KUNA taarifa za kutatanisha juu ya afya ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, huku baadhi ya vyanzo vikidai amelishwa sumu.
Taarifa zilizozagaa jana kupitia simu na mitandao mingine ya kijamii, zilidai kwamba kutokana na hali tete aliyokuwa nayo jana, mipango ilikuwa inafanyika kumsafirisha nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Awali, taarifa zilisema amelishwa sumu; baadaye zikaja nyingine kwamba Dk. Mwakyembe amekula chakula kichafu kikamsababishia kuvimba mwili mzima.
Hata hivyo, gazeti hili lilipowasiliana na mmoja wa wadogo zake mkoani Mbeya, alisema taarifa hizo zilikuwa za kuzusha, kwa sababu za kisiasa.
Baadaye zilipatikana taarifa kutoka kwa ndugu zake wa karibu waliosema kwamba mbunge huyo wa Kyela hakulishwa sumu, bali anaumwa tu kawaida, na kwamba anaendelea vizuri.
Gazeti hili halikufika nyumbani kwake, na lilipomtafuta kwa simu iliita bila kupokewa, baadaye ikazimwa kabisa.
Chanzo kimoja cha habari kilichodai kimefika nyumbani kwake Kunduchi Beach, Dar es Salaam, kilisema: “Kwa kweli afya yake ni mbaya sana. Wizara inafanya mipango akachunguzwe nje ya nchi.”
Wakati hayo yakisemwa kuhusu Dk. Mwakyembe, katika hali isiyokuwa ya kiungwana, uvumi mwingine ulizagaa kuhusu afya inayodorora ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Prof. Mark Mwandosya, ambaye yupo India kwa matibabu.
Baada ya kuibuka tetesi kuhusu afya yake, huku nyingine zikienda mbali na kudai huenda amepoteza maisha, Profesa. Mwandosya alisikika akizungumza na mwandishi wa Radio One, akakanusha uvumi huo.
Katika mahojiano hayo ya simu, Profesa Mwandosya alisema uvumi huo unamwongezea maisha. Alisema anaendelea vizuri, akawashukuru wote wanaomwombea.
“Mimi ninaendelea vizuri, ni kwamba ukiona mtu anakutangazia kifo, basi ujue anakutakia maisha marefu… kwa sisi waumini na watu wa dini tunaamini hilo, hivyo ni jambo la heri, tunaomba waendelee kutuombea maisha marefu na hakuna mtu anayejua siku yake ya kufa… nimeshauriwa niwe karibu na wataalamu … vipimo vikikamilika nitatibiwa na kurudi nyumbani muda si mrefu,” alisema Profesa Mwandosya.
CHANZO: TANZANIA DAIMA