Yanga yampigia 'magoti' Manji




Na Suleiman Mbuguni

UONGOZI wa Klabu ya Yanga, umwendikia barua aliyekuwa mfadhili wao, Yusuf Manji ili arudi tena kuokoa jahazi.Akizungumza Dar es Salaam jana Mwenyekiti wa
Yanga, Lloyd Nchunga alisema Manji kujiweka pembeni ameacha pengo kwani tangu alipoondoka hakuna mfadhili mwingine yeyote aliyejitokeza.

"Napenda kuwaeleza kwamba tumekuwa na majadiliano ya muda mrefu na mfadhili wetu wa zamani, ndugu Yusuf Manji ambaye alijitoa katika kuifadhili klabu na kubaki kuwa mwanachama wa kawaida mtiifu.

"Hili limetokana na ukweli kwamba pengo lake limekuwa ni dhahiri katika kuiendeleza Yanga, na kipindi chote alichoondoka hakuna mfadhili wa aina yake aliyewahi kujitokeza japo wakorofi wachache walimbeza," alisema Nchunga.

Alisema ingawa wana mikakati endelevu ya kujitegemea kama kuuza vifaa vyenye logo ya Yanga, ambapo wameingia mkataba na Kampuni ya Nsejjere Sports Wear, lakini bado wanamhitaji Manji kwa kuwa ndiye amekuwa chachu ya maelewano na maendeleo ndani ya klabu hiyo.

Nchunga alisema anawaomba wana-Yanga kuonesha upendo kwa Manji ili aweze kurudi na kuifadhili tena klabu hiyo.

Mwenyekiti huyo alisema katika ufadhili wake Manji, alichangia mambo mengi makubwa ndani ya Yanga, ikiwemo kuleta muafaka uliodumu kwa kipindi kirefu.

Alisema ana imani Manji atakubali ombi lao kwa kuwa katika majadiliano naye, alionekana kukubali lakini ametaka muda wa kulitafakari na kupata ushauri kutoka kwa familia yake na watu wake wa karibu.

Alisema hata hivyo, Manji ametaka kukutana kwanza na Kamati ya Utendaji ya Yanga, ili kuwekana mambo sawa.

"Hivi sasa Manji hayupo nchini, yupo Marekani lakini atakapokuja nitawaomba wana-Yanga kwenda kumpokea na kumkaribisha kwa upendo kwa kuwa anarudi na kusherehekea siku yake ya kuzaliwa," alisema.

Alisema kwa wale wanaotaka kwenda kumpokea uwanja wa ndege kesho, wanaweza kufanya hivyo.

Categories: