• WAPINZANI WANG’ANG’ANIA
ISIPITISHWE
na Salehe Mohamed, Dodoma
UTORO wa wabunge uliokemewa na
Spika wa Bunge, Anne Makinda, wiki
iliyopita jana ulikwamisha kupitishwa
kwa bajeti ya Wizara ya Kilimo,
Chakula na Ushirika.
Wiki iliyopita Makinda alisema utoro
kwa wabunge hivi sasa umekithiri na
akaonya kuwa kama wataendelea na
tabia hiyo ipo siku watakwamisha
upitishaji wa bajeti ya wizara husika.
Utabiri huo wa Spika Makinda, jana
ulitimia baada ya wabunge hasa wa
kambi ya upinzani kuibua hoja ya
kukwamisha upitishwaji wa bajeti ya
Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika
kwa mwaka 2012/2013 kutokana na
uchache wa wabunge.
Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia
(NCCR-Mageuzi), ndiye aliyekuwa wa
kwanza kutoa hoja kwa kutumia
kanuni ya 112 ambapo alitaka bajeti
hiyo isipitishwe kwa kuwa wabunge
waliopo hawajafikia nusu ya wabunge
wote.
“Mheshimiwa Naibu Spika, kanuni
inataka Bajeti ipitishwe ikiwa idadi ya
wabunge waliohudhuria itafikia nusu
ya wabunge wote.
“Hapa tulipo mimi nimeshahesabu
mara mbili wabunge wote hatuzidi
110, na tunajua idadi ya wabunge
wote ni 352 na nusu yake ni wabunge
175, ili tutende haki nakuomba
uhesabu idadi ya wabunge waliopo
kabla ya kupitisha bajeti hii ili
tuwatendee haki Watanzania,”
alisema.
Baada ya hapo alisimama Mbunge wa
Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-
Mageuzi) akitumia kanuni ya 77 (1) na
(2) kuwa wabunge waliopo hawafikii
nusu ya wabunge wote.
“Mheshimiwa Naibu Spika, kanuni ya
77 (1). Akidi kwa kila kikao cha Bunge
wakati wa kufanya maamuzi itakuwa ni
nusu ya wabunge wote, kama
ilivyofafanuliwa katika ibara ya 94 ya
Katiba, isipokuwa kwamba idadi hiyo
haitahusu hoja kuhusu uamuzi wa
kubadilisha masharti yoyote ya Katiba
kwa mujibu wa Ibara ya 98 ya Katiba.
“Mbunge yeyote aliyehudhuria
anaweza kumjulisha Spika kwamba,
wabunge waliopo ni pungufu ya akidi
inayohitajika kwa ajili ya shughuli
inayoendelea.
“Kwa maana hiyo, Mheshimiwa Naibu
Spika, nasisitiza kuwa hatufiki nusu
humu ndani,” alisema.
Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses
Machali (NCCR-Mageuzi) naye
alisisitiza kanuni hiyo hiyo kipengele
cha tatu. “Endapo Spika ataridhika
kwamba kweli idadi ya wabunge walio
ndani ya Ukumbi wa Bunge ni
pungufu ya akidi inayohitajika basi
atasimamisha shughuli za Bunge kwa
muda atakaoutaja na atamwagiza
katibu kupiga kengele.”
Naibu Spika Job Ndugai, alisema idadi
hiyo inatakiwa wakati wa kupiga kura
ya mwisho ya kuipitisha bajeti hiyo si
wakati wa hatua za awali za kamati ya
matumizi.
Kauli hiyo ilimfanya Mnadhimu wa
Kambi Rasmi ya Upinzani, Tundu
Lissu, asimame na kutaka kiti cha
Spika kisiliburuze Bunge kwa kukiuka
kanuni na kuliomba Bunge liahirishe
shughuli hiyo.
Hata hivyo Ndugai hakukubaliana na
kauli ya Lissu. Ndugai huku akisema
kuahirisha shughuli za Bunge ni
gharama kubwa, alichukua muda
kuamua jambo hilo.
Ndugai aliamuru Kamati ya matumizi
iendelee huku Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge),
William Lukuvi, alitoka nje
kuwahamasisha wabunge warejee
ukumbini. Mbali na juhudi za Waziri
Lukuvi pia kengele ilikuwa ikipigwa nje
ya ukumbi wa Bunge kuwahamasisha
warejee ukumbini.
Juhudi zakwama
Pamoja na jitihada za viongozi
mbalimbali wa serikali na Bunge
kuhakikisha idadi ya wabunge inafika
nusu, jambo hilo lilishindikana na
ndipo Ndugai alipoamua kuahirisha
shughuli za Bunge.
“Ni Vizuri wananchi waelewe kuwa
tuna huu msiba wa kitaifa
unaoendelea Zanzibar kuna wabunge
wenzetu wako kule Zanzibar hasa
kutoka Zanzibar kwa ruhusa ya
Spika…, kuna mawaziri na manaibu
wapo kule na wengine wako kule kwa
shughuli maalumu.
“Kuna wabunge kadhaa ambao mimi
mwenyewe nimewaruhusu wapo
kwenye msiba wa mazishi ya mama
wa mbunge mwenzetu, Mike Lekule
Laizer (CCM).”
Wakati Ndugai akiendelea kutoa
ufafanuzi huo, wabunge wa upinzani
walikuwa wakitoa kauli na kugonga
meza kuonesha kupinga utetezi huo.
Vitendo hivyo vilimfanya Ndugai
kuwataka wamsikilize badala ya kupiga
kelele ambazo haziwasaidii, kwakuwa
kiti cha Spika hakiwezi kumkandamiza
mtu.
“Nawaombeni ndugu zangu
tunaposikilizana kama watu wazima…
tupeane nafasi, mnalolitaka litakuwa
…..mkisema nyinyi nawapa
nafasi….mimi nikisema mnaanza
kupiga kelele.
“Inanisikitisha sana tunapovunjiana
heshima, tunakuwa kama watoto
wadogo, mimi sidhani kama
inatujengea heshima mahali popote
katika nchi yetu, tunafanya jambo la
msingi la taifa,” alisema.
Alisema kwa busara alizonazo
ameamua kuahirisha kikao hicho,
hatua ya kamati ya Bunge zima hadi
Jumatatu (kesho).
Baada ya kauli hiyo wabunge wengi
hasa wa upinzani walikuwa wakipiga
meza kwa kushangilia ‘ushindi’
walioupata.
NCCR-Mageuzi wakomalia
Mara baada ya Bunge kumalizika
wabunge wa NCCR-Mageuzi
walikutana na waandishi wa habari na
kuweka bayana kuwa hivi sasa
wanafanya uchunguzi kujua ni vikao
gani vilifanyika bila idadi ya wabunge
kutimia, baada ya hapo wapeleke hoja
kutaka maamuzi yaliyofikiwa
yatenguliwe.
Mbunge wa Kasulu Kusini, David
Kafulila, alisema maamuzi mengi
yamekuwa yakifanywa bila akidi
kutimia, jambo ambalo ni hatari kwa
maendeleo ya taifa.
“Tutaomba Spika atupe orodha ya
wabunge waliohudhuria katika kikao
hiki cha Bajeti na tukibaini tutaomba
maamuzi yaliyoafikiwa yatenguliwe,”
alisema.
Chanzo FreeMedia
Categories:
None