Na Ellen Manyangu
UTAFITI umebainisha kwamba kati ahadi 235 alizotoa Rais Jakaya Kikwete mwaka jana wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu, asilimia 10 zimetekelezwa.Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Agenda Participation 2000 (AP2000), ilitoa ripoti jana ikieleza tathmini ya hali ya nchi na mahitaji ya wananchi baada ya uhaguzi mkuu, uliopita.
Mbali na hayo wageni walioalikwa katika uzinduzi wa ripoti ya kitabu ‘Tamko la Wananchi Tanzania: Taifa letu, uongozi wetu, ahadi na mahitaji ya wananchi’, hawakutokea na kusababisha kitabu hicho kutozinduliwa. Mmoja wa wageni hao alikuwa ni Professa Max Mmuya ambaye alitoa taarifa kuwa alikuwa mgonjwa.
“Tunaomba radhi sana kwa kilichotokea, mgeni rasmi anaumwa na mimi nimechelewa kwenye foleni, hivyo uzinduzi wa kitabu hiki umeshindikana, mpaka hapo tutakapowatangazia tena,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa AP2000, Moses Kulaba.
Ripoti hiyo inafafanua kwamba Rais Kikwete alitoa ahadi 80 za papo kwa hapo nje ya ilani ya chama na ahadi 155 ambazo zilikuwa kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).Msingi wa utafiti huo ulizingatia kuwapa nafasi wananchi wa kawaida kutambua na kufuatilia kazi za kiongozi aliyeko madarakani ili kubaini jinsi zinavyotekelezwa.
“Hii itamsaidia mwananchi wa kawaida kujua na kufanya maamuzi mazuri katika chaguzi zijazo kwa kuona na kufahamu uongozi uliopita ulivyotenda kazi zake,” alisema Kulaba.Kulaba alisema kitabu hicho kimetungwa ili kuwaongezea wananchi uwezo wa elimu ya uraia yenye kusaidia ushiriki katika uendeshaji wa nchi.
Kitabu hicho pia kimeeleza mbinu ambazo wananchi wanaweza kuzitumia kuwawajibisha viongozi endapo hawatatekeleza ahadi ambazo walizitoa kama vile kutowachagua katika uchaguzi ujao.
Ripoti hiyo ilifafanua kwamba ahadi za CCM kwenye Ilani yake kwa sekta ya Kilimo, Uvuvi na Ufugaji zilikuwa 23 na ahadi alizotoa kwenye sekta wizara ya viwanda zilikuwa 15. Sekta zingine na ahadi zake kwenye mabano ni Nishati na Madini (34), Miundo mbinu (6), Ajira na Uwezeshaji wananchi (7), Huduma za jamii (5), Elimu (32) Afya (22)na Huduma za maji (7).Watafiti wa ripoti hiyo walisema kwamba wamefanya utafiti kwa chama tawala kwa kuwa kipo madarakani na kuviacha vyama vingine vya siasa.
Categories: