Na Moses Mabula, Uyui
MAHINDI ya msaada gunia 41 zilizotolewa katika Kijiji cha Tambukareli, Wilaya ya Uyui, mkoani Tabora, yamepotea katika mazingira ya
kutatanisha.
Akizungumza na Majira, Diwani wa Kata ya Nsololo katika kijiji hicho, Bw.Abbas Kibiriti, alisema mahindi hayo yamepotea juzi mchana na kusababisha wananchi kutishia maisha ya Mtendaji wa Kijiji hicho, Bw.Mohamed Kudema na mgambo wawili, Bw.Juma Mpina na Bw.Rajab Mbena, ambao wamekimbia kusikojulikana ili kunusuru maisha yao.
Alisema mahindi hayo yalikuwa gunia 158 ambapo gunia 25, ziligawiwa kwa wananchi na kubaki gunia 92 ambazo kati ya hizo, 44 ndio zimepotea katika mazingira tata yakiwa yamehifadhiwa katika darasa la Shule ya Msingi Nsololo.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Stanley Kolimba, amethibitisha kupotea kwa mahindi hayo na kuagiza Bw.Kudema na Mwenyekiti wa kijiji hicho wakamatwe kutokana na upotevu huo.
“Naomba Jeshi la Polisi lifanye upelelezi wa kina ili kujua mahindi haya yamepotea katika mazingira gani bila wahusika kukamatwa wala kujulikana yalipo,” alisema.
Aliagiza kukamatwa kwa viongozi wa kijiji na walinzi ili ukweli uweze kupatikana, kwani wananchi wanahitaji kupatiwa mahindi hayo ambayo yametolewa na Serikali kukabiliana na tatizo la njaa.
“Haya mahindi hayajapotea kama viongozi wa kijiji wanavyosema bali yameibiwa, kwa nini yasipotee magunia yote, kuna watu wanajua ukweli wa mahindi haya na yapo wapi.
“Mkono wa Seriakali ni mrefu, utawakamata wote waliohusika na wizi huu na kuwafikisha katika vyombo vya sheria ili wajibu mashtaka,” alisema Bw. Kolimba.
Categories: