Showing posts with label Tanesco. Show all posts
Showing posts with label Tanesco. Show all posts

SERIKALI ISITISHE OMBI LA TANESCO




















Habari Na Rachel Balama

SERIKALI imetakiwa kusitisha ombi la dharura la kupandisha bei ya umeme kwa kiwango kikubwa ili kuepusha athari katika usalama na
uchumi kutokana na mfumuko wa bei na kupanda kwa gharama za maisha.

Pia serikali imetakiwa kuchukua hatua za haraka kulinusuru Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) dhidi ya mzigo mkubwa wa gharama unaotokana na ufisadi wa muda mrefu katika mikataba ya gesi asilia na gharama za mitambo ya kufua umeme wa dharura badala ya kuweka mkazo katika kuongeza bei ya umeme kwa wananchi wa kawaida.

Taarifa hiyo iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es salaam jana na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo kupitia CHADEMA, Bw. John Mnyika.

Alisema kuwa izingatiwe kuwa Novemba 9, mwaka huu Mamlamka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ilipokea ombi la dharura toka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) la kuidhinisha ongezeko la bei za huduma ya umeme kwa wastani wa asilimia 155 ya bei ya sasa (zaidi ya mara tatu).

Bw. Mnyika amewaomba wananchi kushiriki kwa wingi katika mkutano wa kukusanya maoni ya wadau ulioitishwa na EWURA ifikapo Desemba 2, mwaka huu.

Aliutaka Umma wa watanzania ufahamu kwamba ongezeko hilo sio ombi la TANESCO pekee bali ni agizo kutoka kwa serikali kwa kurejea maelezo ya Waziri wa Nishati na Madini Bw. William Ngeleja katika kikao cha bunge kilichopita.

Alisema hii ni mara ya pili katika kipindi cha takribani mwaka mmoja kwa TANESCO kupandisha bei ya umeme ambapo kwa mara ya kwanza ilikuwa ni mwezi Januari mwaka huu ambapo umeme ulipanda kwa asilimia 18.5 na kuchangia katika kupanda kwa gharama za uzalishaji katika nchi na kuongeza ugumu wa maisha kwa wananchi.

Alisema ombi la TANESCO la wakati huo la kupandisha umeme lilikuwa ni asilimia 34 likakataliwa na EWURA na kushushwa mpaka asilimia 18.5, sasa Rais Kikwete, Waziri Mkuu Pinda na Waziri Ngeleja wanapaswa kuwaeleza watanzania sababu za kufanya ombi hilo la dharura kuwa la wastani wa asilimia 155 ili wananchi waweze kutoa maoni kwa kuzingatia mzigo ambao umma unataka kubebeshwa.

Pamoja na matatizo ya kifedha ya TANESCO ambayo serikali inapaswa kuyashughulikia kwa pamoja na mambo mengine kutoa ruzuku katika kipindi hiki cha mpito.

Alisema gharama kubwa za uzalishaji zinazolikabili shirika zinachangiwa na ufisadi wa muda mrefu katika mikataba ikiwemo ya uzalishaji wa gesi na ukodishaji wa mitambo ya kufua na pia maamuzi ya kukopa kibiashara katika kutekeleza mpango wa dharura wa umeme.

Aliongeza kuwa Kabla ya kuongeza bei ya umeme kwa watanzania wa kawaida, Serikali ieleze imewapunguzia mzigo kiasi gani wananchi kwa kupitia upya mikataba ya kifisadi inayolinyonya Shirika la Umeme Tanzania.

Alisema uamuzi wa kupandishwa kwa kiwango kikubwa bei ya umeme utasababisha ongezeko la ziada la mfumuko wa bei hali ambayo ni tishio wa usalama na uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kwa ujumla.

Alisema serikali izingatie kwamba mfumuko wa bei nchini hivi sasa umefikia asilimia 17.9 na bidhaa zinazochangia mfumuko huo kwa kiwango kikubwa ni vyakula, mafuta na umeme.


Alisema kauli iliyotolewa na rais katika hotuba yake kwamba mfumuko wa bei na kuporomoka kwa thamani ya shilingi nchini dhidi ya dola kumetokana na uchumi wa nchi mbalimbali duniani hususani za Ukanda wa Sarafu ya Ulaya kuwa katika kipindi kigumu na cha mashaka na kueleza kwamba suluhisho la tatizo la uchumi wetu litategemea uchumi wao.

Alisema kauli hiyo imedhihirisha kwamba Serikali haina mpango wa haraka wa kukabiliana na mfumuko wa bei, kuporomoka kwa shilingi na kupanda kwa gharama za maisha.

Alisema mpango wa kupandisha bei ya umeme kwa wastani wa asilimia 155 unapaswa kusitishwa au kubadilishwa kwa kulinda maslahi ya makundi mbalimbali kwa kuzingatia aina za matumizi.
[ Read More ]

Posted by newstz.blogspot.com 0 comments»

Dar na Zanzibar visiwani kukosa umeme kwa siku kadhaa kufuatia kulipuka kwa transifoma ubungo jioni ya jana


Moja ya Transifoma iliyopo katika Kituo cha Umeme cha Ubungo jijini Dar es Salaam (Ubungo Grid Sub Station) imeungua moto jioni hii. Akizungumza na waandishi wa
 habari katika eneo la tukio, Naibu Mkurugenzi wa Tanesco, Bi. Sophia Mgonja
 amesema kuwa, kutokana na hitilafu hiyo Jiji la Dar es Salaam na Visiwa vya
 Zanzibar vitakosa umeme kwa siku kadhaa. Akifafanua zaidi juu ya tukio hilo, 
Mgonja alisema lilitokea baada ya kifaa cha kurekebisha nguvu ya umeme 
kiitwacho Reactor kuungua. Picha hizi zinawanyonyesha wafanyakazi wa kikosi 
cha zima moto wakizima moto katika Transifoma iliyokuwa ikiungua.
Picha kwa hisani ya Kulwa Mwaibale/Global Publishers .

[ Read More ]

Posted by newstz.blogspot.com 0 comments»

RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE ATEUA BODI MPYA YA WAKURUGENZI YA SHIRIKA LA UMEME TANZANIA

Napenda kuwajulisha wananchi na wadau wote kuwa kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo chini ya Sheria ya Mashirika ya Umma Sura 257 kama ilivyorekebishwa mwaka 2002 (The Public Corporations Act, Cap. 257 of R.E. 2002) Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Jenerali Mstaafu Robert P. Mboma kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuanzia tarehe 27 Oktoba 2011 baada ya Bodi iliyokuwepo kumaliza muda wake tarehe 26 Oktoba 2011.



Pamoja na uteuzi huo, Mheshimiwa William M. Ngeleja Waziri wa Nishati na Madini kwa Mamlaka aliyonayo amewateua wakurugenzi wanane wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania kuanzia tarehe 27 Oktoba, 2011.  Walioteuliwa kuwa Wakurugenzi wa Bodi ni pamoja na:-

1.    Bw. Baruany Elijah A. T. Luhanga
2.    Bw. Ridhiwan Ali Masudi
3.    Bw. Leonard R. Masanja
4.    Bw. Vintan W. Mbiro
5.    Bw. Beatus P. Segeja
6.    Bw. Hassan Ally Mbaruk
7.    Mhe. Victor K. Mwambalaswa (Mb.)
8.    Bw. Abdul Ibrahim Kitula

                                                                     Imetolewa na:
WIZARA YA NISHATI NA MADINI

[ Read More ]

Posted by newstz.blogspot.com 0 comments»

JK aonja shubiri ya umeme


Rais Jakaya Kikwete akimkabidhi Mkurugenzi wa Masoko wa Benki ya CRDB Tully Mwambapa picha ya Mwalimu Julius Nyerere iliyonunuliwa na Benki hiyo kwa kiasi cha Sh.milioni 35,wakati wa chakula cha jioni kilichoandaliwa na Ofisi ya Rais kwa ajili ya kukusanya pesa za upanuzi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam juzi na kupatikana Sh.722 milion.Fidelis Felix







Na Aziza Masoud

RAIS Jakaya Kikwete juzi usiku alionja adha ya kukatika kwa umeme alipokuwa akiendesha hafla ya kuchangia ujenzi wa kituo cha wanafunzi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwenye ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.  Tukio hilo lilitokea majira ya saa 5:43 usiku takriban saa nne tangu hafla hiyo ianze.
Rais Kikwete alifika ukumbini hapo saa 2:33 muda mfupi akitanguliwa na viongozi wengine wa Serikali.  Baadhi ya viongozi hao ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk Shukuru Kawambwa, Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki.  Kukatika huko kwa umeme, kuliwafanya wageni waliokuwapo ukumbini kuanza kupiga kelele za: “Ngeleja... Dowans... Ngeleja... Dowans... Ngeleja... Dowans.”

Tukio hilo lilidumu kwa dakika mbili kabla uongozi wa Mlimani City kuwasha genereta. Katika hafla hiyo, Rais Kikwete alichangisha Sh720 milioni kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho kinachotarajiwa kujengwa katika Kampasi ya Mlimani katika kumbukizi ya Miaka 50 ya Uhuru.  Kituo hicho kitakuwa na maeneo ya kupumzika wanafunzi, hosteli, sehemu za michezo, maktaba, huduma za vyakula, benki, ofisi za serikali ya wanafunzi na kituo cha intaneti.

Akizungumza kabla ya uchangishaji huo, Rais  Kikwete alisema lengo la kuchangisha fedha hizo za kujenga kituo cha wanafunzi ni kuboresha mahitaji ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambayo kwa sasa  yamekuwa changamoto kubwa inayosababisha wanafunzi kupata elimu katika mazingira magumu.

 “Mara  nyingi ukipita katika maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, unakuta wanafunzi wamezagaa katika maeneo mbalimbali na wengine chini ya miti. Hii yote inatokana na kukosa eneo maalumu la kujisomea na kupumzika mara wanapomaliza au kusubiri kuingia katika vipindi,” alisema Kikwete.

  Alisema kutokana na ongezeko la watu na shughuli za kimaendeleo, chuo hicho kwa sasa kinakadiriwa kuchukua wanafunzi 20,000 kwa mwaka, tofauti na miaka ya nyuma   kilipokuwa kinachukua wanafunzi 14,000.  Alisema kutokana na hali hiyo, wahitimu wanapaswa kuchangia maendeleo ya chuo hicho kwa kuwapatia wanafunzi nafasi za malazi ambazo kwa sasa hazitoshi na kuwalazimu wengine kulala nje ya eneo la chuo.

Awali, Dk Kawambwa alisema kukutana kwa wanafunzi na wahitimu wa chuo hicho ni kuendeleza utamaduni unaotumika duniani kote wa kuchangia maendeleo ya shule au vyuo wanavyotoka.  “Jambo tunalolifanya jioni hii lina maana kubwa, tunajenga utamaduni wenye manufaa katika nchi yetu kuendeleza elimu nchini kwa kuchangia maendeleo ya shule au chuo,” alisema.

Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala alisema kituo hicho kitagharamu Sh17bilioni na hatua ya kwanza ya kupata fedha za ujenzi huo ni kuandaa kampeni hizo za uhamasishaji na uchangiaji kutoka kwa wadau mbalimbali.  “Hafla ya uzinduzi wa michango hiyo ilifanyika Januari 27 mwaka jana.

Iliwahusisha wanajumuiya ya chuo na wajumbe wa baraza la chuo na tulibahatika kupata Sh1.2bilioni, nyingi zikiwa ni ahadi za wafanyakazi,” alisema Profesa Mukandala.  Alisema baada ya hafla hiyo, kulifanyika hafla nyingine Ikulu mwezi huohuo iliyokuwa ikiongozwa na Rais Jakaya Kikwete. Katika hafla hiyo jumla ya Sh1.5bilioni zilikusanywa.

Alisema hafla ya tatu ilikusanya Sh658 milioni za ambazo zilitolewa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye naye ni muhitimu wa chuo hicho. Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba aliwataka wahitimu waliosoma chuoni hapo kuwa mstari wa mbele kuchangia maendeleo yake.

Katika hafla hiyo Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) iliahidi kutoa Sh150 milioni, Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro Sh130 milioni, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Sh100 milioni, Mikumi Interprises Sh20 milioni, Benki ya NMB Sh20 milioni.  Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) ilitoa Sh30 milioni, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Sh30 milioni, Mfuko wa Pensheni wa PSPF Sh20 milioni na Mnyika alitoa Sh2milioni na kuahidi kutoa Sh milioni moja kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano.

Benki ya CRDB ilinunua katika mnada wa kuchangisha fedha za ujenzi huo, picha ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa Sh35milioni. Rais ndiye aliyeendesha mnada wa picha hiyo.


[ Read More ]

Posted by newstz.blogspot.com 0 comments»

Mashuhuda mkataba wa Richmond waibuka

Ni wanasheria Dk Tenga, Makia wa Tanesco

Na Mwandishi wetu

WAKATI Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) likibanwa kuilipa Kampuni ya Dowans Sh 111 bilioni, wanasheria walioshuhudia mkataba kati za kampuni hizo, wameibuka na kusema ni kawaida migogoro inayojitokeza kwenye makubaliano kama hayo, kusuluhishwa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Biashara (ICC).

Wanasheria hao wameeleza kuwa mikataba mingi ya kimataifa ina kipengele kilichoweka bayana kwamba migogoro inayojitokeza inasuluhishwa na ICC.

Walisisitiza kuwa kipengele kilichopo katika mkataba wa Richmond na Tanesco kinachoeleza kwamba iwapo mgogoro baina ya pande mbili utatokea lazima upelekwe ICC, ni jambo la kawaida katika mikataba ya kimataifa.

Kauli ya Dk Tenga
Wakili wa kujitegemea kutoka Kampuni ya Law Associates, Dk Ringo Tenga ambaye alitia saini mkataba huo Juni 23, 2006 kama shahidi wa Kampuni ya Richmond, aliliambia Mwananchi Jumapili katika mahojiano maalumu kuwa wawekezaji wanapenda migogoro yao kusuluhishwa na mahakama hiyo kwa sababu ina uzoefu wa masuala ya biashara za kimataifa.

"Kuhusu Tanesco kuingia mkataba na Richmond na kuwepo kipengele cha mgogoro kupelekwa ICC, mikataba mingi ya kimataifa inakuwa na kipengele hicho," alisema Dk Tenga.

Katika kesi iliyofunguliwa na Dowans mwaka 2009 kupinga kuvunjwa kwa mkataba wake iliorithi kutoka Richmond kwenye Mahakama ya kimataifa, kampuni hiyo ilishinda na Tanesco kuamriwa kulipa Sh111 bilioni.

Baada ya hapo Januari 25 mwaka huu Kampuni ya Dowans iliiomba Mahakama Kuu isaijili tuzo hiyo. Hata hivyo, Tanesco ilipinga. Mahakama Kuu ya Tanzania katika hukumu yake Septemba 28 mwaka huu, iliyosomwa na Jaji Emilian Mushi, ilikubali kuisajili tuzo ya ICC na Tanesco kutakiwa kulipa kiasi hicho cha fedha.

Jaji Mushi, alisema mahakama hiyo haina uwezo wa kuingilia maamuzi ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya kibiashara iliyotoa tuzo hiyo, Novemba 15, mwaka jana.

Kwa mujibu wa mkataba huo, waliotia saini kwa upande wa Kampuni ya Richmond ni Mkurugenzi wake, Mohammed Gire na Tanesco iliwakilishwa na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji, Johannes G. Loterring (Net Group Solution).

Dk Tenga, alisema wawekezaji wengi wanahofia kama mkataba usipokuwa na kipengele cha matatizo yao kumalizwa na ICC, wanaweza kupoteza haki yao kutokana na uhaba wa wataalamu wa sheria katika mahakama za kawaida.

Alisema ugeni katika sekta ambayo mwekezaji anawekeza pia unaweza kuwa moja ya sababu ya kuamua migogoro itakayoibuka na mtu aliyeingia naye mkataba, iende ICC.

Mtaalamu huyo wa sheria alisema kupeleka migogoro ya usuluhishi katika mahakama za kawaida mara nyingi hutumia muda mwingi na pengine kulazimika mahakama kutafuta utaalamu katika eneo hilo.

Alitoa mfano wa mgogoro wa kibiashara ambao ulitokea kati ya Kampuni ya Microsoft ya Marekani na kampuni zingine ambazo zilikuwa zikifanya biashara na kampuni hiyo kwamba kesi yake baada ya kupelekwa katika mahakama ya kawaida, iliwafanya mahakimu kuhitaji muda zaidi kujua undani wa masuala ya sekta hiyo.

Dk Tenga alisema: "Katika kesi hiyo ili mahakama kupata uwezo wa kuisikiliza ilibidi mahakimu waende kupata elimu ya mambo ya ‘software’ hali ambayo ilichelewesha zaidi kumaliza kesi hiyo tofauti na kama wangekwenda ICC."

Alisema kutokana na hali hiyo, ndiyo maana wawekezaji wa nje hupendelea wanapoingia mikataba kuwa na kipengele kinachoeleza kuwa migogoro ikitokea, lazima ipelekwe Mahakama ya Usuluhishi wa Kimataifa.

"Ninachotaka kusema ni kwamba, si jambo la ajabu mkataba wa mwekezaji kuwa na kipengele cha usuluhishi wa mgogoro kupelekwa ICC," alisema Dk Tenga ambaye pia ni Mhadhiri mstaafu wa Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Alisema kila sekta ina chombo kinachosimamia usuluhishi wake, akitoa mfano jinsi migogoro katika sekta ya habari nchini inavyopelekwa Baraza la Habari Tanzania (MCT) kusuluhishwa badala ya mahakamani.

Dk Tenga alisema hajaisoma hukumu ya Jaji Mushi kuhusu tuzo ya Dowans, lakini kama kuna kipengele ambacho Tanesco inaona kimekiukwa katika hukumu hiyo, wanaweza kukata rufaa Mahakama ya Rufani.

Alisema sheria ya usuluhishi nchini sura ya 15, inaeleza wazi kuwa unaweza kukata rufaa kupitiwa upya hukumu kama msuluhishi aliyesikiliza kesi hiyo kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi, alisikiliza upande mmoja, hakuweka kumbukumbu sawasawa maelezo ya ushahidi au msuluhishi alikuwa na mgongano wa kimaslahi katika kesi hiyo.

Dk Tenga, alisema lakini kama aliamua kesi hiyo kulingana na misingi ya kisheria, huwezi kukata rufaa ukashinda.

Alisema Tanesco lazima itafakari kwanza uamuzi wa kukata rufaa kwani sheria zote zinafahamika.Hata hivyo, Dk Tenga aliishauri Serikali kuwa wakati wa kuingia mikataba mikubwa kimataifa, lazima ifuate weledi wa watalaam.

Alisema kila sekta ina utaalamu wake hivyo, wakati inapoingia mikataba hiyo, lazima itafute wanasheria wenye ujuzi na sekta hiyo.

Mtalaam huyo wa sheria alisema kuwa, kabla ya kuingia mkataba mikubwa ni vyema kwa sasa serikali ikawatumia washauri wa kukodi kutoka Benki ya Dunia na Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola ambao wana uzoefu wa muda mrefu.

Vilevile, aliishauri serikali kurejesha utaratibu wa kupeleka wanasheria wake kusoma kwenye Chuo cha Kimataifa cha Maendeleo ya Sheria (IDLI) kilichopo Italia kama ilivyokuwa ikifanya miaka ya nyuma ili kuwaongezea uwezo kwenye mikataba ya kimataifa.

"Zamani wanasheria wengi wa mashirika ya umma walikuwa wakipelekwa IDLI Rome, Italia kusomea masuala ya mikataba," alisema na kuongeza:

"Wanasheria wanatakiwa kuwa na uelewa mpana kuhusu masuala ambayo wanaingia mikataba."

Kuhusu wanaharakati na baadhi ya wanasiasa ambao wanaoshinikiza wale walioingia mikataba hiyo kulipa fedha hizo, Dk Tenga ambaye alikuwa shahidi wa Kampuni ya Richmond wakati wakiingia mkataba huo, alisema watu hao wana haki ya kusema hayo lakini suala hilo ni la kisheria.

"Suala hili ni la kisheria sio la mtu kusema tu," alisema na kuongeza : "Kama wanaona kuna eneo ambalo bado lina udhaifu kisheria, waende mahakamani badala ya kulizungumza tu."

Dk Tenga ambaye alisema anazungumza kama mwanasheria, alionya kuwa shinikizo la kisiasa kutolipa fedha hizo bila ya kufuata sheria, linaweza kuifanya Serikali ibanwe kwa kutaifishwa mali zake.

Alisema endapo Tanesco kwa sasa itakata rufaa na kushindwa kesi hiyo halafu ikagoma kulipa, mahakama itaamuru mali zake kutaifishwa au wahusika kufungwa kwa kosa la kudharau mahakama.

Mwanasheria wa Tanesco
Kwa upande wake, Mwanasheria wa Tanesco, Godson Makia, ambaye alitia saini mkataba huo kama shahidi wa shirika hilo, aliiambia Mwananchi Jumapili kuwa wanatafakari kuona kama watakata rufaa katika siku 60 ambazo wamepewa na mahakama kisheria.

Alisema, wanapitia hukumu ya Mahakama Kuu kuona kama kuna kipengele ambacho hakikuwekwa sawa na mahakama hiyo ili wakate rufaa Mahakama ya Rufani.

Makia ambaye alikuwa shahidi na Mwanasheria wa Tanesco aliyesaini mkataba wa Richmond, alisema kwanza wataangalia hukumu kuona kama kulikuwa na makosa wakati wakusikilizwa kesi hiyo au tafsiri ya kisheria haikuzingatiwa, ndipo wakate rufaa.

Hata hivyo, alikiri kuhusu kipengele katika mkataba huo kinachotaka usuluhishi wa mgogoro wowote kati ya pande hizo mbili lazima upelekwe kusikilizwa ya ICC kwa maelezo kuwa kinawafunga.

Makia alisema mara nyingi kwenye mikataba ya wawekezaji wa nje kuwepo kipengele kinachobainisha kuwa migogoro itakayoibuka ipelekwe mahakama ya ICC, kwani huichukulia mahakama hiyo kama kinga yake.


Kuhusu wanaharakati na wanasiasa ambao wanaoshinikiza waliosaini mkataba huo kulipa tuzo hiyo ya sh bilioni 111, Makia alisema hawaelewi masuala ya sheria ndiyo maana wanasema hivyo.

Aliongeza: "Wanaharakati wanaweza kusema chochote, lakini sheria ndio tunayotakiwa kuifuata."

Wanaharakati mahakamani
Septemba 6, mwaka huu, wamiliki wa Kampuni ya Dowans walishinda kesi iliyofunguliwa Mahakama Kuu ya Tanzania na wanaharakati nchini, kupinga kulipwa tuzo yake ya Sh94 bilioni.

Wanaharakati hao ambao walidai kuwa wameamua kupinga usajili wa tuzo hiyo kwa maslahi ya umma ni pamoja na Kituo cha Msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Wengine ni Chama cha Wanasheria wa Mazingira (LEAT) na Kampuni ya Sikika (Sikika Company Limited- CL). Taasisi hizo ziliwakilishwa na wakili, Dk Sengondo Mvungi pamoja na mwanahabari Timothy Kahoho.

CHANZO: MWANANCHI
[ Read More ]

Posted by newstz.blogspot.com 0 comments»