Habari na Boniface Meena
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kinahofu kuwa chaguzi za jumuiya zake zinazotarajia kufanyika mapema mwakani, zinaweza kutumiwa na baadhi ya makada wake kujiimarisha kwa ajili ya mbio za urais 2015 hivyo kuzidi kuongeza mpasuko.
Kutokana na hofu hiyo, chama hicho kimependekeza kuwekwe utaratibu wa kudhibiti hali hiyo na kuhakikisha kuwa mgombea urais wa CCM mwaka 2015, hatokani na nguvu ya fedha aliyonayo wala makundi aliyojitengenezea.Hayo yamo kwenye waraka namba 4(B) ulioandaliwa na Idara ya Oganaizesheni ya chaka hicho kwenda mkutano wa Halmashauri Kuu (NEC) uliofanyika Dodoma, Novemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa waraka huo ambao Mwananchi umefanikiwa kuuona, CCM imesema baadhi ya wanachama wake, wameanza kupigana vikumbo kwa ajili ya kumrithi Rais Jakaya Kikwete huku wengine wakijipanga kutumia chaguzi za ndani kujisafishia njia.Chama hicho kimekiri kuwa kina mpasuko mkubwa ndani yake, unaotokana na mambo matatu; harakati za uchaguzi 2015, kura za maoni ya ubunge 2010 na mapokeo ya mageuzi ndani ya chama hicho.
“Wana CCM wengi na Watanzania kwa ujumla, wanaamini kwamba moja ya vyanzo vya migawanyiko ndani ya chama, ni kuibuka kwa makundi ya harakati za kugombea urais mwaka 2015,”unafafanua waraka huo.Imesema, harakati hizo za kuwania urais mwaka 2015, ni chanzo kikuu cha mpasuko ndani ya chama hicho, ingawa hadi sasa hakuna mwana CCM aliyekwishatangaza nia ya kuwania kiti hicho.
Katika waraka huo, CCM imeendelea kueleza kwamba inaaminika baadhi ya wana-CCM wenye nia ya kuomba nafasi ya kuwania urais 2015, wameanza harakati za kutengeneza makundi ya kuwaunga mkono miongoni mwa viongozi na wanachama na hivyo kutengeneza makundi ndani ya chama hicho tawala.
Sakata la kujivua gamba
Kuhusu mapokeo ya mageuzi ndani ya chama, waraka huo umesema, baada ya kutangaza uamuzi wa kujivua gamba, kumekuwapo na harakati za makundi ndani ya chama kujipanga kwa ajili ya kupata uamuzi wanaoutaka, hali ambayo pia, inasababisha kuongezeka kwa mgawanyiko.
CCM katika waraka huo ilisema kwamba, kati watuhumiwa wanaotakiwa kujiuzulu, wapo ambao inaaminika wana dhamira ya kuwania urais mwaka 2015, kwa maana hiyo, kuondolewa katika uongozi wa chama kunatafsiriwa na wao kwamba ni njia ya kuwaondoa katika mchakato huo.
"Wengine wanaamini kwamba iwapo zoezi la kuwaondoa kwenye uongozi watuhumiwa hao litafikiwa, basi watakuwa wamepunguza kihunzi kwenye dhamira yao," imeendelea sehemu ya waraka huo.
Hata hivyo, CCM ilisema mageuzi ndani ya chama yana maana pana zaidi ya kuwafukuza uongozi wanachama watatu. Ni dhana endelevu ambayo haiwezi kumalizika katika kikao kimoja cha NEC, umeeleza waraka huo.
Hali kisiasa
Waraka huo umeelezea pia kwamba hali ya kisiasa ndani ya chama hicho si shwari kwa kuwa kumekuwepo na migogoro ya kiuongozi, migawanyiko, kutokuelewana, kutokupendana na kuhasimiana baina ya viongozi katika baadhi ya mikoa na wajumbe wa Nec.
Categories: