Kinondoni kukusanya bilioni 4.5/-

Imeandikwa na Oscar Job


BARAZA la Madiwani la Kinondoni, limeafiki urejeshwaji wa ada za leseni huku ikitarajia kukusanya zaidi ya kiasi cha Sh bilioni 4.5 zitakazotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Meya wa Manispaa hiyo Yusuph Mwenda, alisema uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha madiwani hao cha Oktoba 8, mwaka huu na utaanza kutekelezwa Januari mwakani.

Alisema uamuzi huo uliafikiwa ili kutekeleza mwito wa Serikali Kuu wa kurejesha ukusanyaji wa ada za leseni kwa mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuzingatia Sheria ya Fedha.

Mwenda alisema malengo makuu ya kurejeshwa kwa ada hizo ni pamoja na kuimarisha usimamizi wa biashara, kuzijengea uwezo wa mapato mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na kuwa na takwimu sahihi za wafanyabiashara wote.

Kuhusu viwango vya ada vitakavyotozwa, Mwenda alisema vitazingatia viwango vilivyokuwa vikitumika mwaka 2004 kabla ya kufutwa kwa ada hizo na mtaji wa wafanyabiashara uliogawanyika katika makundi matatu, wafanyabiashara wakubwa, wadogo na wa kati.

“Kwa kuzingatia hali halisi ya Jiji la Dar es Salaam na changamoto zake, halmashauri haitatoza ada za leseni za biashara katika maeneo ambayo siyo rasmi, kama vile mama lishe, machinga na gereji bubu,” alisema Mwenda.

Alisema sababu za kutowatoza ada kwa wafanyabiashara hao ni kuepuka kuwaidhinisha katika maeneo hayo kwa kuwa si maeneo rasmi yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli hizo.

Mapendekezo hayo yanatarajiwa kuwasilishwa kwa Katibu Tawala wa Mkoa (RAS), ambaye kwa mujibu wa taratibu zilizopo ndiye atakayewasilisha Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na baadaye Wizara ya Viwanda na Biashara itayapitia na kutoa uamuzi ili itumike kwa mujibu wa sheria.

CHANZO: HABARI LEO

Categories: