*Yazifadhili asasi kuvuruga amani Loliondo
*Yazichotea mamilioni kufanikisha vurugu
Shirika
la Misaada la Kimataifa la Oxfam limejiingiza kwenye ufadhili wa
vikundi na asasi za kiraia, zinazozua na kuchochea mgogoro kati ya
Serikali na wafugaji wa jamii ya Kimaasai katika Wilaya ya Ngorongoro
mkoani Arusha.
Kujiingiza kwa Oxfam ni juhudi za asasi za Tanzania zilizo na baadhi ya
raia wa kigeni, kuhakikisha kuwa Loliondo haitawaliki. Pia ni mwendelezo
baada ya kukwama kwa baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Ulaya ambao mwaka
jana walijiingiza huko kinyemela hata bila kuitaarifu Serikali ya Mkoa
wa Arusha.
Habari
za uhakika zilizopatikana kutoka Arusha zimesema kwamba shirika hilo
limetoa mamilioni ya shilingi zilizowezesha baadhi ya asasi hizo
kukutana mjini Arusha wiki iliyopita. Fedha hizo, pamoja na kuwawezesha
viongozi na wanachama wa asasi hizo, zinatumika pia kulipia matangazo na
propaganda katika vyombo vya habari.
Asasi
zilizo katika mkakati huo ni mtandao wa wanaharakati wa haki za
binadamu (FEMA CT), mtandao wa mashirika yanayotetea haki za wafugaji,
wawindaji na wachuma matunda nchini (PINGO’s Forum), mtandao wa utetezi
wa masuala ya ardhi (TALA), na shirika lisilo la kiserikali lililopo
Ngorongoro (NGONET).
Asasi
hizo kwa mara ya kwanza kwenye tamko lake, kwa vyombo vya habari
mwishoni mwa wiki, zimetamka wazi kuunga mkono harakati za kuichafua
Tanzania zinazoendeshwa kwenye mtandao.
“Kutokana
na hayo, sisi mashirika yanayojishughulisha na utetezi wa haki za
binadamu nchini Tanzania, tunaunga mkono kampeni za mtandao wa kimataifa
wa Avaaz,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Kufanyika
kwa mkutano wa pamoja wa asasi hizo kumekuja baada ya hivi karibuni
Rais wa Oxfam Ireland, Monica Gorman, na viongozi wengine wa shirika
hilo kuzuru Ngorongoro bila kuwataarifu viongozi wa Serikali ngazi ya
mkoa.
Akiwa
Loliondo, Gorman alijaribu kuibua tatizo “lisilokuwapo” na kutaka
wananchi wanaoishi hapo wasibughudhiwe. Kimsingi anapinga kusudio la
Serikali ya kuandaa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi katika vijiji vya
Loliondo. Mpango huo umelenga kuainisha maeneo ya malisho ya mifugo,
maeneo ya uhifadhi wanyamapori, maeneo ya kilimo, na shughuli nyingine
za kijamii.
Akiwa
katika Kijiji cha Arash kilicho karibu na Loliondo, aliwataka
wanavijiji wawe makini katika kuingia mikataba na kampuni kwa maelezo
kwamba watapoteza ardhi yao.
Wengine
waliokuwa kwenye msafara huo ni Mkurugenzi Mkuu wa Oxfam, Jim Clarken;
Mwenyekiti wa Kamati ya Uhusiano wa Mambo ya Nje wa Bunge la Ireland,
Jim Wells, na Pat Breen, ambaye ni Mbunge.
Mwenyejiti
wa Arash, Kiaro Orminis, aliueleza ujumbe huo kwamba kuna matatizo ya
ardhi katika eneo hilo, hasa unaohusisha Kijiji cha Malambo na kampuni
ya uwindaji wa kitalii ya Ortello Business Corporation (OBC).
Kwa
muda sasa, mgogoro katika eneo la Loliondo ulikuwa umetulia hasa baada
ya wananchi kuelimishwa juu ya umuhimu wa kupanga matumizi bora ya
ardhi.
Utulivu
huo umekuwa ukiathiri mapato ya asasi zinazojitanabaisha kuwa
zinawatetea wafugaji, ilhali zikiwa hazifanyi juhudi za kutosha katika
kuwasaidia wananchi hao.
Kampeni
ya hivi karibuni ilipamba moto kwenye mtandao wa Avaaz, ikidai kwamba
Serikali ilikuwa mbioni kuwahamisha wafugaji wa Kimaasai kutoka
Serengeti. Taarifa hiyo ilipingwa vikali na Serikali kupitia Wizara ya
Maliasili na Utalii.
Taarifa ya Serikali ya Agosti 15
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Khamis Sued Kagasheki, amekanusha
uvumi unaosambazwa na shirika moja kupitia mtandao wake wa AVAAZ.org
kuwa Watanzania wa jamii ya Kimaasai wapatao 48,000 watahamishwa kutoka
eneo lao (la Serengeti), kupisha wafalme kutoka Mashariki ya Kati ili
walitumie eneo hilo kwa uwindaji wa simba na chui.
Taarifa
hiyo iliyosambazwa na mtandao huo imewataka watu kutoka duniani kote
kujiorodhesha ili wafikie angalau 150,000, ili kumshinikiza Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuacha kusaini mkataba utakaofanya
uhamisho huo utekelezwe.
Waziri Kagasheki amesisitiza kuwa uvumi huo si wakweli na hauna msingi wowote kutokana na sababu zifuatazo:
Kwanza,
hatua kama hii haiwezi kuchukuliwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
katika Hifadhi ya Serengeti maana hakuna watu wanoishi ndani ya hifadhi
hiyo. Pia kitendo hicho hakijapangwa kufanyika katika Wilaya ya
Serengeti iliyoko mkoani Mara.
Pili,
hata kama taarifa hiyo ilimaanisha Wilaya ya Serengeti mkoani Mara bado
si yakweli maana wilaya hiyo haina idadi ya Wamaasai wanaofikia jumla
ya 48,000.
Tatu,
ndani ya ya Hifadhi ya Serengeti hakuna eneo lolote lililotengwa kwa
ajili ya wafalme wa Mashariki ya Kati, ili waweze kulitumia kwa uwindaji
wa simba na chui.
Nne,
habari hizo si za kweli maana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
hahusiki kabisa na ugawaji wa vitalu vya uwindaji popote pale nchini.
Hii ni kazi ya Wizara ya Maliasili na Utalii, na Wizara haijafanya hivyo
katika eneo tajwa.
Pamoja
na ufafanuzi huo, Waziri Kagasheki amewaasa watu waliojiorodhesha na
wanaotarajia kujiorodhesha, kuwa wamepotoshwa, hivyo wanatakiwa
wasisaini kubariki kitu ambacho hawakijui wala hakipo.
CHANZO - JAMHURI
Categories: