KUTOKANA na kuendelea kwa hali ya utoaji huduma isiyoridhisha katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa mgomo unaoendelea, madaktari bingwa wa hospitali hiyo wamekubaliana kuifuata Serikali kuzungumzia matatizo yaliyopo, ili yamalizwe kabla athari zaidi hazijawafika wagonjwa.
Wakati wakikubaliana hivyo katika kikao na Menejimenti ya Hospitali hiyo Dar es Salaam jana, uongozi wa MNH ulikiri kuwapo hali mbaya ya huduma mahali hapo tangu Januari 25 na kueleza kuwa, ndiyo iliyowasukuma madaktari hao kukutana na Waziri Mkuu kushawishi suluhu ya haraka.
Huku hao wakiamua hivyo na kuunda Kamati ya Madaktari Bingwa watano watakaotekeleza jukumu hilo wakati wowote kuanzia leo, Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya Taifa (TUGHE) kimewaomba madaktari waliogoma warejee kazini, ili kutoa nafasi ya kumalizwa kwa mgogoro huo wa maslahi kati yao na Serikali.
Dakika chache baada ya kumalizika kwa mkutano wa mabingwa hao na Menejimenti yao, uliodumu zaidi ya saa nne, Ofisa Habari Mwandamizi wa MNH, Aminiel Algaesha, aliwaambia
wanahabari kuwa wanafanya kila wawezalo kuhakikisha mgomo unamalizwa kwa mazungumzo na Serikali, ili kurejesha hali nzuri ya utoaji huduma kwa wagonjwa.
“Madaktari bingwa wameonesha kutoridhishwa na hali ya wagonjwa kutoonwa wala kutibiwa, wanaumizwa pia na kupungua kwa mahudhurio ya wagonjwa na ndiyo maana wameendelea kuwajibika na kusisitiza umuhimu wa wao kukaa na Serikali kuzungumzia maslahi ya madaktari kwa jumla licha ya matatizo yanayofahamika kuwa chanzo cha migomo.
“Hakuna anayetaka migomo iendelee kwa madaktari nchini, kwa sababu ina athari mbaya. Huu wa sasa umesababisha madhara mengi kwa wagonjwa na madaktari wetu hawa wameona waingilie kati, kwa imani kwamba huenda Serikali ikafanya namna na kuweka mambo sawa,” Algaesha alisema.
Alisisitiza kuwa hali bado haijatengemaa hospitalini hapo, kwa sababu idadi ya wagonjwa inaongezeka kwa kasi ndogo sana hadi 25 jana ikilinganishwa na 60 hadi 70 kabla ya
mgomo kwa siku. Akitoa maelezo kuhusu Kamati hiyo, Algaesha alisema haihusiani na
ya Jumuiya ya Madaktari walio kwenye mgomo, kwa sababu inaundwa na madaktari bingwa wasio kwenye mgomo.
“Majina ya wanakamati hiyo ndogo yatatajwa baadaye, lakini kwa ufupi haina uhusiano na ya madaktari wanaogoma. Hawa ni mabingwa waliokuwa kazini siku zote tangu tatizo hilo lianze”. Naibu Katibu Mkuu wa Tughe, John Sange, aliwasihi madaktari warejee kazini kwa maelezo kuwa mgogoro wao wa kimaslahi na Serikali unatafutiwa ufumbuzi wa mazungumzo kwa kuwa unazungumzika.
Alisema ingawa chanzo chake ni Serikali kushindwa kutekeleza mkataba iliyowekeana na madaktari kipindi cha nyuma kuhusu mambo mengi yakiwamo ya maslahi, itakuwa ni busara kuingia kazini kuokoa maisha ya wananchi wanaoumwa wakati ufumbuzi ukitafutwa. “Tughe inaunga mkono madai yote ya madaktari na tunaisihi Serikali isiendelee na msimamo wake mkali, kwa sababu unaweza kuleta athari mbaya zaidi kwa wagonjwa.
Tuna imani kuwa mgogoro huu unaweza kutatuliwa kwa kukaa mezani na kuzungumza na si kuvutana,” Sange alisema.
Madai ya wauguzi
Pamoja na kusisitizia madai ya madaktari, Tughe pia imeitaka Serikali iangalie namna ya kurejesha Kurugenzi ya Wauguzi Muhimbili kwa kuwa wenyewe wanaihitaji. Sange alisema mbali ya kulilia maslahi bora, wauguzi hao wanaingia katika mgogoro kutokana na Kurugenzi yao kufutwa. “Si suala la kuachwa mpaka lilete mvutano, Serikali irejeshe Kurugenzi ya Wauguzi wa Muhimbili kwa sababu wengine wanazo.
Hali halisi Muhimbili
Madaktari wa ziada 80 waliotakiwa kuanza kazi hawakuripoti na kwa mujibu wa maelezo ya Aligaesha, hawakuwa wametuma maombi ya kuongezwa madaktari kutoka wizarani. Wakati mgomo ukiendelea, baadhi ya madaktari wazalendo hospitalini hapo, wamesambaza ujumbe kwa madaktari wenzao wakiwasihi warejee kazini mara moja. Ujumbe huo uliosambazwa kwa njia ya barua pepe, ujumbe mfupi wa simu na vipeperushi, unasomeka:
“Tafadhalini sana waheshimiwa madaktari tuwaonee huruma wananchi wenzetu, wanaopoteza maisha yao kwa kitendo chetu cha kugoma. “Kama ni ujumbe wa madai yetu bila shaka tayari umefika kwa wahusika serikalini, sasa imetosha. Tuache mgomo huu usio na tija. Tuwe na moyo wa utu, uzalendo na ubinadamu kwa wananchi wenzetu.
Turejee kazini, tutumikie Taifa letu, wakati madai yetu yakitafutiwa ufumbuzi.” Aidha, ujumbe huo uliosainiwa na daktari wa hospitali hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja tu la Dk. Ndimbo, unaeleza kwa hisia za uchungu, kwamba mgomo huo umewaathiri sana wananchi wasio na hatia wakiteseka na kutaabika, huku baadhi yao wakipoteza maisha.
Daktari huyo anawasihi wenzake kupitia ujumbe huo, wavae moyo wa huruma na kuacha mgomo huo, ili kuhudumia wananchi. Vipeperushi vyenye ujumbe huo, vimesambazwa katika wodi na maeneo mbalimbali ya hospitali hiyo kuanzia jana mchana.
Mgomo wa madaktari nchini ulianza takribani wiki moja iliyopita wakishinikiza watekelezewe madai yao mbalimbali yakiwemo ya nyongeza za posho na mishahara. Hata hivyo, wakati Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipowaita madaktari hao ili kuzungumzia madai yao katika
ukumbi wa Karimjee Januari 29, mwaka huu, madaktari hao hawakufika kitu ambacho kilitafsiriwa kuwa ni kiburi kwa Serikali na wananchi.
MOI
Huduma zilizotolewa jana ni za wagonjwa wa dharura waliopata ajali ndani ya saa 24. Wengine wa kliniki na wa nje walitangaziwa mapema kuwa hawatapewa huduma, hivyo warejee nyumbani.
Wakati huo huo, CCM imewaomba madaktari kurudi kazini huku wakiendelea na mazungumzo na Serikali na kwamba madai yao yanawezekana kushughulikiwa ikiwa pande zote mbili zitakaa chini na kuzungumza. Imeitaka Serikali itafute kwa makini chanzo cha mgogoro huo na majibu, na madaktari nao wawe tayari kuzungumza.
Mgomo wa madaktari ulioanza hivi karibuni katika hospitali za umma, kwa kiasi kikubwa unatajwa na CCM kuwa na madhara makubwa kwa Watanzania masikini ambao ni wengi, kiasi cha kugharimu maisha yao. Kilipongeza pia madaktari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuitikia mwito wa kwenda kusaidia kutibu Watanzania wenzao.
CHANZO: HABARI LEO
Categories: