WABUNGE WA CCM WATISHWA


Katika hatua nyingine, imedaiwa kuwa wabunge wa Chama cha Mapinduzi, wameitwa na kutishwa kuchukuliwa hatua ikiwa watasaini azimio hilo.

Mmoja wa wabunge wa CCM aliyekiri kuitwa ni Deo Filikunjombe (Ludewa) ambaye alisema alilazimika kusaini kabla ya kuitikia wito huo.

Filikunjombe, alikiri kuitwa na Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, na kumtaka kutosaini azimio hilo, lakini akamwambia alikwishasaini na alifanya hivyo kwa niaba ya wananchi wa Ludewa ambao wamechukizwa na ubadhirifu mkubwa uliofanywa na watendaji hao wa serikali.

Kuhusu wabunge wa CCM kutosaini azimo hilo, Filikunjombe alisema kanuni haikusema wabunge wote, kwani inafahamika wengine wanarudi nyuma alisema.

Mbunge wa Mtera Livingstone Lusinde alisema suala la hoja ya kikanuni ina lengo la kuchelewesha mchakato wa kuwaondoa wanaolalamikiwa na kuahidi kuwaondoa hata kama Bunge litawakingia kifua.

Alisema kama mawaziri wanaolalamikiwa wataendelea kubakia katika nafasi zao ni bora wabunge wa CCM wakaondoka na kuwaachia wao majukumu yote.

Alipoulizwa kama msimamo wake hauwezi kuwakera viongozi wake na kuamua kumchukulia hatua ikiwa ni pamoja na kumuondoa katika chama, Lusinde alisema kuwa hilo halihofii kwa kuwa hana hati miliki ya ubunge wa Mtera na zaidi ataendelea kubakia Mtanzania anayepigania maslahi ya nchi yake.

Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM), alisema katika mapendekezo yaliyoafikiwa juzi hakuna azimio katika kamati yoyote lililotaka waziri aondolewe na kusema kuwa alichokuwa akikifanya Zitto ni usanii.

“Katika taarifa yake ile alipaswa aseme Bunge limependekeza mtu fulani awajibishwe, hivyo alitakiwa kuleta nyongeza katika taarifa yake. Hakuna aliyeleta. Ile ni burudani tu,”alisema na kuongeza kuwa hoja hiyo haina mashiko.

Alihoji kuwa iwapo Pinda alishindwa kumuondoa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, atawezaje kumuondoa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo.

Alisema kuwa ili hoja hiyo ifanikiwe ni lazima Spika aridhike kwamba ilifuata taratibu na ina sifa hata ikisainiwa na wabunge 200 kama haina sifa haiwezi kupita.

Zitto asema wembe ni uleule

Akizungumzia vikwazo hivyo, Zitto alisema haviwatishi na wanaendelea na mchakato huo, na kwamba watakabidhi hoja hiyo, Jumatatu baada ya kukamilika.

Zitto alisema kama watashindwa kusaini fomu hizo watakuwa wawakilishi wa ajabu kwa kuwa wao ndiyo waliokuwa wakipiga kelele juzi kutaka waliosababisha ubadhirifu kuwajibika na kwamba kama watashindwa kuunga mkono litakuwa ni jukumu la wananchi kupima uwakilishi wao.

Alisema ni jambo la aibu kwa Bunge zima likimaliza kikao bila kuwawajibisha mawaziri waliohujumu mali za taifa.

“Tukiondoka hapa bila kuwawajibisha watu, wananchi huko nje watalidharau Bunge kwa hiyo tunalinda heshima ya Bunge na kulinda heshima ya wabunge kwa kutaka kuona tunaimarisha uwajibikaji.

“Bila watu kuwajibika madudu haya yatarudia na ndiyo maana tunataka uwajibikaji ufanyike,” alisema.

Alisema kuwa anajua wabunge wa CCM wamechukizwa na wizi na ubadhirifu na wamesema kwa nguvu sana juzi na jana na hakuna asiyeona hilo.

“Mimi sijafanya kama mbunge wa CHADEMA, bali kama mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.

Hivyo, alitaka wabunge wasigawanywe katika misingi ya vyama na kwamba anayefanya hivyo hana maslahi na nchi na kuhoji iwapo CCM ina hoja nzuri ambayo inaisimamia.

“Tusiruhusu maneno ya propaganda ya kutugawa na ninyi ndiyo mashahidi mnalalamika na juzi mlimuuliza CAG,”alisema.

Alisema katika masuala ya kitaifa wabunge wanapaswa kuweka pembeni itikadi zao na kuwatumikia wananchi wanaowawakilisha na kusisitiza kuwa wanachokitaka ni mabadiliko na si mapinduzi.

Wasomi waunga mkono

BAADHI ya wananchi wa kada na rika mbalimbali nchini wamesema mwenendo wa Bunge la sasa ni ishara za kuamka kwa mhimili huo inayotokana na changamoto za wabunge wa upinzani.

Wakizungumza na mwandishi wetu  kwa nyakati tofauti wananchi hao walisema msimamo wa wenyeviti ambao ni wabunge kutoka upinzani wanaoongoza kamati tatu za Bunge umesaidia kuonyesha uozo wa watendaji serikalini hususan mawaziri wasiotimiza vema wajibu wao.

Wenyeviti wa kamati hizo ni Zitto Kabwe (CHADEMA) Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Agustine Mrema (TLP) Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na John Cheyo (UDP) Hesabu za Serikali (PAC).

Kwa mujibu wa Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Profesa Issa Shivji, Katiba ya sasa inaruhusu kupiga kura ya kutokua na imani japo ni mapema kufanya hivyo huku akisisitiza kwamba jambo la msingi ni kusubiri uamuzi wa wabunge hao.

Kwa upande wake mhadhiri mwandamizi mstaafu wa UDSM Dk. Azaveli Lwaitama alisema wabunge hao wanagombana na mfumo wa kumweka Waziri Mkuu madarakani hali inayoonyesha wazi kwamba hawana imani na Rais.

“Ninavyoona hapo kinachowachukiza wabunge hao ni uwaziri mkuu na mfumo wa kumpata waziri mkuu kwa sababu wanalalamikia utendaji wa baadhi ya mawaziri lakini waziri mkuu hana uwezo wa kuwafukuza mawaziri hao.

“…Hebu tukumbuke wakati wa Jairo, Waziri Mkuu alitamani kumfukuza akashindwa lakini Katibu Mkuu Kiongozi alikuwa na uwezo; ndiyo maana alimpa likizo yenye malipo.

“Tatizo ni mfumo wa utawala walioteuliwa wanawajibika kwa aliyewateua lakini waliochaguliwa wanatumwa na wananchi ndiyo,” alisema Dk. Lwaitama na kuongeza kwamba lazima mambo hayo yaingie kwenye Katiba mpya.

Mjasiriamali Celina Ezekiel wa Isimani Iringa alisema Bunge limeanza kutambua mamlaka yake ya kuisimamia serikali hasa kwa wabunge wa CCM.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Profesa Sifuni Mchome alisema wabunge wana uhuru wa kufanya hivyo kwa maslahi ya nchi na kuongeza kwamba ni jambo la kawaida.

Mkazi wa Igunga mkoani Tabora Nicholous Ngassa alisema haafikiani na suala la kumwondoa Waziri Mkuu madarakani badala yake mawaziri walioguswa na ripoti ya CAG wanapaswa kuwajibika na kupelekwa mahakamani.

“Hali ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu na serikali yake kunashusha thamani Chama cha Mapinduzi (CCM) katika jamii na kujiondoa kwenye ramani ya siasa nchini na Afrika,” alisema Ngassa.

Naye Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Dk. Benson Bana alisema wabunge wametimiza wajibu wao na kuwataka mawaziri wanaotuhumiwa kuchukua hatua.

Akitolea mfano wa ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Dk. Bana ambaye ni mwenyekiti mwenza ya Taasisi ya Utafiti wa Elimu ya Demokrasia Tanzania (Redet) alisema umaskini unaongezeka kwa sababu ya wachache walio kwenye ngazi za uamuzi.

“Ripoti ya CAG inaonyesha kushuka kwa kiwango cha uwajibikaji serikalini hususan eneo la matumizi ya fedha za walipa kodi… kwa nini wanaotajwa kwenye ripoti hiyo wasijiuzulu?” alisema Dk. Bana na kutaka wabunge washikamane katika hilo.

Naye Mahadhiri wa Chuo Kikuu cha Kiislam cha Morogoro (MUM) Profesa Juma Mikidadi alisema wabunge wako sahihi katika uamuzi wa kutaka kumjadili Waziri Mkuu kwa sababu ya mawaziri wa chini yake kushindwa kuwajibika.

Sheikh Jabir Ramadhan aliwashauri wabunge hao kutoa muda wa mwisho kwa mawaziri hao ili kabla hawajaondoka waanze kuchunguzwa huku akiwashauri wasifanye hivyo kwa chuki.

Mkazi wa Tabata Jamila Athuman alisema serikali ya awamu ya nne imeongeza pengo kati ya matajiri wachache na maskini wengi hali inayowafanya wananchi kuichukia serikali yao.

“Walioteuliwa hawana uchungu wa nchi ndio maana wanafanya ufisadi huku Rais akiwakingia kifua kwa kuendelea kuwaacha madarakani na wakati mwingine anawahamisha vituo vya kazi,” alisema Jamila.

Joseph Mhimbilila alisema wananchi wamechoka kuvumilia wizi wa mali ya umma unaofanywa na watawala wao sasa wananchi wamechoka hivyo wabunge hao wakishindwa kuwasaidia watachukua hatua kali zaidi.

“Hili linaweza kuwa fundisho kwa viongozi wenye ndoto za kuliibia taifa hili,” alisema.

Kwa Upande wake Mwanasheria Alex Mgongolwa alisema sheria inampa mamlaka Waziri Mkuu kusimamia shughuli zote za serikali na kuhakikisha kunakuwepo na uwajibikaji.

Alisema katika Katiba ibara ya 53 (A 1-6) inasema hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu inaweza kuwasilishwa bungeni kukiwa na sababu za msingi juu ya majukumu ya Waziri Mkuu na kushindwa kuyatekeleza.

“Nafuu inayoweza kupatikana ni kama anayetolewa hoja hajapitisha miezi sita tokea kuteuliwa kwake au kabla ya miezi tisa kupita tokea hoja kama hiyo kuwasilishwa bungeni, na hapa ni lazima Spika ajiridhishe kuwa masharti yamezingatiwa,” alisema Mgongolwa.

Categories: