YANGA NA SIMBA WAKABIDHIWA VIFAA NA KILIMANJARO

Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu (kushoto) na Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ (kulia), wakionesha baadhi ya vifaa vya michezo  walivyokabidhiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), ambao ndio wadhamini wakuu wa klabu hizo. Wa pili kushoto ni Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe na Mkurugenzi wa Mashindano, Saad Kawemba. Hafla hiyo ilifanyika katika ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), jijini Dar es Salaam
 
Na Clezencia Tryphone
KLABU kongwe nchini za Simba na Yanga, zimekabidhiwa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya sh milioni 34 kila moja kutoka kwa mdhamini wao mkuu, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager.
Akikabidhi vifaa hivyo katika Ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), jijini Dar es Salaam, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe, alisema, kukabidhi vifaa hivyo ni moja ya sehemu katika mkataba baina yao na klabu hizo.
Kavishe alisema lengo kubwa la kudhamini timu hizo ni kutokana na historia kubwa ya klabu hizo, pamoja na kuleta ushindani wenye burudani kwa Watanzania, ambao ni wadau wakubwa wa kunywa kinywaji hicho.
“Sisi tunafanya kazi vema na klabu hizi, tunajisikia faraja kubwa kutokana na timu hizi kuwa na historia kubwa hapa nchini na ushindani mkubwa katika soka na huu ni udhamini wa nusu msimu peke yake,” alisema Kavishe.
Alivitaja vifaa hivyo walivyotolewa kuwa ni jezi, bukta, soksi, viatu, bips, nguo za kusafiria, vikinga ugoko na mifuko.
Katika hatua nyingine, Kavishe alisema, kuhusu mabasi ya timu hizo, wako katika hatua za mwisho kuyakabidhi kwa wahusika, kwani tayari yamewasili hapa nchini, ambapo kuna mambo kadhaa wanayakamilisha.
Akizungumza kwa niaba ya klabu ya Simba, Makamu Mwenyekiti, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, aliwashukuru wadhamini hao kwa moyo walionao, huku akiwaahidi kuhakikisha wanafanya vema na kushinda ili kuonesha umuhimu wa vifaa ambavyo wamewapa.
“Nawashukuru TBL kwa kutudhamini na kuona umuhimu kwa sisi Simba bila ya kupepesa macho na ndiyo maana hata sisi tutapigana kufa na kupona ili kuhakikisha tunavitendea haki vifaa hivi,” alisema Kaburu.
Kwa upande wa Yanga, Ofisa Habari wake, Louis Sendeu, naye aliishukuru TBL, huku akiwaomba kutoishia kwa Simba na Yanga, bali waziangalie na timu nyingine.
“Tunawashukuru sana ila msiishie kwa Yanga na Simba tu, mziangalie na klabu nyingine ambazo zinasuasua,” alisema Sendeu.
CHANZO : Francis Dande

Categories: