VIGOGO WA TANAPA WAMKERA KIKWETE


*Asema wanalipana posho badala ya kutangaza utalii
*Ataka juhudi ziongezwe kutangaza vivutio vilivyopo
*Asisitiza kiwango cha watalii kwa mwaka hakijafikiwa

****

Na Rabia Bakari

RAIS Jakaya Kikwete, amekasirishwa na kitendo cha viongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), kushindwa
kutangaza vya kutosha sekta ya utalii nchini huku wakizunguka dunia na kulipana posho.

Alisema Tanzania ina vivutio vingi vya utalii lakini idadi ya watalii wanaotembelea vivutio vilivyopo si ya kuridhisha kwa sababu havijatangazwa ipasavyo.

Rais Kikwete aliyasema hayo juzi katika uzinduzi wa kampasi ya Chuo cha Taifa cha Utalii Dar es Salaam.

“TANAPA wana fedha nyingi sana lakini wanazitumia kugawana posho na wajumbe wa NCAA kuzunguka katika nchi mbalimbali alafu tunabaki kulalamika wakati nchi jirani ya Kenya inatangaza kuwa mlima Kilimanjaro upo nchini kwao.

“Ukweli ni kwamba mlima Kilimanjaro upo Tanzania sasa tangazeni watu wafahamu badala ya kulalamika, pungezeni posho mnazolipana ili mpate fedha za kujitangaza katika soko la dunia,” alisema.

Aliziagiza mamlaka hizo, kushirikiana na kampuni zinazotoa huduma za utalii nchini kwa kukaa pamoja na kuweka mikakati ya kuchangia ili kutangaza utalii kwa sababu kampuni hizo nazo zinafaidika na vivutio vilivyopo.

“Sisi tuendelea kutangaza ila sizungumzii Serikali bali mashirika ambayo yananufaika na vivutio vyetu yachangie kutangaza utalii uliopo maana wao wananufaika japo nasi tutapata kodi kidogo,” alisema Rais Kikwete.

Alisema kwa miaka kadhaa sasa, Tanzania imeweka kiwango cha kutembelewa na watalii milioni moja kwa mwaka lakini hadi sasa wamefikisha 700,000 hivyo pengo lililopo ni watalii 300,000.

Aliongeza kuwa, baadhi ya nchi hazina vivutio vizuri wala idadi kubwa ya vivutio kama vilivyopo nchini lakini wamekuwa wakipokea idadi kubwa ya watalii kutokana na matangazo.

“Haitoshi kutangaza vivutio vyetu nchini Marekani pekee, tangazeni na Ufaransa, Japan na kwingineko kwa lugha za mahali husika, kwani kila mahali wanatumia lugha yao tu, tatizo la Watanzania wanajua kuwa kila mtu kutoka nje anajua Kingereza.

“Tutafanikiwa zaidi kama huduma zinazotolewa katika hoteli zetu zitakuwa nzuri, huduma zikiwa mbovu hata tuwe na vivutio kiasi gani hatuwezi kupaata kitu,” alisema.

Alisema ndoto ya Tanzania kuwa na Chuo cha Utalii chenye hadhi ya kimataifa imetimia baada ya kukamilika kwa kampasi hiyo ambayo imejengwa kwa ushirikiano mkubwa wa Serikali ya Ufaransa.

“Tunataka hadhi ya chuo hiki isishuke ili wanaotoka hapa waweze kufanya kazi sehemu yoyote duniani, inasikitisha ukienda baadhi ya nchi unakuta katika sekta ya hoteli wenzetu Wakenya wanafanya kazi lakini sisi tunashindwa kufika huko kwa sababu ya viwango,” alisema.

Awali akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Ezekiel Maige, alisema sekta ya utalii inachangia asilimia 17.2 ya pato la taifa ambapo pato hilo linazidi kukua.

Mkuu wa chuo hicho Bi. Agnes Mziray, alisema kuanzishwa kwa kampasi hiyo, kunafanya Chuo cha Utalii kufikisha kampasi tatu.

Categories: