Waangalizi waibua utata walioandikishwa Igunga

Na Tumaini Makene

SIKU chache baada ya kumalizika kwa uchaguzi mdogo Jimbo la Igunga na mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Dalaly Kafumu kuibuka mshindi, kimeibuliwa
kitendawili juu ya idadi halisi ya wapiga kura walioandikishwa kushiriki shughuli hiyo na ukiukaji mkubwa wa taratibu.

Akizungumza na Waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Mtandao wa Asasi za Kiraia Tanzania (TACCEO) inayojumuisha asasi zipatazo 17 chini ya uratibu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Bi. Martina Kabisama alisema matatizo hayo yalibainishwa na waangalizi wao waliokuwepo katika kata 25 kati ya 26 za Jimbo la Igunga.

"Tulibaini mapungufu katika daftari la kudumu la wapiga kura, tulielezwa na Tume ya Uchaguzi Jimbo la Igunga kwamba takwimu zitakazotumika ni zile zilizotumika katika uchaguzi mkuu, 2010.

Idadi ya wapiga kura walioandikishwa mwaka 2010 ilikuwa ni watu 177,077. Tarehe 3/10/2011 tulisomewa idadi ya wapiga kura walioandikishwa ni 171,019. Tofauti ya idadi kwa walioandikishwa ni 6,058," alisema Bi. Kabisama.

Kwa mujibu wa Bi, Kabisama, kutoboreshwa kwa daftari hilo kungelikosesha wananchi wengi haki yao ya kupiga kura, mathalani wale ambao mwaka jana walikuwa hawajatimiza umri wa kupiga kura au waliohamia.

"Tunaiomba Tume ya Uchaguzi itusaidie ni lini daftari la wapiga kura liliboreshwa. Pia tulishuhudia idadi kubwa ya wapiga kura waliokuwa wakiomba msaada wa kupigiwa kura...wengine walikuwa wakiandika maneno kwenye karatasi ya kura. Kwa mfano waliandika 'kaliwe', 'nabado' na maneno mengine ya matusi," alisema Bi. Kabisama.

Alisema waangalizi wao walokuwepo tangu ufungaji wa kampeni na kufika katika vituo 410 siku ya upigaji kura, walibaini masuala mbalimbali ambayo TACCEO wameyatolea mapendekezo kwa ajili ya kuboresha chaguzi zijazo.

Mwenyekiti huyo ambaye alikuwa akiwasilishaji muhtasari wa ripoti ya awali ya waangalizi wa ndani wa uchaguzi huo alisema waangalizi wao walifanya kazi hiyo kwa mwezi mzima tangu Septemba 4, 2011 hadi Oktoba 4, 2011.

Alisema mbali ya mkanganyiko huo juu ya uhalisia wa idadi kamili ya wapiga kura pia uchaguzi huo uligubikwa na ukiukwaji haki za binadamu akitolea mfano wa kudhalilishwa kwa mkuu wa wilaya hiyo huku vyama viwili vikubwa vya CCM na CHADEMA vituhumiwa kukiuka maadili ya uchaguzi kwa kufanya kampeni siku ya uchaguzi.

Alisema kulikuwa na vitendo vya rushwa katika uchaguzi huo na kudai kuwa shahada za kupigia kura zilikuwa zikibadilishwa kwa vitu kama vile fulana na fedha taslimu kati ya sh.10,000 hadi 15,000.

Alisema wakati hayo yakifanyika maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) walishindwa kufanya kazi yao katika moja ya matukio kwa madai ya kutumia gari aina ya Suzuki ambayo isingeweza kufua dafu katika barabara mbovu yenye umbali wa kilometa takriban 90.

Bi. Kabisama alisema katika uangalizi wao huo walibaini pia kuwepo kwa idadi kubwa ya wasiojua kusoma na kuandika huku baadhi yao wakibainika kufanya udanganyifu kwa malengo yasiyojulikana.

Alisema walipobanwa kwa kuombwa vitambulisho vyao vilionekana wametia saini ya maandishi na si ya dole gumba ambayo hutiwa na watu wasiojua kusoma na kuandika, hivyo kutia shaka kama kweli hawajui kuandika au walielekezwa kufanya hivyo.

"Waangalizi wetu walishuhudia ununuzi wa mapanga 30 kwa wakati mmoja, vurugu zilizotokea Hoteli ya Kilimanjaro Lodge saa nne asubuhi tarehe 3 (Oktoba), wafuasi waliokuwa wamevalia sare za kijani na njano walitumia mapanga, upinde na mishale, visu, fimbo na marungu na wengine waliokuwa mchanganyiko walitumia mawe, mmoja akijihami kwa kuonesha bastola, pia kumwangiwa tindikali, afisa mtendaji kata kudhalilishwa alisema.

Aliendelea,"Kituo cha Mwamashiga msimamizi wa kituo, alikuwa anatoka nje na kusema Kafumu hana mpinzani.

Alitaja kasoro zingine kuwa ni matumizi mabaya ya watoto katika mchakato wa uchaguzi wakivalishwa skafu kupandishwa magari kwa njia ya hatari na kutangulizwa katika maandamano mbalimbali yaliyokuwa yakiambatana na fujo za kisiasa.

Alisema Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEKNOHAMA) pia haikutumika ipasavyo hivyo kusababisha ucheleweshwaji matokeo na kuibua hisia za uchakachuaji na vurugu eneo la kuhesabia kura.

Majira ilipomtafuta Msimamzi wa Tume ya Uchaguzi (NEC) Igunga kwa njia ya simu, Bw. Protace Magayane ili kuzungumzia tuhuma hizo alisema hawezi kuzungumza lolote kwa sasa kwa kuwa uchaguzi umekwisha na sasa anaandaa taarifa.

"Mimi sasa hivi naandaa taarifa kuwasilisha kwa Mkurugenzi wa NEC, uchaguzi umekwisha sasa watafuteni wagombea wataongea si mimi," alisema Bw. Magayane.

Alipobanwa kuwa yeye ndiye msemaji wa mwisho kwa mujibu wa sheria kuhusu masuala yote ya uchaguzi huo alisema "Labda naweza kuongea au nitafute baada ya kuwasilisha taarifa ila sasa mtafute MNkurugenzi wa Tume,"alisema.

CHANZO: MAJIRA

Categories: