Basena apika dawa ya African Lyon

KOCHA wa Simba, Moses Basena


DORIS MALIYAGA

KOCHA wa Simba, Moses Basena, amewaandaa nyota watatu kwa ajili ya kubeba mikoba ya Victor Costa "Nyumba" wakati timu hiyo itakapoikabili African Lyon katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa Uwanja wa Taifa kesho Jumapili jijini Dar es Salaam.

Kiungo Patrick Mafisango, ambaye ameifungia timu hiyo mabao manne, ni mmoja wa waliotayarishwa kwa ajili ya kazi hiyo maalum. Wengine ni Jerry Santo, ambaye pia ni kiungo na beki Obadia Mungusa aliyesajiliwa kutoka Mtibwa Sugar.

Watatu hao wamepewa mafunzo maalumu na Basena ili kuziba pengo la Costa, aliyeko nje ya uwanja kutokana na kuumia msuli wa paja, huku kukiwa na pengo pia la Kelvin Yondani aliyeingia mitini na Amir Maftah ambaye ni majeruhi.

Akizungumza kwenye kambi ya timu hiyo iliyoko Bamba Beach, Kigamboni, jijini Dar es Salaam, Basena hakuweka wazi nani hasa atacheza nafasi ya Costa, lakini alieleza ana imani na wote watatu kwa mbinu na mazoezi aliyowapa.

"Kila mmoja wao yuko katika kiwango cha kufanya kazi nzuri ya kutupatia ushindi," alisema Basena ambaye timu yake yenye pointi 18 inataka kuwapiku vinara JKT Oljoro inayoongoza ligi ikiwa na pointi 19.

"Tuna Mafisango, Santo na Mungusa, wanaoweza kucheza nafasi ya Costa, ninachofanya ni kuwaangalia kujua nani kati yao atafaa zaidi,"alisema Basena, ambaye alitamba kuwa timu yake ipo vizuri kutokana na kuwa katika kambi tulivu na kufanya wachezaji kushika haraka kile anachofundisha tofauti na wakiwa mjini penye vurugu nyingi.

Basena kwa sasa anakuna kichwa kusaka mtu wa kucheza na Juma Nyosso, ambaye ndiye beki pekee mzoefu aliyesalia kufuatia kutoweka kwa Yondani, ambaye katika siku za karibuni hajakuwamo katika mipango ya Basena.

Wakati Nyosso akiwa na Taifa Stars huko Morocco, Basena aliwachezesha kwa vipindi tofauti Mungusa na Shomari Kapombe, Jerry na Mungusa kwa nafasi hiyo ili kuangalia kombinesheni.
Alipofanya hivyo, Mafisango alicheza nafasi ya kiungo mshambuliaji wakati timu hiyo ilipotoka sare ya bao 1-1 na Azam kwenye mechi ya kirafiki iliyochezwa asubuhi ya Jumatatu iliyopita.

Basena alidokeza pia anawaangalia wachezaji waliokuwa katika mashindano ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.

Wachezaji hao ni Juma Kaseja na Nassor Said "Chollo" waliokuwa na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, pamoja na Gervais Kago aliyekuwa na kikosi cha Afrika ya Kati.

Alisema kuwa anawafuatilia wachezaji hao kisaikolijia kuona kama hawajaathirika baada ya timu zao kushindwa kufuzu kutinga fainali hizo zitakazochezwa mwakani huko Gabon na Guinea ya Ikweta.

Akizungumzia mchezo dhidi ya African Lyon, Basena alisema kuwa ana matumaini makubwa ya ushindi kwani ameishaipeleleza timu hiyo, ambayo inashika nafasi ya 11 ikiwa na pointi tisa.
"Si kwamba African Lyon ni mbovu, lakini nilivyoiona inafungika tu," alisema Basena, ambaye alikuwapo uwanja wa Chamazi wakati Lyon ilipofungwa na Kagera Sugar mabao 2-1.

Kuhusiana na majeruhi, Basena alieleza kuwa Salum Machaku na Mwinyi Kazimoto wanakaribia kurejea uwanjani. Ambao hali zao bado ni Costa na beki wa kushoto, Amir Maftah, ambaye pengo lake uwanjani litazibwa na Juma Jabu.

Katika mechi nyingine ya Ligi Kuu leo Jumamosi, Azam itaikaribisha JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Chamazi, ulio nje kidogo ya Dar es Salaam.
Azam inatazamiwa kumrejesha uwanjani raia wa Ivory Coast, Kipre Tchetche, ambaye kwa muda sasa amekuwa majeruhi.

Categories: ,