NAPE ASEMA WAMEPENYA TUNDU LA SINDANO
Na Efracia masaweCHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimekiri kuwa hakikustahili kushinda katika uchaguzi mdogo uliomalizika jimboni Igunga mwanzoni mwa mwezi huu.
Badala yake, kilisema waliopaswa kushinda ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambacho kilikuwa kinaungwa mkono na wananchi wengi.
Hata hivyo, CCM imedai kwamba ushindi wake Igunga umetokana na CHADEMA kutumia vitisho, ikiwamo kumkamata na kumwadhibu Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario, aliyekutwa anakula njama za ushindi wa CCM.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, katika mkutano wa mapokezi ya mbunge aliyechaguliwa, Dk. Peter Kafumu, katika viwanja vya Bakhresa, Manzese, Dar es Salaam.
Dk. Kafumu alishinda kwa tiketi ya CCM kwa kura 26,484 dhidi ya 23,260 za mgombea wa CHADEMA, Joseph Kashindye. Vyama vingine sita, kikiwamo CUF, vilipata kura chache sana ambazo katika jumla yake hazifiki hata 2,800.
Nape alisema: “Kama CHADEMA wasingejihusisha na vitendo vya kikatili, basi leo hii chama hicho kingekuwa madarakani. Nakiri wazi kuwa CHADEMA wangeweza kuchukua kura zaidi ya 5,000 Igunga…
“Tumeshinda kupitia tundu la sindano, hiyo ipo wazi kabisa… CHADEMA waliwateka wananchi kwa asilimia zote. Kosa lao la kwanza waliwakashifu siku moja kabla ya kupiga kura kwa kuwaleta wasomi ili waje wahesabu kura kwa usahihi, hapo ndipo tatizo lilianza.”
Alisema CHADEMA ilikuwa imewateka wananchi wa Igunga, lakini baadaye walikerwa na kitendo cha chama hicho kuingiza walinzi wa kura kutoka nje ya jimbo.
“Nawahakikishieni baadhi ya wanachama waliokerwa na kitendo hicho cha kutokuaminiwa, kiliwafanya kundi kubwa la wanachama hewa wakichague chama cha CCM, tukaongezewa kura, ” alisema Nauye.
Naye Mbunge wa jimbo hilo, Dk. Kafumu alitumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wote waliomchagua na akaahidi kuwa nao bega kwa bega katika ufanisi wa kazi.
“Nitawatumikia bila ubaguzi wa chama au mtu yeyote. Nawashukuru kwa kila jambo na Mungu awabariki katika shughuli zenu; naomba tuendelee kushikamana,” alisema Kafumu
Categories:
ccm,
chadema,
igunga,
nape,
urais 2015