Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete amesema kuwa
hali ya mashariki mwa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC)
inatia wasiwasi na hivyo Tanzania
inafuatilia kwa makini hali
inavyoendelea katika eneo hilo la
nchi hiyo jirani.
Aidha, Rais Kikwete amesema
kuwa Tanzania ingependa kuona
hali ya amani inarejea katika DRC
kwa sababu nchi hiyo inahitaji
kupata muda wa amani ili
waelekeze nguvu zake kwenye
maendeleo badala ya kupigana.
Rais Kikwete amesema hayo jana,
Jumanne, Juni 3, 2012, wakati
alipokutana na kufanya
mazungumzo na Profesa Ntumra
Luaba Alphonce, Katibu Mtendaji
wa Umoja wa Nchi za Maziwa
Makuu wa International
Conference on Great Lakes Region
(ICGLR) kwenye Hoteli ya Roca
Golf mjini Bujumbura, Burundi.
Rais Kikwete akifuatana na Mama
Salma Kikwete alikuwa mjini
Bujumbura kushiriki katika
Sherehe za Miaka 50 ya Uhuru wa
Burundi na kurejea nyumbani jana,
3 Juni, 2012. Kabla ya kuja hapa,
Rais Kikwete alikuwa mjini Kigali,
Rwanda, kushiriki katika sherehe
za namna hiyo zilizofanyika Julai
Mosi, mwaka huu. Rwanda na
Burundi zilipata uhuru kutoka kwa
Wabelgiji Julai Mosi na Julai 2,
mwaka 1962.
Rais Kikwete amemwambia Katibu
Mtendaji huyo: “ Kwa hakika hali
mashariki mwa Congo inatutia
wasiwasi mkubwa na Tanzania
inafuatilia kwa makini hali hiyo.
Congo imekuwa katika vita muda
mrefu kupita kiasi kwa sababu
tokea mwaka 1997 imekuwa katika
vita mfululizo.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Wakati
umefika kwa Congo kutulia ili
nguvu inayoingia katika
mapambano na vita ielekezwe
katika maendeleo ya wananchi wa
nchi hiyo.”
Rais Kikwete pia ameunga mkono
wazo la kuitishwa kwa mkutano
wa mawaziri wa nchi wanachama
wa ICGLR ili kujadili hali ilivyo
katika mashariki mwa Congo
kufuatia ombi la DRC kutaka
kuitishwa kwa mkutano huo.
Hali katika mashariki mwa Congo
imeanza kutia wasiwasi baada ya
kikundi cha waasi wa Serikali ya
nchi hiyo wakiongozwa na jambazi
la kivita John Bosco Ntaganda
kuanza tena harakati zake za
kivita dhidi ya Serikali ya Rais
Joseph Kabila.
Usiku wa jana, Jumanne, Julai 3,
2012, alikutana na kufanya
mazungumzo na Rais wa
DRC,Mheshimiwa Kabila kuhusu
hali ilivyo mashariki mwa DRC.
Wakati akiwa Kigali,
Rwanda,mwishoni mwa wiki, Rais
Kikwete pia alikutana na kufanya
mazungumzo na Rais Paul Kagame
kuhusu hali ilivyo mashariki mwa
DRC.
Aidha, usiku huo huo wa kuamkia
jana, Rais Kikwete alikutana na
kufanya mazungumzo na Naibu
Waziri Mkuu wa Ubelgiji,
Mheshimiwa Didier Reynders
ambaye pia anahusika na masuala
ya nchi za nje, biashara ya nje na
masuala ya Umoja wa Ulaya (EU).
Katika mazungumzo Rais Kikwete
na Mheshimiwa Reynders
walizungumzia hali ya mashariki
mwa Congo pamoja na mchakato
wa ushirikiano ndani ya Jumuia ya
Afrika Mashariki (EAC).
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya
Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
4 Julai, 2012