• AJALI YA MV SKAGIT, URAIS 2015
VYAITESA
na Mwandishi wetu
UPEPO wa mabadiliko ya kisiasa
uliozikumba nchi nyingi duniani,
unaelekea kukiathiri Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ambacho sasa
kinahaha kujinusuru kung’oka
madarakani katika Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2015.
Chama tawala hivi sasa kina
msuguano mkubwa wa kiuongozi
ambapo baadhi ya viongozi wake
wamekuwa wakimshutumu Katibu
Mkuu, Willison Mukama, kwa
kukwamisha mikakati ya kujiimarisha
na kurejesha matumiani yaliyofifia
miongoni mwa wanachama wake.
Licha ya Katibu wa Itikadi na Uenezi,
Nape Nnauye, wiki hii kukanusha
kutokuwa na msuguano na Mukama,
makada wa chama hicho
wamelidokeza Tanzania Daima
Jumapili, kuwa vita ya makundi ya
kuwania uongozi na ile ya ufisadi
inakitesa chama hicho.
Mnyukano wa kisiasa unaonekana
wazi hivi sasa ni baina ya Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe, dhidi ya
kundi linalomuunga mkono aliyekuwa
Waziri Mkuu, Edward Lowassa,
anayetajwa kutaka kuwania urais
katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2015.
Wakati hali ya mambo ikionekana
kutokuwa nzuri ndani ya chama hicho,
nguvu kubwa sasa imehamishiwa
kwenye Bunge kwa lengo la
kuwadhibiti wabunge wa CHADEMA
ambao wanaelezwa kutishia uhai wa
chama hicho.
Makada wa CCM wamedokeza kuwa
wamebaini wabunge wa CHADEMA
mwaka 2005-2010 walilitumia vizuri
Bunge kujenga hoja za msingi ambazo
ziliwasaidia kujijenga na hatimaye
kupata wabunge 22 wa majimbo
kutoka watano.
Waliongeza kuwa kutokana na kubaini
jambo hilo, chama hicho kimeamuap
‘kuzishughulikia’ hoja zinazotolewa na
CHADEMA bila kujali kama zina
masilahi kwa taifa au la.
Inadaiwa kuwa viongozi wa Bunge
nao wamepewa maelekezo ya
kukisaidia chama chao hasa
wanapoona kuna hoja zinazoelekea
kuwapatia umaarufu wabunge wa
CHADEMA.
Tanzania Daima Jumapili,
limedokezwa kuwa pamoja na
maelekezo hayo baadhi ya viongozi
wa Bunge wameonekana kushindwa
kukisaidia chama tawala kwa sababu
ya kutozijua ipasavyo kanuni, hivyo
kutumia ubavu kukataa jambo
linalotolewa na wapinzani, hivyo
kuwaongezea umaarufu.
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai,
anatuhumiwa kutoa fursa zaidi kwa
wabunge wa CCM kurudia maneno ya
dharau na lugha ya kuudhi dhidi ya
wapinzani.
Kiongozi huyo pia juzi alionesha
‘ukada’ wake pale alipojifanya kukosea
jina la Mbunge wa Viti Maalumu, Rose
Kamili, kwa kumuita Rose Kamili Slaa,
ilhali akijua mbunge huyo
alishatarikiana na Dk. Slaa.
Hata hivyo CCM hivi sasa pia
kinakabiliana na wakati mgumu wa
kushutumiwa kushindwa
kuwachukulia hatua watendaji wake
wanaobainika kufanya uzembe katika
shughuli zao za kila siku.
Ajali ya mv Spice Islanders iliyotokea
mwaka jana na mv Skagit iliyotokea
wiki iliyopita inadaiwa ilichangiwa na
uzembe wa wataalamu kwa
kushindwa kukagua ubora wake.
Serikali ya CCM pia inalaumiwa kwa
kushindwa kuwa na vifaa vya kisasa
vya uokoaji licha ya kila mara
kukumbwa na matukio ya ajali za
baharini na ziwani.
Katika ajali hizo mbili za majini
zilizopoteza maisha ya Watanzania
zaidi ya 400, serikali ya CCM
inalaumiwa kwa kushindwa
kusimamia sheria za usafiri wa majini
na kuficha taarifa ya uchunguzi wa
ajali ya awali.
Mmoja wa wabunge wa CCM ambaye
jina lake limehifadhiwa, aliilaumu
serikali kwa kuunda tume kuchunguza
ajali ya mv Bukoba na Spice Islanders,
lakini haikutoa matokeo ya uchunguzi
huo.
“Serikali iliunda tume kuchunguza ajali
ya awali ya mv Spice Islanders na mv
Bukoba lakini ikaficha matokeo ya
uchunguzi wake. Leo imetokea ajali
nyingine na binafsi naamini kama
matokeo ya uchunguzi wa awali
yangetolewa, bila shaka ajali ya juzi
ingeepukika,” alisema kada huyo.
Kufichwa kwa matokeo ya uchunguzi
wa ajali za awali za majini,
kumeelezwa kuwa ndiyo sababu ya
Spika wa Bunge, Anne Makinda,
kuzima hoja za wabunge wa kambi ya
upinzani walioungana na wabunge
wote wa Zanzibar kutaka kujadili ajali
ya mv Skagit iliyosababisha vifo vya
zaidi ya watu 150.
Chanzo: FreeMedia
Categories:
None