Na Daud Magesa, Mwanza
*Mkuu wa kituo adaiwa kurejesha 20,000 ya dhamana
ASKARI Polisi wa Kituo Kikuu cha Polisi Kati Nyamagana jijini Mwanza, wamenusurika kipigo baada ya wananchi wa Kitongoji cha Nyambiti, Kata ya Nyakato,
Wilaya ya Ilemela mjini hapa kuwaweka chini ya ulinzi kwa madai ya kuchoshwa na kukamatwa kinyume cha utaratibu.
Habari kutoka eneo la tukio zilieleza kuwa askari hao walifika katika kitongoji hicho saa 4:00 asubuhi, Desemba 2, mwaka huu kuendesha msako wa pombe haramu ya gongo na kuwakamata baadhi ya wananchi wakiwa wanakunywa pombe hiyo.
Baada ya kuwafunga pingu waliwapeleka watuhumiwa hao Kituo Kidogo cha Polisi ESSO Mabatini mjini hapa na kwamba baada ya kuwafikisha kituoni hawakufunguliwa jalada lolote badala yake walitakiwa wajidhamini wenyewe kwa sh.20,000 na kwamba walifanikiwa kisha kukabidhi fedha hizo kwa mkuu wa kituo hicho kisha kuachiwa.
Ilidaiwa kuwa askari hao walirejea tena katika kitongoji hicho wakiwa na pingu bila silaha na kuwakamata watu wengine wawili kisha kuwatia pingu kwa madai hayo hayo ya kukutwa wakinywa pombe ya gongo.
Wananchi wa eneo hilo waliamua kuingilia kati suala hilo kuwazuia askari hao kuondoka na watuhumiwa hao wakihoji msako huo kuendeshwa bila kuwahusisha viongozi wa serikali ya mtaa huo ambao walidaiwa kutokuwa na taarifa za kuwepo kwa kazi hiyo.
Baada ya mahojiano hayo wananchi hao waliwaweka chini ya ulinzi askari hao akiwemo mwanamke mmoja aliyefanikiwa kukimbia na kuelekea kusikojulikana huku wenzake waliobaki wakiamriwa kuwafungua pingu watuhumiwa waliokuwa wamewakamata kwa madai kuwa wamevunja taratibu za kazi zao.
Ilidaiwa kuwa baada ya askari hao kuona wako katika hali ya hatari walimpigia simu Mkuu wa Kituo cha Esso ili awaletee funguo za pingu haraka na kwamba kiongozi wao huyo aliitikia wito huo kisha watuhumiwa hao kufunguliwa.
Hata hivyo mkuu huyo wa kituo naye 'alionja joto la jiwe' baada ya wananchi hao kumtaka arudishe sh. 20,000 anazodaiwa kupewa na wananchi sita waliofikishwa kituoni kwake kwa madai ya kukutwa wakiwa wanakunywa gongo kwa kujidhamini wenyewe na kwamba alirudisha fedha hizo.
Kutokana na tukio hilo askari hao watatu kati ya wanne waliohusika katika tukio hilo waliotajwa kuwa ni MG 201601 Issa Abdalah, MG 201165 Odila John na MG 223115 Jonas Machage, walidaiwa kuwekwa mahabusu katika Kituo cha Polisi cha Kati Nyamagana kwa mahojiano zaidi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, alipoulizwa kuhusu tukio hilo alisema alikuwa safarini na kumtaka mwandishi wa habari hizi kuwasiliana na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana (OCD) kwa taarifa zaidi huku akihoji fedha hizo zilizodaiwa kuwa ni za dhamana walikuwa wanazipeleka wapi.
"Mimi niko safarini, wasiliana na OCD wa Nyamagana akupe taarifa kama wanashikiliwa ama la, mimi sijui lolote, hivi hizo fedha walikuwa wanazipeleka wapi?" Alisema RPC Barlow kwa njia ya simu yake ya mkononi.
Hata hivyo OCD wa Nyamagana Kisusi alipotafutwa kwa njia ya simu alisema si msemaji wa polisi na kumtaka mwandishi kuwasiliana na RPC.
Hata hivyo Mkuu wa Kituo cha Polisi Mabatini ESSO alipopigiwa simu kuhusu madai ya kuwatoza sh. 20,000 wananchi sita waliotuhumiwa kukamatwa na gongo na kufikishwa kituoni kwake alisema hayo ni majungu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa Nyambiti, Bw. Abel Mwesa, alithibitisha askari hao kufika katika mtaa
wake na kuendesha msako haramu bila uongozi kuwa na taarifa na kudai kuwa hata pombe waliyokutwa wakinywa wananchi hao si haramu kama ilivyodaiwa.
Aliwataja wananchi waliokumbwa na mkasa huo kuwa ni Kundi, wanawake wawili, Bruno Sigonda, Manyama, Kiseri Hamis.
CHANZO: MAJIRA
Categories: