VIONGOZI WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA PAMOJA NA VYOMBO VYA HABARI KATIKA KUTOA TAARIFA MUHIMU.



NA SALAMA NJANI-BEIJING CHINA       

Viongozi wa mataifa mbali mbali duniani wametakiwa kuwa tayari kufanya kazi kwa pamoja na vyombo vya habari hasa katika kutoa taarifa muhimu zinazohusu jamii,siasa,utamaduni na uchumi.

Hayo yameelezwa leo na Rais wa China Central Television (CCTV) Ling Ju wakati wa mkutano wa kwanza wa kimataifa kwa vyombo vya habari na watumiaji wa vyombo vya habari uliofanyika katika ukumbi wa Media Centre Hotel uliopo mjini Beijing China.

Amesema kuwa vyombo vya habari vinawajibika kubeba jukumu la kutangaza kwa kina taarifa zinazohusu maisha ya watu ya kila siku, ikiwemo mafanikio na changamoto zinazoukabili uchumi wa dunia.

Ling Ju amesema watu wote duniani wanategemea vyombo vya habari kama ni mhimili mkuu,kujua hali ya kupanda na kushuka kwa uchumi kwa kina, ili kubuni mbinu mpya za kupambana na maisha.

 Amefahamisha kuwa masuala ya siasa,jamii,utamaduni na uchumi duniani, yanachukua nafasi kubwa katika maisha ya kila siku ya  mwanadamu, hivyo ni jukumu la vyombo vya habari kuhakikisha vinafanya kazi yakukuza uelewa wa watu kuhusu mambo hayo muhimu.

 Amesisitiza kuwa mashirikiano na nguvu ya kutosha kutoka kwa viongozi yanahitajika,pamoja na uhuru wa kutoa taarifa muhimu zikiwemo za uchumi,ambapo kwa sasa vyombo vya habari vinakabiliwa na changamoto sugu ya kutokuwa na uhuru wa kufanya kazi zao ipasavyo.

 Amesema hakuna chombo chochote cha habari kinachoweza kufanya kazi na kufanikiwa peke yake bila ya mashirikiano ya viongozi wa nchi husika, wanajamii ambao ni walengwa pamoja na vyombo vyengine vya habari vya kimataifa.

 Akizungumzia mafaninikio ya CCTV tokea kuanzishwa kwake mwaka 1958 amesema kupitia vituo na chanel zake mbali mbali imefanikiwa kuunganisha nchi nyingi duniani zikiwemo za Afrika katika kutoa habari muhimu kwa jamii sambamba na matumizi ya teknolojia mpya za kupata habari.

Katika mkutano huo ambao unazishirikisha nchi zaidi ya thelathini ni wa kwanza kufanyika, ikiwa ni mikakati ya kuweka mashirikiano ya nchi nyingi duniani kihabari pamoja na kujua umuhimu wa jamii katika upashaji wa habari.
            
 IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR 20/10/2011