Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Uendeshaji wa Benki ya Exim Tanzania Eugen Massawe (kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) Dar es Salaam leo juu ya benki hiyo kuingia katika mfumo mpya wa teknolojia ya huduma kwa wataeja wao iliyoanza kutumika tangu Oktoba 17 mwaka huu.Katikati ni mmoja wa maofisa wa benki hiyo Jacqeline Kweka na kulia ni Meneja Masoko na Mahusiano wa benki hiyo Linda Chiza.
Na Mwandishi Wetu
Benki ya Exim Tanzania imekamilisha mikakati yake ya kubadilisha mfumo wa teknolojia wa huduma zake ambapo kuanzia Oktoba 17 mwaka huu imeingia katika mfumo wa kisasa wa teknolojia utakaoboresha huduma za jumla za kibenki kwa wateja wake.
Mabadiliko ya teknolojia ndani ya benki hiyo sasa yanawawezesha wateja husika kupata huduma za kibenki kwa mtandao wa Internet, kulipa kodi mbalimbali za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kufanya malipo ya biashara kwa mtandao katika maeneo tofauti ya nchi kwa pamoja na ulipaji wa ada za shule na hudumu nyinginezo za kibenki bila ulazima wa kwenda benki.
Mkuu wa kitengo cha huduma za uendeshaji wa benki hiyo Eugen Massawe alisema leo jijini Dar es Salaam kuwa hatua hiyo inalenga kuongeza ufanisi wa huduma zake wakiamini teknolojia hiyo itakuwa mfumbuzi wa kuduma katika uboreshaji wa huduma zao.
Alisema wakati wote wamekuwa wakichukua hatua madhubuti katika kuhakikisha wateja wao wanapata huduma bora na za kuridhisha na kwamba wamekuwa mhimili katika ufumbuzi na kutumia teknolojia za kisasa katika kuhakikisha huduma zao zinakwenda haraka.
"Katika muendelezo wa nguvu ya kibenki kuimarisha huduma zetu, tumelazimika sasa kutoka na kuingia katika matumizi ya kisasa ya uwanja wa matumizi ya teknolojia (IT) katika huduma zote muhimu za benki",
"Teknolojia hiyo mpya pamoja na kuwa itasaidia kuboresha huduma za ndani ya benki lakini pia itatuwezesha kuzalisha huduma nyingine bora na za kisasa kwa wateja wetu", alisema Massawe.
Aliongeza kuwa benki tayari ilitoa angalizo kuhusu kuingia katika teknolojia hii siku chache zilizopita na kwamba mabadiliko hayo yamekamilika na sasa tayari yameingia katika mfumo wa huduma za kibenki.
Alitoa nafasi kwa wateja wote kuwasiliana na tawi lao lolote kama kutakuwa na uhitaji wa kupata taarifa zaidi au msaada katika kipindi hiki cha matumizi ya teknolojia ya kisasa kwa wateja.
Benki ya Exim ni miongoni mwa benki za kizalendo zenye mafanikio makubwa ikiwa na matawi 21 katika maeneo mbalimbali nchini na matawi mengine matatu nje ya Tanzania.
Categories:
exim