Bunge lavunjika Dodoma

Dar/Dodoma. Kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana usiku kilivunjika baada ya vurugu kutawala ukumbini humo.
Vurugu hizo zilianza saa 04:42 usiku hadi saa 04:49 usiku wakati Spika Anne Makinda alipolazimika kuahirisha Bunge hadi leo saa tatu asubuhi.
Chanzo cha vurugu ni kutokana na ugumu wa kutokukubaliana na azimio la tisa, lililolenga kumwajibisha moja kwa moja Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Azimio la PAC lilitaka Waziri Muhongo aadhibiwe kwa kufukuzwa kazi kutokana na tuhuma zilizokuwa zinazomkabili ikiwamo kulidanganya Bunge.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge wengi wakiwa wa CCM walitaka waziri huyo asiadhibiwe... Soma zaidi
[ Read More ]

Posted by newstz.blogspot.com 0 comments»

Kenya yatoa uzoefu kwa Bunge la Katiba

Ujumbe maalum kutoka nchini Kenya umehutubia wajumbe wa Bunge la Katiba nchini Tanzania kuelezea uzoefu wao kuhusu mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya nchini Kenya ulivyofanyika.
Akizungumza na Wajumbe wa Bunge maalum la katiba, Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Kenya,Amos Wako ameainisha masuala ya msingi ya kuzingatia katika upatikanaji wa Katiba mpya ya Tanzania.
Bwana Wako ameeleza uzoefu wake wa upatikanaji wa katiba ikizingatiwa kuwa wakati mchakato wa kupata katiba mpya nchini Kenya alikuwa miongoni mwa watendaji wakuuu wa mchakato huo akiwa mwanasheria mkuu wa serikali. soma zaidi

[ Read More ]

Posted by newstz.blogspot.com 0 comments»

Chadema yampitisha Mathayo Torongey kupambana na Ridhwani Kikwete

Mgombea Ubunge wa Chalinze kwa tiketi ya Chadema, Mathayo Torongey akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana baada ya kutambulishwa. Picha na Michael Jamson Read More


[ Read More ]

Posted by newstz.blogspot.com 0 comments»

Mgombea Ubunge kwa tiketi ya CCM jimbo la Kalenga ahutubia kwenye mvua, wananchi wavumilia

 Mgombea Ubunge Jimbo la Kalenga kwa tiketi ya chama cha Mapinduzi (CCM),Ndugu Godfrey Mgimwa akiwa amebebwa juu na mmoja wa wanakijiji,mara baada ya kumaliza kuhutubia mkutano wa kampeni wa uchaguzi mdogo wa jimbo hilo,uliofanyika katika kijiji cha Wenda kata ya Mseke-Iringa Vijijini,huku kukiwa na mvua kubwa ikinyesha,ambayo hata hivyo haikuzuia kufanyika kwa mkutano huo.Wananchi wa Kijiji hicho walionekana kuw ana shauku kubwa ya kutaka kumsikiliza Mgombea huyo bila kujali kulowana na mvua.Uchaguzi unatarajiwa kufanyika Machi 16.

[ Read More ]

Posted by newstz.blogspot.com 0 comments»

Kura ya Siri au wazi kaa la moto Bunge la Katiba

Na Daniel Mjema na Sharon Sauwa, Mwananchi


.......Habari kutoka katika kikao cha ndani cha Chama Cha Mapinduzi (CCM), zilisema kutokana na mvutano huo, mjumbe mmoja, Chritopher Ole Sendeka, alijikuta akilia hadharani akitetea upigaji kura ya wazi.
Dodoma. Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, juzi na jana wamekuwa katika mtihani mgumu wa kufikia uamuzi wa pamoja kuhusu utaratibu wa upigaji kura, kati ya kura ya wazi na kura ya siri.

Habari kutoka katika kikao cha ndani cha Chama Cha Mapinduzi (CCM), zilisema kutokana na mvutano huo, mjumbe mmoja, Chritopher Ole Sendeka, alijikuta akilia hadharani akitetea upigaji kura ya wazi.

Kikao hicho kilichofanyika juzi kati ya saa 2:00 na saa 5:30 usiku chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kilishuhudia mabishano makali kati ya wanaotaka kura ya siri dhidi ya wale wanaotaka kura ya wazi.

Habari hizo zilisema baada ya Pinda kufungua kikao hicho, alimkaribisha Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM, Shamsi Vuai Nahodha, ili atoe mrejesho wa kikao cha mashauriano.

Inaelezwa kuwa katika kikao hicho, Nahodha aliwaambia wajumbe kuwa kutokana na mazingira yaliyopo ndani na nje ya Bunge kwa upande mmoja na wananchi kwa upande mwingine, kura ya siri haiepukiki.

“Kilio cha Ole Sendeka kwenye party cocas kikao cha chama (party cocus) juzi usiku kilitokana na kauli ya Nahodha kwamba kura ya siri haiepukiki,” alidokeza mbunge mmoja wa CCM aliyehudhuria kikao hicho cha faragha.

Mbunge huyo alilidokeza gazeti hili kuwa ndani ya kikao kulikuwa na mabishano makali baada ya kauli ya Nahodha, huku baadhi ya wabunge wakisema wananchi wamechoshwa na msimamo wa CCM.

Ni kutokana na mabishano hayo ndipo Ole Sendeka aliposimama akipinga mapendekezo yaliyotaka CCM kulegeza msimamo na kuridhia kura ya siri na wakati alipokuwa akizungumza alipobubujikwa na machozi.

Huku akilia katika kikao hicho, inadaiwa Ole Sendeka akisema kwamba kukubali kura ya siri ni kuitosa CCM na msimamo wake wa kutaka muundo wa Serikali mbili.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho, zilidai kuwa Ole Sendeka alienda mbali zaidi na kusema endapo Pinda ataridhia kura hiyo ya siri, basi yeye (Pinda) na viongozi waandamizi wa CCM waliohudhuria watawajibishwa na CCM.

Kutokana na mtafaruku huo, kikao hicho kilishindwa kufikia mwafaka na kuahirishwa hadi jana saa 5:00 asubuhi ambapo hoja ya ama kura ya siri au ya wazi, iliendelea kuwagawa wabunge katika makundi mawili.

Wakati akifungua kikao cha jana, Pinda alisema kutokana na yaliyotokea katika kikao chao cha juzi usiku na baada ya kutafakari kwa mapana yake, chama kimeamua kibakie na msimamo wake wa kura ya wazi.

“Kutokana na yaliyojitokeza jana (juzi) na hasa ukiona mtu mzima analia, tumetafakari tumeona tubaki na msimamo wa kura ya wazi,” alisema mmoja wa wabunge akimkariri Waziri Mkuu Pinda.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, katika kikao hicho ilielezwa kuwa kukubali upigaji kura wa siri ni kuiua CCM kwa sababu wajumbe wengi wa Bunge Maalumu la Katiba, watapitisha muundo wa Serikali tatu badala ya mbili.
Katika hatua nyingine, baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, wamehoji kitendo cha Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hilo, Pandu Ameir Kificho kuhudhuria kikao cha ndani cha wabunge wa CCM.
“Kificho ni mwenyekiti wa Bunge lenye makundi tofauti, sasa anapoingia kwenye kikao cha wabunge wa CCM kinachoweka mikakati ya kupingana na makundi mengine anatoa picha gani?” alihoji mbunge mmoja.
Taarifa za Kificho kuhudhuria kikao hicho cha jana cha CCM zilionekana kuwakera wajumbe wengine wa Bunge hilo, wanaotokana na vyama vya upinzani na wale wanaotoka katika kundi la wajumbe 201.
“Bado tunatafakari tuchukue uamuzi gani, lakini tukiona vipi, tutasusia kikao cha leo (jana) jioni, nyie njooni ndani lolote linaweza kutokea,” alidokeza mjumbe huyo anayetoka katika kundi la vyama vya hiari.
Kura ya siri, wazi yawekwa kiporo
Hata hivyo, jana mara baada ya Kificho kuanza kikao cha semina saa 10:40 alasiri badala ya saa 9:00 alasiri alisema semina hiyo imechelewa kuanza kwa sababu ya masuala muhimu.
Kificho aliwaambia wajumbe kuwa kamati ya mashauriano ilikuwa imemshauri kanuni ya 37 na 38 zinazohusu kura ya siri viwekwe kiporo kutokana na kutopatikana kwa mwafaka.
“Kamati imenishauri bado tuache kanuni ya 37 na 38 ili kamati ya mashauriano iendelee kunishauri vizuri zaidi ili baadaye tuje tuwaambie kamati ya kanuni iziandike vipi,” alisema.
Kutokana na ombi hilo, wajumbe waliafiki waendelee kupitia kanuni ya 32 hadi 36 na 39 hadi 43 ambavyo havina mvutano.
[ Read More ]

Posted by newstz.blogspot.com 0 comments»

OXFAM YAIVURGA LOLIONDO

*Yazifadhili asasi kuvuruga amani Loliondo
*Yazichotea mamilioni kufanikisha vurugu

Shirika la Misaada la Kimataifa la Oxfam limejiingiza kwenye ufadhili wa vikundi na asasi za kiraia, zinazozua na kuchochea mgogoro kati ya Serikali na wafugaji wa jamii ya Kimaasai katika Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha.
Kujiingiza kwa Oxfam ni juhudi za asasi za Tanzania zilizo na baadhi ya raia wa kigeni, kuhakikisha kuwa Loliondo haitawaliki. Pia ni mwendelezo baada ya kukwama kwa baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Ulaya ambao mwaka jana walijiingiza huko kinyemela hata bila kuitaarifu Serikali ya Mkoa wa Arusha.

Habari za uhakika zilizopatikana kutoka Arusha zimesema kwamba shirika hilo limetoa mamilioni ya shilingi zilizowezesha baadhi ya asasi hizo kukutana mjini Arusha wiki iliyopita. Fedha hizo, pamoja na kuwawezesha viongozi na wanachama wa asasi hizo, zinatumika pia kulipia matangazo na propaganda katika vyombo vya habari.

Asasi zilizo katika mkakati huo ni mtandao wa wanaharakati wa haki za binadamu (FEMA CT), mtandao wa mashirika yanayotetea haki za wafugaji, wawindaji na wachuma matunda nchini (PINGO’s Forum), mtandao wa utetezi wa masuala ya ardhi (TALA), na shirika lisilo la kiserikali lililopo Ngorongoro (NGONET).

Asasi hizo kwa mara ya kwanza kwenye tamko lake, kwa vyombo vya habari mwishoni mwa wiki, zimetamka wazi kuunga mkono harakati za kuichafua Tanzania zinazoendeshwa kwenye mtandao.

“Kutokana na hayo, sisi mashirika yanayojishughulisha na utetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania, tunaunga mkono kampeni za mtandao wa kimataifa wa Avaaz,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Kufanyika kwa mkutano wa pamoja wa asasi hizo kumekuja baada ya hivi karibuni Rais wa Oxfam Ireland, Monica Gorman, na viongozi wengine wa shirika hilo kuzuru Ngorongoro bila kuwataarifu viongozi wa Serikali ngazi ya mkoa.

Akiwa Loliondo, Gorman alijaribu kuibua tatizo “lisilokuwapo” na kutaka wananchi wanaoishi hapo wasibughudhiwe. Kimsingi anapinga kusudio la Serikali ya kuandaa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi katika vijiji vya Loliondo. Mpango huo umelenga kuainisha maeneo ya malisho ya mifugo, maeneo ya uhifadhi wanyamapori, maeneo ya kilimo, na shughuli nyingine za kijamii.

Akiwa katika Kijiji cha Arash kilicho karibu na Loliondo, aliwataka wanavijiji wawe makini katika kuingia mikataba na kampuni kwa maelezo kwamba watapoteza ardhi yao.

Wengine waliokuwa kwenye msafara huo ni Mkurugenzi Mkuu wa Oxfam, Jim Clarken; Mwenyekiti wa Kamati ya Uhusiano wa Mambo ya Nje wa Bunge la Ireland, Jim Wells, na Pat Breen, ambaye ni Mbunge.

Mwenyejiti wa Arash, Kiaro Orminis, aliueleza ujumbe huo kwamba kuna matatizo ya ardhi katika eneo hilo, hasa unaohusisha Kijiji cha Malambo na kampuni ya uwindaji wa kitalii ya Ortello Business Corporation (OBC).

Kwa muda sasa, mgogoro katika eneo la Loliondo ulikuwa umetulia hasa baada ya wananchi kuelimishwa juu ya umuhimu wa kupanga matumizi bora ya ardhi.

Utulivu huo umekuwa ukiathiri mapato ya asasi zinazojitanabaisha kuwa zinawatetea wafugaji, ilhali zikiwa hazifanyi juhudi za kutosha katika kuwasaidia wananchi hao.

Kampeni ya hivi karibuni ilipamba moto kwenye mtandao wa Avaaz, ikidai kwamba Serikali ilikuwa mbioni kuwahamisha wafugaji wa Kimaasai kutoka Serengeti. Taarifa hiyo ilipingwa vikali na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii.

Taarifa ya Serikali ya Agosti 15
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Khamis Sued Kagasheki, amekanusha uvumi unaosambazwa na shirika moja kupitia mtandao wake wa AVAAZ.org kuwa Watanzania wa jamii ya Kimaasai wapatao 48,000 watahamishwa kutoka eneo lao (la Serengeti), kupisha wafalme kutoka Mashariki ya Kati ili walitumie eneo hilo kwa uwindaji wa simba na chui.

Taarifa hiyo iliyosambazwa na mtandao huo imewataka watu kutoka duniani kote kujiorodhesha ili wafikie angalau 150,000, ili kumshinikiza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuacha kusaini mkataba utakaofanya uhamisho huo utekelezwe.

Waziri Kagasheki amesisitiza kuwa uvumi huo si wakweli na hauna msingi wowote kutokana na sababu zifuatazo:

Kwanza, hatua kama hii haiwezi kuchukuliwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Hifadhi ya Serengeti maana hakuna watu wanoishi ndani ya hifadhi hiyo. Pia kitendo hicho hakijapangwa kufanyika katika Wilaya ya Serengeti iliyoko mkoani Mara.

Pili, hata kama taarifa hiyo ilimaanisha Wilaya ya Serengeti mkoani Mara bado si yakweli maana wilaya hiyo haina idadi ya Wamaasai wanaofikia jumla ya 48,000.

Tatu, ndani ya ya Hifadhi ya Serengeti hakuna eneo lolote lililotengwa kwa ajili ya wafalme wa Mashariki ya Kati, ili waweze kulitumia kwa uwindaji wa simba na chui.

Nne, habari hizo si za kweli maana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hahusiki kabisa na ugawaji wa vitalu vya uwindaji popote pale nchini. Hii ni kazi ya Wizara ya Maliasili na Utalii, na Wizara haijafanya hivyo katika eneo tajwa.

Pamoja na ufafanuzi huo, Waziri Kagasheki amewaasa watu waliojiorodhesha na wanaotarajia kujiorodhesha, kuwa wamepotoshwa, hivyo wanatakiwa wasisaini kubariki kitu ambacho hawakijui wala hakipo.

CHANZO - JAMHURI
[ Read More ]

Posted by newstz.blogspot.com 0 comments»

YANGA NA SIMBA WAKABIDHIWA VIFAA NA KILIMANJARO

Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu (kushoto) na Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ (kulia), wakionesha baadhi ya vifaa vya michezo  walivyokabidhiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), ambao ndio wadhamini wakuu wa klabu hizo. Wa pili kushoto ni Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe na Mkurugenzi wa Mashindano, Saad Kawemba. Hafla hiyo ilifanyika katika ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), jijini Dar es Salaam
 
Na Clezencia Tryphone
KLABU kongwe nchini za Simba na Yanga, zimekabidhiwa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya sh milioni 34 kila moja kutoka kwa mdhamini wao mkuu, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager.
Akikabidhi vifaa hivyo katika Ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), jijini Dar es Salaam, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe, alisema, kukabidhi vifaa hivyo ni moja ya sehemu katika mkataba baina yao na klabu hizo.
Kavishe alisema lengo kubwa la kudhamini timu hizo ni kutokana na historia kubwa ya klabu hizo, pamoja na kuleta ushindani wenye burudani kwa Watanzania, ambao ni wadau wakubwa wa kunywa kinywaji hicho.
“Sisi tunafanya kazi vema na klabu hizi, tunajisikia faraja kubwa kutokana na timu hizi kuwa na historia kubwa hapa nchini na ushindani mkubwa katika soka na huu ni udhamini wa nusu msimu peke yake,” alisema Kavishe.
Alivitaja vifaa hivyo walivyotolewa kuwa ni jezi, bukta, soksi, viatu, bips, nguo za kusafiria, vikinga ugoko na mifuko.
Katika hatua nyingine, Kavishe alisema, kuhusu mabasi ya timu hizo, wako katika hatua za mwisho kuyakabidhi kwa wahusika, kwani tayari yamewasili hapa nchini, ambapo kuna mambo kadhaa wanayakamilisha.
Akizungumza kwa niaba ya klabu ya Simba, Makamu Mwenyekiti, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, aliwashukuru wadhamini hao kwa moyo walionao, huku akiwaahidi kuhakikisha wanafanya vema na kushinda ili kuonesha umuhimu wa vifaa ambavyo wamewapa.
“Nawashukuru TBL kwa kutudhamini na kuona umuhimu kwa sisi Simba bila ya kupepesa macho na ndiyo maana hata sisi tutapigana kufa na kupona ili kuhakikisha tunavitendea haki vifaa hivi,” alisema Kaburu.
Kwa upande wa Yanga, Ofisa Habari wake, Louis Sendeu, naye aliishukuru TBL, huku akiwaomba kutoishia kwa Simba na Yanga, bali waziangalie na timu nyingine.
“Tunawashukuru sana ila msiishie kwa Yanga na Simba tu, mziangalie na klabu nyingine ambazo zinasuasua,” alisema Sendeu.
CHANZO : Francis Dande
[ Read More ]

Posted by newstz.blogspot.com 0 comments»

DK MARY NAGU ANG'OKA NEC HANANG'

MBIO za uchaguzi ndani ya CCM zimefikia patamu, baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji) Dk Mary Nagu kuenguliwa kugombea nafasi ya Ujumbe wa Nec kupitia Wilaya ya Hanang', huku Mke wa Rais, Salma Kikwete akiwa mgombea pekee wa nafasi hiyo Lindi Mjini.

Mkoani Dar es Salaam, mbio hizo zimeonekana kuwaweka pabaya Mwenyekiti wa UWT wa mkoa huo Zarina Madabida na Katibu wake, Tatu Maliaga baada ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa, John Guninita kueleza kuwa viongozi hao watafikishwa kwenye kamati ya maadili kueleza kwa nini wamesitisha uchaguzi wilayani Kinondoni.

Habari kutoka Hanang' zimeeleza kuwa Kamati ya Siasa ya CCM ya Wilaya hiyo imemwengua Dk Nagu na kuwabakiza wagombe wawili, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na Leonsi Marmo.

Taarifa kutoka kwenye kikao hicho kilichofanyika juzi katika Ofisi ya CCM ya wilaya hiyo na kuhudhuriwa na wajumbe 12 zimeeleza kuwa Dk Nagu ameenguliwa kutokana na maelezo kuwa kanuni hazimruhusu kugombea.
Chanzo cha habari kimeeleza kuwa kanuni iliyomwondoa Dk Nagu kwenye kinyang’anyiro hicho ni ile inayowataka viongozi wenye kazi za kila siku; ubunge na uwaziri kutogombea.

Imeelezwa kuwa jitihada za wajumbe watano waliojipambanua katika kikao hicho kumtetea Dk Nagu ziligonga mwamba, baada ya wenzao saba kuunga mkono uamuzi huo.

“Kikao kilikuwa kizito, lakini tulitazama zaidi kanuni, sifa za wagombea na uwezo wa wagombea hasa katika nafasi hii nyeti ya Nec kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015,” alisema mmoja wa wajumbe wa kikao hicho.
Alisema mapendekezo ya kikao hicho, tayari yamefikishwa ngazi ya CCM mkoa kwa uamuzi zaidi na baadaye yatafikishwa Kamati Kuu (CC) ya CCM.

“Sisi tumemaliza kazi yetu, tunaamini kuwa tumetenda haki kwa manufaa ya chama chetu Wilaya ya Hanang’,” alisema kiongozi huyo.

Hata hivyo, mjumbe mwingine wa kikao hicho alisema, mgawo wa mkopo wa matrekta ambao umekuwa ukiendelea Hanang’ umechangia kumwengua waziri huyo.

“Hapa kuna mambo mengi, nadhani hao waliokuwa na taarifa hizi, wameshindwa kueleza zaidi. Kuna mambo ya chinichini hasa baada ya baadhi ya viongozi kutounga mkono uamuzi wa Waziri Nagu kusaidia baadhi ya wanaCCM wakiwamo viongozi kukopeshwa matrekta,” alisema mjumbe huyo.

Kiongozi mmoja wa CCM Wilaya ya Hanang’ ambaye hakutaka jina lake litajwe, alikiri kufanyika kwa kikao hicho na kueleza kuwa tatizo la Dk Nagu ni kutoombewa kibali na kamati ya siasa wilaya au mkoa kama kanuni zinavyotaka.
Alieleza kuwa kanuni za CCM zinataka viongozi wenye majukumu ya kila siku kuombewa kibali kwanza na Kamati ya Siasa ya Wilaya au Mkoa kabla ya kugombea jambo ambalo halikufanyika kwa Dk Nagu.

“Hadi kikao hicho kinafanyika, Dk Nagu alikuwa hajaombewa kibali hicho na hili limetokana na migogoro ya kisiasa iliyoko wilayani Hanang’,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu hilo, Katibu wa CCM Wilaya ya Hanang’, Allan Kingazi alisema: “Ni kweli kikao kilifanyika, lakini mapendekezo yetu ni siri na hao waliokuambia wamekiuka kanuni. Sisi baada ya kumaliza kikao chetu, mapendekezo yetu tumeyapeleka ngazi ya mkoa ambako pia yataendelea kuwa siri hadi majina yatakapotangazwa rasmi,” alisema.

Uamuzi wa Dk Nagu kuamua kugombea NEC kupambana na Sumaye ambaye ndiye alimwachia jimbo hilo, ulitabiriwa kuibua mgawanyiko mkubwa ndani ya wana CCM wa Hanang’.
Jitihada za gazeti hili kumpata Dk Nagu kuzungumzia uamuzi huo zilishindikana baada ya simu yake ya mkononi kuita muda mrefu bila kupokewa.

Kuenguliwa kwa Dk Nagu kunatokana na sababu za kuwa na kazi za muda wote kumeibua hofu kuhusu hatima ya viongozi wengine waliochukua fomu ambao kwa mujibu wa kanuni iliyomwondoa Dk Nagu nao hawakupaswa kugombea.
Hao ni pamoja na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika na Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Dk Abdallah Kigoda, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk Emmanuel Nchimbi.

Wengine ni Wabunge Deo Filikunjombe (Ludewa), Mussa Azzan Zungu (Ilala), Dk Hamis Kigwangalla (Nzega) na Andrew Chenge (Bariadi Magharibi).

Salma akosa mpinzani Lindi
Katika hatua nyingine Mke wa Rais, Salma Kikwete amerudisha fomu ya kuwania ujumbe wa Nec Taifa kupitia Wilaya ya Lindi Mjini.

Katibu wa CCM Wilaya ya Lindi Mjini Mohamed Kateva, alisema jana kwamba Salma ni mgombea pekee aliyejitokeza kuwania nafasi hiyo katika wilaya yake.

Kateva alisema mwisho wa kurudisha fomu ilikuwa Agosti 28, mwaka huu na mpaka tarehe hiyo hakukuwa na mtu mwingine aliyekuwa amejitokeza kuwania nafasi hiyo.

Madabida kiti moto

Katika Mkoa wa Dar es Salaam, Madabiba na Maliaga watahojiwa kwa kukiuka uamuzi ya Halmashauri Kuu ya Mkoa.
Viongozi hao wanadaiwa kusimamisha uchaguzi wa UWT Wilaya ya Kinondoni ambao ulipangwa kufanyika Agosti 31, mwaka huu.
Guninita alisema jana kuwa kikao hicho cha Nec mkoa kiliagiza uchaguzi wa jumuiya zote ufanyike kuanzia Agosti 31 hadi Septemba 2, mwaka huu lakini UWT Wilaya ya Kinondoni haikufanya uchaguzi huo.
Alisema katika kikao chake cha Agosti 29, mwaka huu Nec Mkoa kilipitisha wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi katika wilaya zote tatu na kuagiza uchaguzi ufanyike.
“Mwenyekiti wa UWT na katibu wake kwa sababu zao binafsi walisimamisha uchaguzi na kwa mujibu wa katiba yetu hili ni kosa,” alisema Guninita.
Alipotakiwa kuzungumzia madai hayo Madabida alisema: “Nipo kikaoni. Lakini ndani ya chama chetu cha CCM hakuna mtu anayeweza kuusimamisha uchaguzi peke yake.”
Habari hii imeandikwa na Nora Damian, Dar; Mussa Juma, Hanang' na Mwanja Ibadi, Lindi.

 CHANZO - MWANANCHI
[ Read More ]

Posted by newstz.blogspot.com 0 comments»