saa 72 tu kuwalisilisha azimio la bunge serikalini baada ya bunge kuahirishwa, sisi kama bunge tumemaliza kazi yetu labda tusubiri tu maamuzi ya serikali," alisema.

Majira lilipofika ofisi ya Waziri Mkuu kuomba ufafanuzi wa suala hilo lilijibiwa kuwa Bw. Pinda yupo katika ziara za kikazi nje ya Mkoa.

Majira ilipofika ofisi ya Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge Bw. William Lukuvi, ambaye kwa kawaida hupokea ripoti hizo kabla ya kumfikia Waziri Mkuu naye hakuwepo ofisini.

"Mheshimiwa Waziri hayupo tangu wiki iliyopita, alikuwa kwenye maadhimisho ya siku ya UKIMWI, hajafika ofisini bado, huenda atafika kesho (leo), yeye ndiye anaweza kusema lolote juu ya suala hilo, vuta subira," alisema mmoja wa wasaidizi wa waziri huyo.

Hata hivyo baadhi ya wanasheria waliozungumza na Majira kuhusu suala hilo walidai kuwa baada ya kupitia taarifa ya Bunge walibaini kuwa chombo hicho kilikosea baadhi ya vipengele vya taarifa ya Kamati Teule iliyochunguza suala hilo hivyo kuonesha wasiwasi iwapo serikali itachukulia hatua stahili kama ilivyoshauriwa dhidi ya wahusika.

Awali akiwasilisha taarifa ya uchunguzi juu ya sakata hilo la kuchangisha fedha kinyume na taratibu, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Bw. Ramo Makani (CCM) alisema kutokana na utaratibu huo ni vyema Bunge likaendelea kukemea kwa nguvu zote utaratibu wa uchangishaji wa fedha uliofanywa na wizara hiyo.

"Kamati teule inapendekeza kwamba serikali ichukue hatua za kinidhamu kwa ndugu David Kitundu Jairo, kwa matumizi mabaya ya madaraka, kukusanya na kutumia fedha za serikali kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za umma na kuruhusu matumizi mabaya ya fedha za umma," alisema.

Mbali na hatua hizo kwa Bw. Jairo pia kamati hiyo imependekeza watumishi wote wa wizara hiyo ambao waliainishwa katika taarifa yao wachukuliwe hatua za kisheria.

"Aidha, kwa kuwa waziri kwa mujibu wa mwongozo wa Baraza la Mawaziri ndiye msimamizi mkuu wa wizara, hivyo suala la uchangishaji halikupaswa kufanyika bila yeye kufahamu, kamati Teule inapendekeza serikali ichukue hatua zinazofaa kwa Waziri wa Nishati na Madini, mheshimiwa William Ngeleja ambaye ni mbunge," alisema Bw. Makani.

Alisema kamati yake ilisitisha na jinsi Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG),Bw. Ludovick Utoh kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake kikamilifu.

"Hususan katika kulisaidia Bunge na umma kwa ujumla, Kamati teule inapendekeza serikali ichukue hatua zinazofaa kwa CAG kwa upotoshaji huo," alisema Bw. Makani.

Katika hatua nyingine kamati hiyo ilipendekeza Katibu Mkuu Kiongozi, Bw. Phileom Luhanjo achukuliwe hatua zinazofaa na serikali.

"Katibu Mkuu kiongozi kwa makusudi aliamua kumsafisha ndugu David Kitundu Jairo kwa kufisha ukweli wa taarifa ya ukaguzi maalumu uliofanywa na mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali na kuamua kwamba ndugu Kitundu Jairo hakuwa na kosa la kinidhamu,kitendo ambacho kimeupotosha umma na Bunge," alisema Bw. Makani.

Categories: