HATIMAYE mawaziri saba kati ya nane wakiwemo wanaokabiliwa na tuhuma za ubadhirifu, wamekubali kuandika barua za kujiuzulu wenyewe kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kukinusuru Chama cha Mapinduzi (CCM).
Habari za kuaminika kutoka mjini Dodoma zimesema kuwa mawaziri hao, walilazimishwa kujiuzulu katika kikao cha dharura kilichokuwa chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kilichofanyika mara tu baada ya kumalizika kwa kikao cha Bunge.
Taarifa zimewataja waliokubali kujiuzulu kuwa ni pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara, Cyril Chami; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Mkuchika; Waziri wa Uchukuzi Omari Nundu; na Waziri wa Afya, Dk. Haji Mponda.
Wengine wanaodaiwa kujiuzulu ni: Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja; Naibu Waziri wa Afya, Lucy Nkya; na Naibu Waziri wa Viwanda, Lazaro Nyarandu.
Hata hivyo, Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, ambaye alishambuliwa vikali kwa kuitwa kinara wa ufujaji, hakuwepo katika kikao hicho kwa madai kuwa yuko nje ya nchi, anasubiriwa aungane na wenzake kuachia ngazi.
Kujiuzulu kwa mawaziri hao kumekuja baada ya kuzuka kwa mjadala mzito ndani ya Bunge kwa siku mbili mfululizo kuhusiana na tuhuma za ufujaji wa kutisha wa fedha za umma, kiasi cha kusababisha kuwepo kwa azimio la kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Wakati wa majumuisho ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mashirika ya Umma, mwenyekiti wa kamati hiyo, Zitto Kabwe, alilitaka Bunge kuweka ushabiki na itikadi za kisiasa pembeni na kuazimia kwa pamoja kupiga kura za kutokuwa na imani na Pinda kutokana na uzembe wa mawaziri wake.
Kabla ya kujiuzulu huko Spika wa Bunge, Anne Makinda, jana alizima hoja ya kumwajibisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akidai kuwa utaratibu mzima umekiukwa na hivyo hauwezi kufanyiwa kazi katika kikao cha sasa cha Bunge.
Makinda alisema hayo alipokuwa akitoa mwongozo uliyoombwa na Mbunge wa Bumbuli, January Makamba (CCM) kuhusu suala hilo na kudai kuwa wanaoendesha mchakato huo itabidi wasubiri hadi Bunge lijalo.
Makinda ametoa hoja hiyo, wakati idadi kubwa ya wabunge wakiwa wametia saini za kumwajibisha Waziri Mkuu kutokana na ubadhirifu mkubwa unaowahusisha mawaziri watano wa serikali.
Mchakato wa utiaji saini unaosimamiwa na Zitto Kabwe, ulikuwa ukiendelea kwa kasi na habari za kuaminika zinasema kuwa idadi ya walio tayari kuweka saini zao inaweza kufika wabunge 200.
Akuzungumza jana mchana, Zitto alisema kuwa hadi muda huo alikuwa na saini za wabunge 66, huku akidai kuwa wabunge wote wa CUF walikuwa wameandikiwa barua na chama chao kusaini azimio hilo, jambo ambalo litafanya idadi ya wabunge kufikia 80.
Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya kusimamia Mashirika ya Umma (POAC) alisema kuwa hadi jana majira ya saa 7 mchana, wabunge wa vyama vyote walikuwa wameweka saini azimio hilo isipokuwa wa UDP.
Mawaziri wanaotakiwa kuwajibika ni Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo; Waziri wa Viwanda na Biashara, Cyril Chami na naibu wake, Lazaro Nyalandu; Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Mkuchika; Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja; na Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), alisema wabunge wa CUF 12 wameshasaini azimio hilo na kwamba maagizo yametoka makao makuu ya chama hicho kutaka wabunge wake kusaini kusudio hilo.
Alisema kuwa baadhi ya watu wanasema Waziri Mkuu hana makosa na kwamba anaonewa na kueleza kuwa wanampenda sana, lakini wanaiheshimu zaidi Tanzania.
Alisema kulingana na kanuni za Bunge, wabunge wanaweza kumwajibisha Waziri Mkuu kwa kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye.
“Miongoni mwa majukumu ya Waziri Mkuu ni kusimamia shughuli za serikali pamoja na utendaji wa baraza la mawaziri. Mawaziri wameonekana kusimamia wizara zao ambazo zina wizi na ubadhirifu.
“Kuwepo kwa ubadhirifu ni kushindwa kwa Waziri Mkuu kutekeleza majukumu yake…tunajua hawezi kuwawajibisha mawaziri na ndiyo moja ya mambo tunayotakiwa kuyarekebisha kwenye Katiba, lakini yeye tuko naye hapa na sisi ndiyo tuliomthibitisha na tuna uwezo wa kuondoa uthibitisho wake.
“Kwa hiyo katika hilo hatuna mbadala hatuna muafaka kama mawaziri waliotajwa kuhusika na aina ya ubadhirifu kwenye wizara zao, idara zao, mashirika hayo na halmashauri kama hawajachukua hatua tunaanzia na Waziri Mkuu. Atakuwa Waziri Mkuu wa kwanza nchini kupigiwa kura au kutolewa hoja ya kutokuwa na imani naye.
“Tumempa muda mpaka Jumatatu tutawasilisha rasmi hoja yetu kwa Spika kwa mujibu wa mamlaka ya kanuni 133 inayotutaka kukusanya saini ya wabunge asilimia 20 ya wabunge wote ambao kwa hesabu zetu ni wabunge 70 na tutapata zaidi hao,” alisema.
Alisema kwamba wanatimiza matakwa hayo ya kikanuni na kisha kuwasilisha kwa Spika, ili baadaye Bunge liweze kuonyesha meno yake.
Alibainisha kuwa ili Waziri Mkuu aweze kutoka katika kitanzi hicho, anapaswa kumshauri Rais Jakaya Kikwete awafukuze kazi mawaziri hao ama mawaziri hao wajiondoe mapema.
“Lakini kama wanataka kumuweka kiongozi wao, kiraja wao rehani, wanataka Waziri Mkuu aingie katika hoja ya kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye ni jukumu lao, wachague wao wenyewe,” alisema.
Hata hivyo, Spika kwa upande wake alisema kwa mujibu wa kanuni za Bunge ambazo zimetokana na Katiba zinataka hoja kama hiyo iwasilishwe bungeni angalau siku 14 kabla ya siku iliyokusudiwa, na sio wiki ijayo kama ilivyoelezwa juzi na Zitto Kabwe bungeni.
“Sasa hii habari ya kusema waheshimiwa njooni njooni kusaini huo sio utaratibu. Hiyo haikubaliki kwa sababu mimi sijapata hiyo hoja mpaka sasa. Bunge hili tunaahirisha Aprili 23 maanake Jumatatu. Leo (jana), kesho (leo), Jumapili, Jumatatu haikidhi siku 14 sana sana anaweza (Zitto) kukusanya nyaraka labda kuwasilisha Bunge lijalo,” alisema Spika.
Aliendelea kusema kuwa kanuni na utaratibu alioutangaza Zitto hauwezekani na kwamba zoezi la kukusanya saini za wabunge ni batili. Aliwashauri wanaotaka hoja hiyo wavute subira hadi Bunge lijalo, akidai kuwa kuitimiza ndani ya siku tatu zilizobaki ni kukosa mashiko.
Hata hivyo alikiri kuwa wabunge wana madaraka na Waziri Mkuu kulingana na Katiba kwa kuwa ndiyo wanaomwidhinisha baada ya uteuzi.
Alinukuu ibara ya 53(a) (3) kwamba Waziri Mkuu anapitishwa na wabunge ambao wanamthibitisha. “Msingi wa Zitto ni kwamba huyu ni mtu tuliyempitisha sisi wenyewe. Kwa hiyo tuna mamlaka naye kwani ndiye tulimpitisha sisi,” alisema.
“Waziri ndiye atakayekuwa mkuu wa shughuli za serikali bungeni. Serikali chini ya mamlaka ya Rais ndiyo itakayofanya maamuzi juu ya sera. Na mawaziri chini ya uongozi wa Waziri Mkuu watawajibika kwa pamoja katika utekelezaji wa shughuli za serikali. Hivi vifungu ndivyo vinatupa nguvu ya kuwa na uwezo na Waziri MKuu.”
Categories: