NEC: UCHAGUZI MDOGO JIMBO LA ARUMERU MASHARIKI KUFANYIKA APRIL MOSI MWAKA HUU

Uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Arumeru Mashariki unatarajiwa kufanyika April Mosi mwaka huu.
Uchaguzi huo utafanyika baada ya jimbo hilo kuwa wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wake Marehemu Jeremia Solomon Sumari aliyefariki dunia Januari 19 mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa na Tume ya Taifa ya uchaguzi leo jijini Dar es salaam imesema pamoja na uchaguzi huo mdogo pia kutakuwepo na chaguzi ndogo za madiwani katika kata za Halmashauri mbalimbali nchini.
Taarifa hiyo ya Tume ya Taifa ya uchaguzi inaonesha kuwa katika uchaguzi mdogo wa ubunge kwenye jimbo la Arumeru Mashariki uteuzi wa wagombea utafanyika Machi 8, na kampeni zitaanza Machi 9 hadi 31 mwaka huu.
Aidha, Tume hiyo pia itafanya chaguzi ndogo za madiwani katika kata nane zilizoko katika halmashauri mbalimbali nchini kufuatia kuwepo wazi kwa nafasi za viti vya madiwani ambazo zimetokana na vifo vya madiwani husika.
Katika chaguzi ndogo za madiwani uteuzi wa wagombea utafanyika Machi 5 na kampeni zitaanza Machi 6 hadi 31 mwaka huu. Kata zitakazohusika kwenye uchaguzi huo ni zile vijibweni-Temeke, Kiwanga-bagamoyo, Kirumba-Mwanza, Logangabilili-Bariadi, Chan’gombe-Dodoma, Kiwira-Rungwe, Lizaboni-Songea na Msambweni-Tanga.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Damian Lubuva imesema kuwa hakutakuwa na kuandikisha wapiga kura kwa ajili ya chaguzi hizo ila daftari la kudumu la wapiga kura lililotumika wakati wa uchaguzi mkuu uliopita litatumika.
Tume inawasisitiza wananchi na vyama vyote vya siasa kuzingatia na kufuata ratiba ya uchaguzi na kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mchakato wa uchaguzi kuanzia siku ya uteuzi wa wagombea, kampeni za uchaguzi na siku ya kupiga kura. Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa 1.00 asubuhi na kufungwa saa 10.00 alasiri

Categories: