EDUCATION AND LITERACY 50 YEARS AFTER INDEPENDENCE: REFLECTIONS FOR ACTION 28-30th NOVEMBER 2011 SAVE THE DATE




!










Taasisi ya Usomaji na Maendeleo--
Soma
S.L.P 4460,
Dar es Salaam
Simu: +255754275347
Barua pepe: demeredye@gmail.com
!
Chama cha Wauza Vitabu
Tanzania (BSAT)
S.L.P 80174,
Dar es Salaam
Simu: +255754283866
!
21 NOVEMBA 2011
TAARIFA KWA UMMA
MAJADILIANO YA WAZI JUU YA ELIMU NA KUFUTA UJINGA
Mazungumzo ya kisera miaka 50 ya Uhuru: Hatua na mstakabali wa
elimu na kufuta ujinga nchini Tanzania.
Taasisi ya Usomaji na Maendeleo ya E&D —Soma na Chama cha Wauza Vitabu wa Tanzania
(BSAT) zinajihusisha na harakati za kufuta ujinga kwa njia ya kuhimiza usomaji na maendeleo ya
vitabu. Dira ikiwa ni kuiona Tanzania ikitimiza malengo yake ya maendeleo kama ilivyojiwekea
katika malengo ya milenia na MKUKUTA. Tunaamini jambo hili linaweza kufanikiwa kama
tutatafakari kwa umakini mstakabali wa elimu yetu: falsafa, ruwaza, na utendaji kwa kuzingatia
ubora, ushiriki, rasilimali, uendeshaji na vipaumbele inavyowekewa.
Katika kutimiza hilo, taasisi hizi zimeandaa, kama muendelezo wa Tamasha la VIitabu, mjadala wa
wazi utakaofunguliwa jumatatu ya tarehe 28 Novemba 2011 na kufungwa jumatano tarehe 30
Novemba 2011 muda ukiwa ni saa 11:00 jioni hadi saa 4:00 usiku kwa siku zote ili kutafakari hatua
zilizopigwa na wadau mbalimbali katika elimu na kufuta ujinga ndani ya miaka hamsini baada ya
uhuru wa Tanganyika. Majadiliano haya yatafanyika katika viunga vya Mkahawa wa Vitabu Soma
(Mtaa wa Regent Estate, Kitalu Na. 53, Mlingotini Close) kama sehemu ya Tamasha la Vitabu.
Madhumuni ya majadiliano haya ni kutoa fursa kwa wadau mbalimbali wa elimu: wanajamii,
waelimishaji, watekelezaji na watunga sera, wanataaluma, wanazuoni, pamoja na wanafunzi,
kutafakari kwa kina kuhusu juhudi za wananchi na Serikali tangu enzi za Mwalimu Nyerere katika
kufuta ujinga kama mojawapo ya maadui watatu wa maendeleo yetu.
Mdahalo utafanyika jumanne tarehe 29 Novemba 2011 huku ukihusisha tafakuri ya kina
itakayofungamana na vionjo vya kisanaa, ukiwaleta pamoja wadau wenye stadi, mitazamo, na
uzoefu mbalimbali katika elimu kuzungumzia hatua tuliyopiga katika maendeleo ya elimu na
juhudi za kufuta ujinga. Maswali makuu yatakuwa: “kipi tumefanya vyema?”, “kipi tungeweza
kufanya vyema zaidi?” na “nini tunahitaji kufanya?” ili ndani ya muongo mmoja tuweze kuwa
mfano bora wa jamii inayojua kujifunza.
Mbali na hivyo, kuanzia jumatatu yatakuwa yakifanyika matukio kwa ajili ya jamii nzima kama vile
maonesho ya vitabu na huduma za kielimu, vionjo vya kifasihi kama vile mashairi, ngonjera,
ngano; shughuli za kuchangisha fedha kwa ajili ya huduma za kielimu ikiwemo ujenzi wa maktaba
za jamii na mashindano ya fasihi kwa wanafunzi wa shule ya sekondari, mnada wa vitabu
vilivyotumika, maonesho ya muziki, dansi, nyama choma, na vinywaji.
Hivyo basi, tunatoa rai kwa jamii nzima na watu wote wahudhurie kwa wingi bila kukosa kwa siku
zote tatu ili kuja kubadilishana mawazo na watu wengine wenye maono na mitazamo tofauti
kuelekea kuboresha hali ya elimu nchini. Hapatakuwa na kiingilio chochote kwa siku zote tatu.
! ! ! ! ! !
Demere Kitunga-(SOMA)
!
Hobokela Magale-(BSAT)

Categories: