WAISLAMU KUANDAMANA

*Wapinga maridhiano ya serikali, makanisa
*Wataka Mahakama ya Kadhi

Na Rehema Maigala

UMOJA wa Wahadhiri wa Dini ya Kiislamu nchini, umeandaa maandamano nchi nzima kwa madai ya kupinga mkataba uliofikiwa kati ya Serikali na makanisa ili
kutoa huduma za kijamii, elimu na afya.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kiongozi wa umoja huo Bw.Kondo Bungo, alisema mkataba huo umelenga kuifilisi nchi na kutajirisha makanisa husika.

Alisema maandamano hayo yamepangwa kufanyika Desemba 23 mwaka huu ambapo mkataba huo, hauna ridhaa ya wananchi ndio maana Serikali imeufanya siri kwa kuyapa makanisa mabilioni ya fedha ili kuimarisha huduma hizo.

“Lengo jingine la kufanya maandamano haya ni kushinikiza uwepo wa Mahakama ya Kadhi ambayo itawezeshwa na Serikali kama ilivyo katika nchi nyingine.

“Huduma katika hospitali nyingi za Serikali zimedorora sasa badala ya kuziimarisha, wao wanatoa fedha nyingi na kuzipeleka kwenye makanisa ili yajiimarishe katika shule na hospitali zao,” alisema.

Aliongeza kuwa, Tanzania ni nchi maskini tangu ipate uhuru ambapo bajeti ya Serikali zaidi ya asilimia 60 inatokana na fedha za wahisani na nyingine wanakopa katika taasisi za fedha.

Bw.Bungo alisema, huduma za afya na elimu ambazo zinatolewa na makanisa ni miradi yao ndio maana hakuna hospitali wala shule za kanisa zinazotoa huduma bure ambapo mapato ya miradi husika yanatumika kuimarisha makanisa hayo.

Alisema maandamano hayo kwa wakazi wa mikoani, yataelekea katika Ofisi za Wakuu wa Mikoa husika ambapo Dar es Salaam yataanzia Mnazi Mmoja kwenda katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw.Mizengo Pinda.

“Zaidi ya miaka 20, madai haya yameshindwa kupatiwa ufumbuzi wa kudumu mbali ya kuyafikisha katika ngazi zote muhimu, njia za kidiplomasia zimetumika lakini hazijaleta tija zaidi ya kudharauliwa, kukebehiwa na kupuuzwa hivyo tumeona ni vyema tuwakilishe madai yetu kwa kufanya maandamano,” alisema.

Categories: